Ticker

7/recent/ticker-posts

WATUMISHI WA UMMA MALINYI WAFURAHIA BARAZA LA WAFANYAKAZI

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Khamis Katimba 

Na Mwandishi Wetu

Uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi la Wilaya ya Malinyi, Morogoro umewafurahisha watumishi wa serikali wilayani humo kwamba, wamepata sehemu ya kueleza changamoto na kutetea maslahi yao.


Akifungua kikao cha uzinduzi wa baraza hilo leo Januari 15,2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Khamis Katimba ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza hilo alisema, baraza hilo ni moja ya nyenzo katika utatuzi wa changamoto mbalimbali kwa pamoja na uimarishaji wa maslahi ya watumishi.

 

“Humu tutapanga na kutatua changamoto zetu, tumefanya hivi ili tuwe tunazungumza kwa pamoja, tunapanga kwa pamoja na tunakubaliana kwa pamoja,” alisema mkurugenzi huyo.

Akizungumza kwenye kikao hicho, mgeni rasmi Christina Matage kutoka Ofisi ya Kazi Mkoa wa Morogoro alimsifu Katimba kwa kuhuisha baraza hilo kwa kuwa, ni uwanja wa kutetea maslahi ya watumishi.

 

“Baraza hili lina maslahi makubwa kwenu, litumieni vizuri kuhakikisha changamoto zenu zinatatuliwa, mkitatua changamoto zenu mtafanya kazi kwa moyo na uadilifu. Katika hili nampongeza sana mkurugenzi kuhuisha chama hichi hapa Malinyi,” alisema Christina.

Juhudi Swetu, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi Wilaya ya Malinyi alisema, uzinduzi wa baraza hilo unafungua majadiliano ya moja kwa moja kati ya watumushi na Ofisi ya Mkurugenzi.

 

“Ni jambo jema sana, ni rahisi kupata suluhisho kwenye vikao vyetu kwa kuwa, huu ni mlango wa moja kwa moja na Ofisi ya Mkurugenzi,” alisema.

Katibu wa CWT Mkoa wa Mkoa wa Morogoro, Alphone Benedict aliwataka wanachama wa baraza hilo kutumia baraza kueleza na kutetea maslahi yao na sio nje ya baraza hilo.

“Baraza hili limerahisisha mawasiliano, ni vizuri badala ya kupiga yowe huko nje, tukutane hapa na kueleza changamoto zetu,” alisema.

 


Post a Comment

0 Comments