Fei anajidanganya
Fei anajidanganya wala hakuna anaemdanganya na wanaosema anadanganywa hawajui.
Uhakika nilio nao Fei si mtoto, anaweza asiwe na elimu ya kung'amua na kupembua masuala ya kielimu, lakini hawezi kushindwa kujua baya na zuri.
Uamuzi wake wa kuondoka Yanga kwa mfumo alioutumia iwe amenyanyaswa au amedhulumiwa si mzuri.
Fei kama alitaka kuendelea kucheza soka popote pale, alipaswa kufuata taratibu stahiki za kuvunja mkataba wake.
Alipaswa kukutana na viongozi wake hata kama hawapendi au hawampendi, lakini hao ndio mabosi wake na mkataba wake hata kama hakuuelewa wakati wa kuusaini, ukweli ni kuwa wao ndio wenye mkataba na aliusaini kwao.
Njia anayoitumia sasa inaweza isimsaidie kabisa na zaidi ikamuondoa kwenye ramani ya soka la ushindani.
Inawezekana ni kweli yako mambo hayamridhishi ndani ya Yanga, lakini hiyo si sababu ya kuvunja mkataba bila kufuata utaratibu.
Bahati mbaya sana Fei hajui waliomzunguka sasa wote ni wafanyabiashara na hawako tayari kuona wanaacha hela iliyo nje nje.
Kwa sasa watasimama nae, lakini muda utafika na watamuacha ahangaike mwenyewe.
Fei anapaswa kujua hakuna bure iso ghali, afungue macho mapema.
Nini anapaswa kufanya Fei, kwanza ni kuwa tayari kushuka na kuomba yaishe.
Atafute watu wenye hekima na busara zao na wenye ushawishi mkubwa ndani ya Yanga.
Watu wa kariba ya Mzee Jakaya Kikwete ili awatumie kulimaliza suala hili, vinginevyo ataishia kwenye ndondo cup.
Nakiri kuandika bila haya kuwa Fei anajidanganya, na sitaki kuamini kuwa anadanganywa.
Mchezaji huyu hata aseme amenyanyaswa au ameitwa Mpemba na majina mengine ambayo hakuyapenda, hawezi kukwepa kuwa yeye ni mali halali ya Yanga na Injinia Hersy ndie boss wake.
Sasa Fei ameamua kuishtaki TFF, CAS. Sina hakika kama atatoboa, hata hivyo namuombea Mungu ashinde ili arejee uwanjani akiwa na timu anayoitaka mwenyewe kwa sasa.
Yanga inamkomoa
Imani niliyonayo. Awali viongozi wa Yanga walikuwa na utayari wa kukaa na mchezaji wao na kumboreshea maslahi yake hata kinyume na mkataba aliousaini.
Naamini hivyo kwa sababu nyakati zile Yanga ilimuhitaji Fei kuliko Fei alivyoihitaji Yanga.
Kwa bahati mbaya Fei akakaza, mkazo wake haukuwa na dalili za kulegea.
Yanga ikaishi kwa taabu bila Fei huku ikiwa inamujitaji kikweli kweli.
Maisha ndani ya Yanga yakaendelea, hatimae wakaanza kuzoea kuishi bila yeye.
Mafanikio yakaanza kupatikana bila Fei.
Kikosi cha Yanga bila Fei kikashinda michezo ya Ligi Kuu hadi kuchukua ubingwa huku kikiwa na michezo mkononi, kikashinda michezo ya Kombe la Shirikisho la Azam hadi kutinga fainali na kikashinda michezo ya Kombe la Shirikisho Afrika hadi kutinga fainali.
Hapo ndipo benchi la ufundi, wachezaji, viongozi, wanachama, mashabiki na wamepenzi wa Yanga walipoona wanaweza kupata matokeo mazuri bila ya Fei na hamu ya kuendelea kumsihi arejee kundini ikaishia hapo.
Yanga ya sasa haimuhitaji tena Fei, badala yake imeamua kumkomoa maana hakuna shaka sasa Fei ndio anaihitaji Yanga katika kulinda kipaji chake kuliko nyakati nyengine zote.
Yanga imelitambua hili na ndio imeamua kusimamia hapo Ili kumuonesha kuwa sikio halizidi kichwa.
Naamini Yanga ingeweza kumalizana na huyu mchezaji kwa kufuata sheria ama kwa ubinadamu, lakini haifanyi hivyo Kwa sababu ya kutaka kumkomoa.
Kujidanganya kwa Fei nje ya utaratibu stahiki ndio kunawasukuma viongozi wa Yanga kumkomoa.
Bila shaka Yanga wanajua ni nani yuko nyuma ya sakata hili la Fei na ndio maana wameamua kulishughulikia kwa namna Ile Ile iliyotumiwa na Fei na watu wake.
Imani niliyo nayo, viongozi wa Yanga si makatili wa namna hii, wanao uwezo wa kulimaliza suala hili ndani ya dakika moja tu, lakini wameamua kumkomoa na kijana huyu asipokubali kuweka silaha chini na kuacha busara itumike, atakwama.
Kauli na maneno anayoyatoa sasa hayatamsaidia kufanikisha suala hili.
Huruma anayoitafuta nje ya utaratibu haidumu ni ya muda mfupi sana na bahati mbaya hawa wanaomuhurumia sasa hawachelewi kusahau.
Feisal anapaswa kutambua kuwa yeye si wa kwanza na hatakuwa wa mwisho kuitumikia Yanga.
Nafuu yake ni kukubali kukosea ili huu mwenendo wa kukomoana uishe.
TFF haitaki lawama
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limefanya kazi yake kwa weledi.
Halikutaka lawama, limemtaka mchezaji aendelee kuitumikia Yanga na kama kuna zaidi basi wakae wazungumze.
Nakiri hawakutaka lawama, lakini TFF hii hii ingeweza kumpa nafasi Feisal kwenda anapotaka kwa kumuadhibu zaidi Kwa kosa la kukiuka mkataba wake.
Kama Kamati ya sheria na Hadhi za wachezaji imebaini kuwa Feisal amekosea maana yake alistahili adhabu zaidi ambayo ingemlazimisha kuvunja mkataba wake kwa kufuata utaratibu stahiki.
Hatua ya kumlazimisha kurudi Yanga inaweza kuwa sahihi, lakini ikakosa dhamira njema ya kumpa furaha mchezaji.
TFF imeamua ilichoamua kwa sababu inazijua nongwa za viongozi, wanachama, mashabiki na wapenzi wa Yanga na hasa ikizingatiwa kuwa zipo hoja zisizo rasmi kuwa TFF ya sasa ina mahaba zaidi na Simba.
Hata hivyo naamini bado pande zote zina nafasi ya kulimaliza jambo hili kwa maslahi mapana ya mchezaji, Yanga na taifa kwa ujumla.
(C)Jkiango
0 Comments