NA JIMMY KIANGO-DSM
Moja ya njia za mafanikio ya kila binadamu ni uthubutu na uwezo wa kuyatazama mambo katika sura tofauti na vile yanavyotazamwa na wengi kwa mazoea. Ni kwa bahati mbaya Watanzania wengi hawapendi kuzibadili changamoto kuwa fursa, badala yake wanazigeuza kuwa matatizo, hali inayochangia kwa kiwango kikubwa kushindwa kupiga hatua za kimaendeleo na kuishia kuilalamikia serikali.
Wataalamu wa mambo wanaamini kila changamoto ama tatizo linapojitokeza mahali, nyuma yake linakuwa limebeba fursa. Miongoni mwa matatizo yaliyobeba fursa ni changamoto ya Mabadiliko ya Tabia nchi, kwa sasa dunia inakabiliwa na tatizo hili na linasababisha athari kila kukicha katika mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Miongoni mwa athari zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi ni jua kuwaka kupita kiasi, joto kuongezeka, mafuriko, vimbunga na majanga mengine mengi. Athari hizi zimewafanya wananchi wengi kulitazama jambo hili kwa mtazamo hasi.
Palipo na mtazamo hasi, kamwe hapawezi kuonekana fursa , hata hivyo hali ni tofauti kwa Afisa Wanyamapori Mkuu na Mratibu wa Maliasili, Mazingira na Mabadiliko ya Tabia Nchi, kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bi. Hawa Mwechaga, yeye analitazama tatizo hilo kama fursa kubwa ya kiuchumi, ambayo imeshaanza kuwanufaisha baadhi ya watu ndani na née ya nchi.
Mwechaga, anasema ipo haja ya jamii kuelemishwa juu ya fursa zinazopatikana katikati ya tatizo la mabadiliko ya tabia nchi, ambapo pamoja na kujiingizia kipato lakini pia mtu anashiriki moja moja kutunza misitu, hatua inayoepusha kasi ya ongezeko la tatizo hilo.
Anasema yapo baadhi ya maeneo yameanza kunufaika na biashara ya Hewa Ukaa na serikali imekuwa mdau mkubwa wa kuhakikisha biashara hiyo inafanyika katika maeneo mengi yenye misitu ya asili. Alisema mbali ya misitu, lakini pia mabaki ya chakula na uchafu mwengine uaozalishwa majumbani ambao unatazamwa kama vitu vinavyoweza kuchafua mazingira na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi, ni bidhaa adimu inayoweza kumuingizia mtu kipato.
“Hivi tunajua kama uchafu tunaouzalisha kutoka kwenye shughuli zetu za kila siku nyumbani ni fursa kubwa, kama tutabadilisha mawazo yetu na kuiona hela.
“Kama tutaweza kutenganisha mabaki ya chakula na taka ngumu na kuyahifadhi vizuri ni wazi tutaweza kujiingizia kipato kwa kuuza taka hizo, yapo maeneo hapa Dar es Salaam, yameanza kufanya biashara hiyo.”
Mwechaga ameyasema hayo leo Juni 6,2024 kwenye mdahalo ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa Mradi wa Kupunguza Migongano Baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania, unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani kwa ufadhili wa (BMZ).
Mdahalo huo uliofanyika kwenye Hoteli ya Colosseum, jijini Dar es Salaam ulilenga kuwapa nafasi wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuileza jamii kile ambacho serikali kwa kushirikiana na wadau wake wamefanikiwa kukifanya katika kukabiliana na migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori kwenye ukanda wa Ruvuma.
Alisema utunzaji wa misitu utasaidia kujiepusha na mambo mengi ikiwa ni pamoja na migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori.
“Eneo la msitu linalotunzwa na kulinda maana yake liko salama, hii inamaanisha kuwa wanyamapori hawawezi kutoka kwenye maeneo yao kwenda kutafuta chakula na maji kwenye makazi ya watu, kwa sababu vitu vyote hivyo watavipata kwenye maeneo yao.”
FURSA ZILIZOPO
Miongoni mwa fursa zinazotokana na ujio wa mabadiliko ya tabia nchi ni biashara ya Hewa Ukaa, mabaki ya chakula na makopo.
BIASHARA YA HEWA UKAA NI NINI?
AFRINEWS SWAHILI lilifanya mahojiano na mmoja wa watalamu wanaohusika na biashara ya Hewa Ukaa ambaye hakutaka jina lake kuandikwa, alisema ili uweze kufanya biashara hiyo ni lazima uwe rafiki wa mazingira na hasa misitu iliyokuzunguka ambayo ina uwezo mkubwa wa kufyonza na kuhifadhi hewa ukaa na hewa sumu.
Kitendo cha kuhakikisha unakuwa rafiki wa misitu ya asili kwa kuilinda, kuitunza, na kuwafanya matumizi salama ya misitu na kuhakikisha hakuna uharibifu wowote unaofanyika kunatoa fursa kwa mtu au kikundi cha watu kujitengenezea mazingira mazuri ya kujiingizia kipato.
Mtaalamu huyo alisema mdau mkubwa wa biashara hiyo ni Kituo cha Carbon Tanzania, ambacho kikijiridhisha na mwenendo wa kutunza misitu ya asiliwao wanafanya kazi ya kutafuta wateja duniani.
Hela itapatikana kutoka kwenye ruzuku inayotolewa kwa watu wanaofanya kazi ya kuilinda, kuitunza na kuihifadhi misitu hiyo ya asili, lakini pia watanufaika na mauzo ya hewa ukaa baada ya kuvunwa.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika iliyopo mkoani Katavi ni mnufaika wa biashara hii na wananchi zaidi ya 21,000 kutoka katika vijiji vinane wamenufaika na mradi wa hewa ukaa.
Wanakijiji hawa walitafutiwa mteja, ambae aliivuna na kulipwa kiasi cha shilingi milioni 380 kupitia kituo cha Carbon Tanzania chini ya mradi wa Ntakata Mountains Redd Plus.
Kwa umoja wao wananchi wa wilaya hiyo wamekubaliana kuzuia uharibifu wa aina yeyote ile kwenye misitu yao, ambapo pamoja na mambo mengine wanataka iwasaidie kuepukana na mabadiliko ya tabia nchi, kufyonza hewa ukaa na hewa sumu iliyo katika anga.
Vijiji hivyo mwaka 2020/21 viliweza kuvuna jumla ya tani 82,000 za hewa ukaa na kuziuza kwa thamani ya shilingi milioni 250,000,000. Biashara hii inaweza kufanyika popote pale nchini penye misitu, jambo la muhimu ni kuhakikisha wahusiki hawafanyi uharibifu wowote wa misitu yao.
Kwenye mabaki ya chakula na makopo, jamii inaweza kunufaika kwa kuhifadhi malighafi hizo katika mazingira salama na zipo taasisi zinanunua mabaki hayo na makopo kwa ajili ya kuzalisha vitu mbalimbali vikiwemo vyakula vya kuku.
0 Comments