Ticker

7/recent/ticker-posts

ONGEZEKO LA SHUGHULI ZA KIBINADAMU CHANZO CHA MIGONGANO BAINA YA BINADAMU NA WANYAMAPORI

 

Ofisa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Isaac Yohana Chamba 
NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI-BAGAMOYO
Ongezeko la shughuli za kibidamu hasa kilimo na ufugaji vimetajwa kuwa chanzo kikuu cha migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

 

Ofisa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Isaac Yohana Chamba ndie alieyasema hayo juzi Ijumaa, Februari 23,2024 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, kwenye mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wa kuandika habari za tija Waandishi wa Habari za Mazingira

 

Mafunzo hayo yaliaandaliwa na  Chama Cha Waandishi wa Habari za mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa Mradi wa Kupunguza Migogoro Baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania, unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani (BMZ).

 

Akitolea ufafanuzi suala hilo, Chamba alisema kawaida ya maisha ya wanyamapori ni kuzunguka katika eneo kubwa la mbuga kwa ajili ya kujitafutia chakula na maji na eneo wanalolipata leo hata kama hawatalipita kwa muda mrefu, lakini iko siku watakuja kupita tena kwa ajili ya kujitafutia chakula au maji.

 

“Mfano mzuri ni Tembo, yaani mnyama huyu anahifadhi kumbukumbu na wanafundisha vizazi na vizazi njia zao za kupita, kama walipita mahali na kupata maji na chakula, basi iko siku eneo hilo watakuja kupita tena.

 

“Tembo wanakumbukumbu sana, haijalishi hilo eneo wamelipita lini, wakijikuta wamekosa maji na chakula huko waliko, walizima watahakikisha wanarudi kwenye maeneo ambayo walishawahi kupata huduma hiyo,”alisema Chamba.

 

Aliongeza kuwa hatua hiyo ya Tembo kurui kwenye maeneo yao inaonekana ni kama kuvamia makazi ya binadamu, lakini inakuwa si kweli kuwa wao wamevamia binadamu, bali binadamu ndio wanakuwa wamevamia maeneo ya wanyama.

 

Chamba akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari za Mazingira

Katika miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la shughuli za binadamu katika maeneo mbalimbali ya misitu, lakini pia kasi ya wanyama kurejea kwenye mapito yao ya zamani ni kubwa  hali inayoibua migongano.

 

“Kinachotokea ni mgangano unaosababishwa na ongezeko la shughuli za kibinadamu. Ikumbukwe kuwa ardhi haiongezeki, lakini binadamu wanaongezeka na wanafanya shughuli zinazowazalishia mali, hivyo wanalazimika kuanzisha mashamba na malisho katika maeneo mbalimbali.

 

“Sasa uanzishwaji wa mashamba na malisho mara nyingi hufanyika kwenye malisho ama mapito ya wanyamapori nah apo ndipo migongano inapoubuka, kwani wanyama wanaharibu mazao na wakati mwngine kuua mifugo, huku binadamu nao wakifikia hatua ya kuua wanyama ama kuwajeruhi,”aliongeza Chamba.

 

 

Takwimu za TAWA za wanyama kuingia kwenye makazi na mashamba ya binadamu kwa mwaka 2016/17 zinaonesha kuwa kulikuwa na matukio 833 na mwaka 2027/18 kulikuwa na ongezeko la matukio 164 huku mwaka 2018/19 yalifikia matukio 1510, mwaka 2019/20 matukio hayo yalipungua kutoka 1510 hadi 1426.

 

Kupungua huko kulichangiwa na uzuri wa hali ya hewa iliyochangia kupatikana kwa malisho ya kutosha kwenye maeneo yao.

 

Hata hivyo mwaka 2020/21 hali ilibadilika na kuwa mbaya zaidi kwani matukio 1706 yaliripotiwa na kuanzia hapo hali iliendelea kuwa mbaya zaidi kwani mwaka 2021/22 yaliripotiwa matukio 2304 na mwaka 2022/23 yalifikia matukio 2817.

Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 23.76 kwa mwaka na uharibifu wa mazao ukiwa ni ongezeko la wastani wa asilimia 118..1 kwa mwaka.   

 

Kwa mujibu wa takwimu hizo za TAWA, ni wazi mwaka 2018 kulikuwa na ongezeko kubwa la matukio ya migongano, ongezeko liliifanya wizara ya Maliasili na Utalii kuandaa mkakati wa Taifa wa kusimamia migongano kati ya Binadamu na Wanyamapori wa mwaka 2020-2024.

 

Mkakati huo ulizinduliwa Oktoba 5,2020 na unatekelezwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa -TANAPA, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro -NCAA, Wakala wa Misitu Tanzania -TFS, Mamlaka ya Utafiti wa Wanyamapori, Tawa na wadau wengine wa masuala ya uhifadhi.

 

Aidha ukubwa wa tatizo hilo unaziguza wilaya 44 ambazo zinakabiliwa na changamoto ya wanayamapori kurejea kwenye njia zao za awali hatua inayoonekana ni kama wanavamia maeneo ya watu na kusababisha uharibifu wa mazao, kujeruhi na wakati mwengine kusababisha vifo kwa binadamu.

 

Hatua hiyo haiwaathiri binadamu pekee, kwani hata wanyama nao wanaathirika kwa kujeruhiwa na wakati mwengine kuuwawa na binadamu.

 

Busega, Kilosa, Meatu, Nachingwea, Rufiji, Lindi, Manyoni, Itilima, Tunduru na Bunda ndizo zinatajwa kuwa na tatizo hilo huku Tembo akitajwa kuongoza kwa asilimia 80 kuwa na matukio ya kurejea kwenye njia zake na kuingia kwenye makazi ya watu, huku Simba, Fisi na Nyani wakibeba asilimia 20 ya matukio yote.

 

Moja ya njia zinazotajwa kuwa sehemu ya kusaka suluhu ya mgongano huo ni kuwepo kwa matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo yote yaliyozunguka hifadhi na mapori ya akiba, lakini pia ni vema wananchi wakasikiliza ushauri wa wataalam una kwamba ni vema wananchi wakawa wepesi wa kutoa taarifa kwa TAWA ili kuwaondoa wanyama hao kwa utaratibu na si kuvunja sheria kwa kuwaua.

 

TAWA huwarejesha hifadhini wanyama walioingia kwenye maeneo ambayo yana makazi ya watu kwa utaratibu stahiki na wale wanaoonekana kutokubaliana nah atua hiyo ya kuwarejesha hifadhini huwauwa ili kuepusha madhara.

 

Katika kipindi cha miaka saba 2017-23 jumla ya Simba 60 na Fisi wawili waliswagwa kutoka kwenye makazi ya wat una kurudishwa hifadhini na mwaka 2022 Tembo 270 waliovamia makazi kwenye wilaya ya liwale na Nachingwea walirudishwa hifadhini.



 

  

Post a Comment

0 Comments