Ticker

7/recent/ticker-posts

SERIKALI YAJITOSA KUOKOA SHOROBA 20 TANZANIA

 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kiuruki


NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI

 Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, imetangaza mkakati wa kuokoa shoroba 20 kati ya 61 zilizotengwa ili kuwalinda wanyamapori pamoja na kuondoa migongano baina ya binadamu na wanyama.

 

Katika kuhakikisha dhamira hiyo ya kulinda wanyamapori inafanikiwa wizara pia imeahidi kuchimba mabwawa kwenye maeneo ya hifadhi,  kuwaongezea uelewa Askari wa Wanyamapori pamoja na kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi.

 

Hayo yametangazwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kiuruki katika Tamasha la Utalii lililofanyika wilayani Same mkoani Kilimanjaro mwishoni mwa wiki iliyopita.

 

Dhamira hiyo ya serikali inarandana na ile iliyoanza kutekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) ambayo imewapa mafunzo  waandishi wa Habari za Mazingira ili waandike kwa weledi na tija habari zinazohusu shoroba nchini.

 

Mkurugenzi wa JET, John Chikomo akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari za Mazingira wakati wa mafunzo yaliyofanyika Bagamoyo, mkoani Pwani.

JET inautumia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID), kuwapa waandishi elimu ya kuandika taarifa zitakazo chochea mapambano dhidi ya Uharibifu wa Misitu, Uhalifu wa Wanyamapori, Mabadiliko ya Tabianchi na uhifadhi wa viumbe hai. 

 

JET imelenga kuzifanyia kazi shoroba saba za Kwakuchinja inayoiunganisha Tarangire- Manyara iliyopo wilaya ya Babati na Monduli katika mikoa ya Manyara na Arusha, shoroba ya Kigosi Moyowosi-Burigi Chato inayounganisha Kigosi Moyowosi na Hifadhi ya Taifa ya Burigi iliyopo wilaya ya Biharamulo na kakonko ambayo ni mkoa wa Kagera na Kigoma. 

Shoroba ya tatu ni Nyerere Selous-Udzungwa inayoungana na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa iliyopo Ifakara mkoani Morogoro, shoroba ya Amani-Nilo inayounganisha maeneo ya asili ya Amani na misitu ya hifadhi ya nilo iliyopo wilayani muheza mkoani Tanga ni ya nne.

 

Shoroba ya tano ni ile ya Ruaha Rungwa -Katavi inayoungana na Hifadhi ya Ruaha, hifadhi ya Rungwa, Lukwati, hifadhi ya Pigi na Katavi iliyopo wilayani Chunya mkoani Mbeya.

 

Ruaha Rungwa-Inyonga ambayo inaungana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Rungwa na Inyonga zilizopowilaya ya  Itigi na Sikonge  katika mikoa ya Singida na Tabora ni shoroba ya sita na shoroba ya saba ni ile ya Mahale-Katavi inayoungana na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale iliyopo wilaya ya Uvinza na Katavi iliyopo mkoani Kigoma.

 


Kwa upande wa Serikali Waziri Kairuki alisema kukosekana kwa uangalizi wa kutosha kwenye shoroba kunachangia migongano ya mara kwa mara.

Alisema uvamizi wa maeneo ya Shoroba licha ya kuathiri wanyamapori lakini pia unasababisha migongano baina ya Binaadamu na wanyamapori.

 

Miongoni mwa maeneo ambayo serikali pia itayfanyia kazi ni Shoroba  ya Kwakuchinja iliyopo katikati ya hifadhi za Taifa za Tarangire na Manyara na sasa imevamiwa.

 

Alisema Wizara yake inakusudia kubainisha maeneo yote ya Shoroba kwa kupimwa na kulindwa.

 

"Kama serikali hatufurahii kuona tembo wanakuja kumjeruhi mtu yeyote au kupoteza maisha ya wananchi wetu, tunachokifanya hivi sasa chini ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan tunaangalia kiini au chanzo kinachofanya tembo watokea hifadhini na kuingia kwenye makazi ya watu ni nini," alisema 

Alisema serikali imeendelea kulipa fidia kwa wanaopata shida za wanyamapori ambapo kwa  miaka  mitano imetoa zaidi ya Sh5.9 bilioni kama kifuta jasho na kifuta machozi .

 

" Serikali haiwezi hata kidogo kufidia uhai wa mtu kwani hakuna thamani kwa mwanadamu hivyo tunachokifanya sasa ni kulipa kifuta jasho na kwa wale ambao mazao yao yameathiriwa tayari serikali imetoa Sh1.2 bilioni."

 

Waziri Kairuki alisema, zaidi ya shilingi 462 milioni kwa sasa zipo katika uhakiki na kadiri fedha hizo zitakapopatikana zitalipwa mapema iwezekanavyo kwa wananchi hao.

 

Awali Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la hifadhi za Taifa nchini, Juma Ikuji  alisema TANAPA itaendelea kuboresha mazingira ya hifadhi ili kuvutia watalii na kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na Binaadamu.

 

Ikuji alisema ldadi ya askari wa Jeshi Usu imekuwa ikiongezwa lakini pia doria za mara kwa mara zinafanywa .

 

Kamishna Ikuji pia alisema miundombinu katika hifadhi zote itaendelea kuboresha ikiwepo barabara, maeneo ya kulala watalii na huduma nyingine muhimu kama mawasiliano.

 

Mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni akizungumzia Tamasha Hilo la Utalii la Same alisema litakuwa likifanyika kila mwaka kwa lengo la kuvutia watalii.

Alisema wilaya ya Same imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya Utalii lakini bado havijatangwa ikiwepo maeneo 13 ya Mali kale, Msitu wa Shengena, ndege ambao hawapatikani eneo lolote duniani, Msitu wa Chome na tamaduni nyingi za asili.

Post a Comment

0 Comments