Mtaalamu wa masuala ya migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori, John Noronha |
NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI-BAGAMOYO
Kukosekana kwa uelewa wa kutosha juu ya tabia na maisha ya viumbe pori kunachangia kwa kiasi kikubwa mgongano baina ya binadamu na Wanyamapori.
Kwa miaka mingi kumekuwa na mtazamo hasi kwa binadamu hasa wanaoishi pembezoni mwa hifadhi na mapori ya akiba nchini kudhani kuwa wanyama ndio chanzo cha migongano kwenye maeneo wanayoishi.
Ukweli ni kwamba kwa kiwango kikubwa binadamu ndio wamekuwa kisababishi cha migogoro hiyo kutokana na kuanzisha makazi kwenye mapito ya wanyama au kwenye malisho yao.
Aidha mwenendo wa idadi kubwa ya binadamu kudhani kuwa kila kiumbe pori ni hatari kwa maishayao unachangia migongano zaidi.
Tafiti zinaonesha kuwa viumbepori wengi si wepesi wa kuwadhuru binadamu mahali ambapo hawajachokozwa ama kusumbuliwa kwa namna yeyote.
Pamoja na mambo mengine wapo viumbe pori ambao pamoja na kuwa na sumu kwenye miili yao, lakini hawana madhara kabisa kwa binadamu.
Nyoka wengi ambao idadi kubwa ya Watanzania inawaona kama adui kwao bila kujali aina yake ni moja ya viumbe pori visivyo na madhara kwa binadamu.
Katika aina 3,000 za nyoka wote duniani ni aina 200 tu za nyoka ndio wenye sumu huku aina 2800 wakiwa hawana sumu kabisa.
Aina hii ya nyoka 200 wenye sumu huitumia kwa lengo la kuwinda, kusaidia mmeng’enyo wa chakula na kujilinda dhidi ya adui na wale wasio na sumu hutumia njia mbadala kuhakikisha wanapata chakula na kujilinda.
Jamii zote za Chatu ni miongoni mwa Nyoka wasio na sumu na hujipatia chakula kwa kulinyonga windo lake na kulivunjavunja kabla ya kulimeza na kadiri windo linavyovuta pumzi ndivyo chatu huongeza bidii ya kunyonga.
Mbali na kutafuta chakula, Nyoka wasio na sumu hujikinga na maadui kwa kuwang’ata ili kusababisha maumivu, kujifananisha na mazingira, kujiviringisha ili kuficha kichwa, kutetemesha mkia na wengine hujisugua magamba ili kutoa sauti ya kumtisha adui na hatari inavyokuwa kubwa nyoka hukimbia kwa usalama wao.
Mtaalamu wa masuala ya migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori, John Noronha amewaambia Waandishi wa Habari Februari 22,2024 kuwa nyoka si adui wa binadamu na ukweli ni kwamba kati ya asilimia 100 ya nyoka ni asilimia 30 tu ndio wenye sumu inayoweza kumuua binadamu.
Noronha ameyasema hayo katika mafunzo ya siku mbili ya waandishi wa habari yaliyoaandaliwa na JET kwa ufadhili wa Mradi wa Kupunguza Migogoro Baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania, unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani (BMZ).
Amesema nyoka ni kiumbe mpole sana, ambae hawezi kuanzisha mashambulizi kwa binadamu kama hajachokozwa na kwamba nyoka wengi wanang’ata lakini hawana sumu.“Kabla sijapata elimu ya masuala ya uhifadhi, nilikuwa nawaona nyoka kama adui, lakini baada ya kupata elimu, sitamani kuua hata sisimizi, kwa sababu wadudu na viumbe pori si adui wa binadamu, tunaweza kuendelea kuishi nao kama ilivyokuwa katika miaka yote.
“Hakuna sababu ya kudhuru wanyama kwa namna yeyote ile, si nyoka tu, hata wanyamapori hawaleti madhara mahali bila ya kuchokozwa,”alisema Noronha.
NYOKA HAWANA HASIRA
Mhifadhi Wanyamapori Tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa mkoani Morogoro, Makene Ngoroma ameieleza AFRINEWSSWAHILI kuwa watu wengi wanafikiri kuwa nyoka wana hasira na filamu nyingi zimetengenezwa kuakisi hilo.
Ukweli ni kwamba nyoka hana kumbukumbu nzuri, hana uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu, hajaumbwa kuuma binadamu, mashambulizi mengi ya nyoka ya kumuuma mtu yanatokea kama akihisi tu hayuko salama, anahisi maisha yake yako hatarini.
“Ni kweli nyoka wengi hawana madhara kwa binadamu, binadamu tunapaswa kujua kuwa nyoka hawawezi kutafuna chakula chao ingawa wanaweza kumeza wanyama wakubwa kuliko vichwa vyao. Muundo wa taya zao unafaa kwa hilo.”
NYOKA WOTE WANANG’ATA
Ofisa Uhifadhi kitengo cha uchunguzi kutoka TAWA, Tryphone Kanon amesema kuwa nyoka wote wanang’ata, lakini si wote wanaong’ata wana sumu.
Kanon alisema hata wale wenye sumu ziko nyakati wanang’ata bila kutoa sumu badala yake hujeruhi kwa nia ya kujilinda baada ya kuona uwepo wa hatari kubwa mbele yake.
TAHADHARI
Mtaalamu wa afya, Dkt. Damas Mavika ameliambia AFRINEWSSWAHILI kuwa pamoja na ukweli huo kuwa nyoka wengi hawana madhara kwa binadamu, ipo haja ya kuchukua tahadhari hasa ya kutochokoza nyoka na viumbe pori wengine.
Dkt. Mavika pia alitoa maelekezo kwa mtu atakayeng’atwa na nyoka kuhakikisha anatafuta matibabu kwa haraka.
“Usijajiribu kukamata nyoka kama huna utaalamu huo kwa sababu nyoka wengi hawapendi kubugudhiwa.”
Aidha wataalamu wa wanyamapori na viumbe pori wanashauri binadamu kutoaua nyoka na viumbe pori bila sababu za msingi, lakini pia waepuke kuvamia maeneo ya wanyama pori hasa malisho na mapito yao.
0 Comments