Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo ya Nbs yaliyoandaliwa na IUCN mkoani Tanga
NA SIDI MGUMIA, TANGA
Shirika la Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira
(IUCN) limetoa mafunzo maalum
kwa wadau wa mazingira yenye lengo la kujua kwa kina umuhimu wa uhifadhi wa
maeneo ya bahari na namna bora ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mafunzo hayo ya siku mbili, yaliyofanyika mkoani Tanga hivi
karibuni ni sehemu ya Mradi wa Uhifadhi mzuri wa maeneo
makubwa ya bahari kwa ajili ya maendeleo endelevu ya watu, hali ya hewa na viumbe (ReSea) unaotekelezwa
na shirika la Mission Inclusion (Mi) na IUCN nchini Comoro, Kenya, Madagascar,
Msumbiji na Tanzania.
Mradi huo unalenga kuimarisha uwezo wa kustahimili
hali ya kijamii na kiuchumi kwa watu wanaoishi katika jamii za pwani na
kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Ofisa Programu
Mwandamizi wa IUCN, Wendy Atieno alisema kuwa shirika hilo limedhamiria
kujikita katika kupaza sauti na kuwajengea uwezo washirika wa
ndani na watunga sera kuhusu umuhimu wa kutumia suluhu za asili (Nature based
Solutions-NbS) kwa ajili ya kukabiliana
na hali ya mazingira ya bahari ili kuunga mkono jitihada za kusawazisha na
kuzuia uharibifu wa mazingira kwa ujumla.
“Jukumu letu ni kutoa mafunzo haya ambayo yameundwa kwa ajili ya wadau katika nguzo zote tatu (Sayari ya Bluu, Mazingira ya Bluu na Watu wa Bluu), lengo likiwa ni kuwasaidia wadau kuelewa suluhu zinazotegemea asili kama mbinu muhimu ya kukabiliana na uharibifu wa mfumo wa ikolojia na kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa,” alisema Atieno
Aliongeza kuwa lengo lingine ni kuelewa jukumu la NbS
katika mkakati wa jumla wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kuelewa
kiwango cha NbS kinachofaa na vigezo maalum ndani ya kiwango kinachohitajika
pamoja na kuelewa jinsi ya kujitathmini na NbS.
Kwa
mujibu wa IUCN, NbS ni hatua za kulinda, kudhibiti na kurejesha mifumo ya asili
na iliyorekebishwa ambayo inashughulikia changamoto za jamii kwa ufanisi na
wakati huo huo kunufaisha watu na asili.
Akifafanua kuhusu mafunzo hayo, Ofisa
Programu-Mabadiliko ya Tabia nchi wa IUCN, Christopher Roy, alisema IUCN kwa sasa
inashughulikia changamoto saba za kijamii ambazo ni kukabiliana na mabadiliko
ya hali ya hewa, kupunguza hatari ya maafa, kudhibiti uharibifu wa mfumo
ikolojia na upotevu wa viumbe hai, afya ya binadamu, maendeleo ya kijamii na
kiuchumi, usalama wa chakula na usalama wa maji.
Roy alisema mabadiliko ya tabia nchi ni sababu kuu ya opotevu wa bioanuai na mabadiliko ya mfumo wa ikolijia hasa katika maeneo ya Pwani na hiyo ni kutokana na uharibifu wa miti ya mikoko, nyasi bahari na matumbawe, hivyo basi ipo haja ya kuelewa athari zilizopo na kufanya bidii kukabiliana na changamoto hizo.
“Tathimini ya kimataifa inaeleza kuwa tuko katika
hatari ya kupotea zaidi ya nusu ya mikoko iliyopo ifikapo mwaka 2050. Kina cha
bahari kuongezeka kimekuwa ni moja ya sababu kubwa sana ya uharibifu wa
mazingira. Bila suluhu ambazo ni za kiasili, athari za mabadiliko ya tabia
nchi, majanga yatakuwa ni makubwa na jamii pia itaathirika zaidi. Lakini
tukitumia NbS katika bayoanuai yetu basi tunatarajia kuongezeka kwa huduma za
ikolojia kama uzalishaji wa misitu na mikoko ambao utasaidia upunguzaji wa hewa
ukaa, kupunguza athari za maafa lakini pia mwanadamu kunufaika na huduma hizo
na kuweza kujikimu kiuchumi na kupambana na mabadiliko hayo,” alisema Roy
Kwa upande
wake Mshauri wa Uvuvi Mkoa wa Tanga, Issa Khatibu, alisisitiza kuwa maeneo ya
mwambao wa Tanga pia yapo katika hatari ya kupanda kwa kina cha bahari hali
inayoathiri mfumo ikolojia na maisha ya jamii za pwani. Katika kukabiliana na
changamoto hiyo serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutekeleza wajibu wake kupitia Mkakati wa
Kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi (NCCRS) wa mwaka 2021-2026.
“Tuna kampeni
za upandaji miti, uanzishwaji wa hifadhi za misitu kwenye ardhi na bahari,
ushirikishwaji wa jamii, kutoa elimu na kushirikiana na washirika wa ndani.
Vita dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa ni kubwa na inahitaji kutumia hatua
sahihi na kujitolea, lazima tuendelee kukarabati, kushirikiana na kuchukua
hatua kwa usahihi ili kulinda mazingira yetu na kupata mustakabali endelevu kwa
watoto wetu na vizazi vijavyo,” alisema Khatibu
Mmoja wa washiriki wa mafunzo, Boniventure Mchomvu
ambaye pia ni Meneja Uendeshaji kutoka taasisi ya Climate Action
Network-International (CAN) ameeleza kuwa ni vyema NbS izingatiwe, misitu
ijirejeshe kwenye hali yake ya asili ili ifyonze hewa ukaa iliyopo kwenye
tabaka la ozoni.
“Kikubwa katika mapambano haya ni tubadilishe namna
tunavyofanya shughuli zetu lakini pia tubadilishe tabia zetu ambapo sera na
vinginevyo vitabadililka vyenyewe,” alisema Mchomvu
0 Comments