NA JIMMY KIANGO-MANG’ULA-MOROGORO
Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umekuwa ni kichocheo kikubwa cha kuitunza na kuilinda shoroba ya mfano ya Wanyamapori ya Nyerere Selous - Udzungwa,iliyopo katika mikoa ya Iringa na Morogoro.
Shoroba hiyo sasa inatazamwa kama ni ya mfano kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanyika kuilinda ikiwa ni pamoja na kutengeneza njia ya chini inayotoa nafasi kwa wanyamapori kuvuka barabara kubwa inayounganisha miji ya Ifakara na Mikumi (Under path) bila kuathiriwa na shughuli za kibinadamu.
Mei 27,2024 Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) ambacho kinatekeleza mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kilisafirisha timu ya Waandishi wa Habari za Mazingira kwenda mkoani Morogoro, wilayani Kilombero pamoja na mambo mengine kushuhudia namna shoroba ya Wanyamapori ya Nyerere Selous - Udzungwa inavyotunzwa na kulindwa kwa ubora wa hali ya juu.
Ukweli ni kwamba kazi kubwa imefanyika katika shoroba hiyo, miti ya asili zaidi ya 15,000 imeshaoteshwa ili kurejesha uasili wa eneo hilo ambalo wananchi waliligeuza kuwa mashamba ya miwa na mpunga na matarajio ya taasisi ya Reforest ni kuotesha miti 100,000 kwa mwaka.
Timu ya Waandishi wa Habari za Mazingira wakiongozwa na Mkurugenzi wa JET, John Chikomo (wa nne kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Maofisa wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa waliovaa mavazi ya kijeshi.
Ikumbukwe kuwa Hifadhi ya Milima ya Udzungwa (USNFR) ina ukubwa wa hekta 32,763.2 na urefu wa takriban kilomita 126 na inapatikana nyanda za juu Kusini mwa Tanzania ndani ya mkoa wa Iringa na Morogoro.
Kwa mkoa wa Iringa Hifadhi hiyo iko ndani ya wilaya za Kilolo na Mufindi na katika mkoa wa Morogoro inapatikana ndani ya wilaya ya Kilombero.
Hifadhi hii ya Milima ya Udzungwa, ni sehemu ya mlolongo wa Milima ya Tao la Mashariki, inajumuisha misitu mirefu ya nyanda za juu na misitu midogo midogo.
Miongoni mwa mimea iliyopo ndani ya safu ya milima hiyo ya Tao la Mashariki ni ile inayotumiwa katika tafiti za kitaalamu na baadhi ya wataalamu wa masuala ya dawa kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Kuna njia kuu tatu za kufika katika hifadhi hiyo ya kwanza ni kupitia Ipogoro, Wilaya ya Kilolo ambayo ni takriban kilomita 80 hadi 100 kutoka Iringa Mjini, njia ya pili ni kupitia Wilaya ya Mufindi takriban kilomita 130 kutoka mji wa Mafinga mkoani Iringa, huku njia ya tatu ni kupitia Mikumi mjini, Ifakara ambayo ni takriban kilomita 80 kutoka Ifakara mjini.
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Theodora Batiho (kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa JET, John Chikomo.
Vivutio vya utalii vilivyopo kwenye hifadhi hiyo ni pamoja na Udzungwa escarpment, Colobus monkeys( red and black white ) water falls (Idasi, Funo na Ilutila ) Natural dams (Mkololo/mabwawa ya asili ),chura anayepanda miti (Hyperolius kihangensis), mikunjo (Ilutila,Ngwilo).
Akiizungumzia hifadhi hiyo, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Milima ya Udzungwa , Theodora Batiho anasema kuwa hifadhi hiyo ni ya kimkakati kwani imebeba maisha ya Watanzania wengi ndani na nje mkoa wa Morogoro.
“Hifadhi hii ni ya kimkakati, tunahifadhi vyanzo 11 vya maji, milima ya Udzungwa inazalisha kiasi kikubwa cha hewa safi ambayo sisi Watanzania ndio tunaivuta.
“Tunajitahidi kulinda wanyama na viumbe hai vilivyomo hifadhini kwa gharama yeyote ile na tunawashukuru wadau wetu, hasa USAID wameweza kutusaidia kutunza na kulinda shoroba kwa kushirikiana na taasisi zilizopo hapa Ifakara kama Reforest Africa, Mjumita, STEP na ASSOCIAZIONE Mazingira.” Amesema Batiho.
Amesema uwepo wa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umesaidia kufanikisha harakati nyingi za kuilinda hifadhi kwa ujumla wake, hata hivyo zipo changamoto ambazo wanaamini wadau hao wanawaweza kuwasaidia, alizitaja changamoto hizo kuwa ni uhaba wa vifaa vinavyoweza kuwafikisha kwenye maeneo mengi zaidi ndani ya hifadhi.
“Kwa sasa hatuwezi kufika kwenye maeneo mengi ya hifadhi, msitu umefunga sana, sio rahisi kutuma askari kwenda kwenye kila eneo la msitu, yapo maeneo hayajafikiwa kabisa, kwenye maeneo haya tunahitaji ndege isiyo na rubani (Drone).
Afisa Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Christina Kibwe.
“Tukifanikiwa kupata kifaa hiki tutaweza kufanya kazi nzuri na bora zaidi ya kuilinda hifadhi hii ambayo mimi naamini inaweza kuwa na tija kubwa kama italindwa na kuhifadhiwa kwa viwango vya juu,”amesema.
Katika kuhakikisha hifadhi hiyo inakuwa ni sehemu nzuri ya kutembelea kwa mwaka mzima, Batiho amesema pamoja na changamoto walizonazo, wameamua kufanya maboresho makubwa kwa kuongeza vivutio vya utalii ikiwa ni pamoja na kujenga daraja la juu lenye urefu wa kilomita moja, kuanzisha utalii wa farasi, baiskeli na kuboresha barabara ili magari yaweze kutumika pia fatica kufanya utalii.
“Hili daraja la juu litakuwa ni refu kuliko madaraja yote yaliyopo kwenye Hifadhi kwa nchi za Afrika Mashariki, litakuwa ni namba moja, ujenzi wake umeshaanza.”
Kwa upande wake Afisa Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Christina Kibwe, alisema malengo yao ni kuhakikisha hifadhi hiyo inakuwa ya mfano hasa katika kulinda wanyama na kutunza shoroba.
Mkurugenzi wa JET, John Chikomo alimpongeza Mhifadhi Mkuu, Batiho na timu yake kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kwa timu ya Waandishi wa Habari za Mazingira waliofika ofisini kwake, ambapo aliahidi JET kuendelea kushirikiana na hifadhi hiyo.
Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaotekelezwa katika shoroba za Kwakuchinja, Amani Nilo, Udzungwa na Hifadhi ya Nyerere, Ruaha Rungwa na Katavi, Ruaha Rungwa na Inyonga na Kigosi Moyowosi- Burigi Chato umekuwa na tija kwenye eneo la uhifadhi kwani pamoja na mambo mengine umesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa migongano baina ya binadamu na wanyamapori.
0 Comments