Ticker

7/recent/ticker-posts

‘JUHUDI ZA PAMOJA ZINAHITAJIKA KATIKA KUISADIA SERIKALI KUDHIBITI BIASHARA HARAMU YA VIUMBE PORI’

 

Mkuu wa Kitengo cha Sera mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Allen Mgaza (kushoto) na Mwenyekiti wa Baraza la Wasafirishaji Shehena Tanzania, Clement Kamendu akitoa ufafanuzi wa namna sekta binafsi inavyoshiriki katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya viumbe pori kwenye mdahalo uliofanyika Juni 19,2024, TBC, jijini Dar es Salaam.

NA JIMMY KIANGO

Serikali ya Tanzania imepongezwa kwa jitihada mbalimbali inazozichukua katika kukabiliana na biashara haramu ya viumbe pori. Ikumbukwe kuwa biashara haramu ya viumbe pori ni miongoni mwa biashara haramu kubwa zinazotikisa duniani ikishika nafasi ya nne huku Dawa za kulevya, bidhaa bandia na usafirishaji wa Binadamu zikitajwa kuongoza kwenye mlolongo wa biashara haramu duniani.

 

Uwepo wa biashara haramu ya viumbe pori unatajwa kuwa na athari mbalimbali katika eneo la kiuchumi, kijamii na kimazingira

 

Mkuu wa Kitengo cha Sera mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Allen Mgaza amebainisha kuwa biashara ya viumbe pori imekuwa ikifanyika kwa siri sana na mtandao wake ni mkubwa unaohusisha watu wenye nguvu kubwa ya kifedha. Amesema bila ushiriki wa pamoja haitakuwa rahisi kupambana na biashara hiyo, badala yake uhalifu tuo utaendelea.

 

Mgaza ameyasema hayo jana Juni 19,2024 kwenye mdahalo maalum ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa USAID kupitia mradi wake wa USAID Tuhifadhi Maliasili. Mdahalo huo ulioshirikisha Waandishi wa Habari za Mazingira ulioneshwa moja kwa moja na shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupitia chaneli yake ya Safari.

 

Katika mdahalo huo Mgaza alisema: Biashara haramu ya viumbe pori ni tatizo na ili kukabiliana nalo ni lazima kuwe na juhudi za pamoja kitaifa na  kimataifa, wizara na taasisi za serikali, sekta binafsi na hata mtu mmoja mmoja, wote wanapaswa kushiriki katika kupambana na biashara hii haramu ya viumbe pori.

 

Baadhi ya Waandishi wa Habari za Mazingira wakifuatilia kwa makini mdahalo huo.

“Mimi najivunia kuzaliwa Tanzania, uwepo wa kila maliasili unanifanya niione fahari ya kuwa Mtanzania, sasa ili tusije kujuta baadae ni lazima tushiriki kikamilifu katika vita hii,” alisema.

 

Mgaza anasisitiza kuwa biashara haramu ya viumbe pori inayofanyika kwa siri kubwa na watu wanaoifanya wana mbinu nyingi za kupunguza mwanya wa kukamatwa na mamlaka, hivyo lazima nguvu ya pamoja itumike katika kuhakikisha inadhibitiwa.

 

Katika hatua nyingine, Mgaza ametoa wito kwa waandishi wa habari kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika kusaidia jamii kubainia madhara ya biashara hii. “Ni muhimu kutoa elimu kwa jamii ili ijue kuwa kuna madhara kwa mtu kujihusisha na biashara hiyo, kwani ikitokea muhusika akakamatwa na kufungwa maana yake ameiacha familia yake kwenye wakati mgumu.

 

“…Lakini pia  ni kulihujumu taifa kwa sababu ukivimaliza viumbe pori maana yake umamaliza urithi wan chi.”

“Nasisitiza, najivunia kuwa Mtanzania, hivyo basi sitamani ifike wakati watoto wetu au wajukuu tuwaonyeshe picha za wanyama badala ya kuja kuwaona live kama sisi tunavyowaona sasa, watoto na wajukuu zetu wanapaswa kufurahia rasilimali hizi za wanyamapori ambazo kama nchi tumebahatika kuwa nazo,” amesema.

 


USHIRIKI WA SEKTA BINAFSI

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wasafirishaji Shehena Tanzania, Clement Kamendu, alisema bado ushiriki wa sekta binafsi kwenye mapambano dhidi ya biashara haramu ya viumbe pori ni mdogo.

 

Kamendu, alisema iwapo sekta binafsi itashiriki kikamilifu upo uwezekano wa kuimaliza biashara hiyo kwa sababu wahusika wapo ndani ya jamii yetu. Alisema kwa upande wao kama wasafirishaji wa shehena wamekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa wadau wao ili kujiepusha na ubebaji wa bidhaa hizo haramu.

 

“Sisi kwa upande wetu tumekuwa mstari wa mbele kuzungumza na kuwapa elimu  wadau wetu wote ambao ni wasafirishaji wa shehena kwa kutumia maroli, mabasi na usafiri mwengine, wasikubali kujiingiza matatani kwa kubeba bidhaa haramu.”alisema.

 

Kamendu alisema biashara haramu ya viumbe pori ni hatari na serikali iko makini kuhakikisha haishamiri na ndio maana katika kipindi cha mwaka 2009-2015 kulikuwa na kesi 391 na watu 301 wamehukumiwa kifungo cha jumla ya miaka 3015.

 

Baadhi ya Waandishi walioshiriki mdahalo huo.


VIUMBE VINAVYOWINDWA SANA

Mgaza ametaja baadhi ya viumbe pori ambavyo vinafanyiwa biashara haramu kuwa ni pamoja na mimea ya pori ikiwamo msandari ambao watu wanauchukua na kukata vipande vyake bila kufuata sheria.

 

“Mbali na mimea kuna mnyama anaitwa Kakakuona ambaye magamba yake yamekuwa yakisafirishwa mara kwa mara, mfano kuna kesi ilitokea Malaysia ambapo kuna tani sita za magamba ya kakakuona zilikamatwa, hivyo tukifikiria umbo la kakakuona hadi upote magamba ya kiwango hicho maana yake ni wanyama wengi wameuwawa, hivyo biashara hii ikifanyika kwa miaka minne mpaka mitano basi wanyama hawa watapotea,” amesema Mgaza.

 

UDHIBITI

Mgaza anasema kuwa kama wadau wanafurahi kuona kwamba nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania zimesaini mkataba wa Vyama vya Mkataba wa Biashara ya Kimataifa ya Viumbe vilivyo Hatarini Kutoweka (CITIES) ambao ni mkataba wa kimataifa unaodhibiti biashara ya kimataifa ya viumbe pori vilivyohatarini kutoweka.

 

“Tumerekebisha sheria yetu kwa kuweka sheria ambayo inaakisi mikataba ya kimataifa iliyokubaliana, tunasheria nzuri sana katika hili, hivyo nadhani kutoa elimu ni muhimu lakini usimamizi wa sheria ni jambo jingine.

 

“Kwanza kunahitajika uwezeshwaji kwa vyombo vyetu vinavyosimamia viumbe pori hawa wakiwamo TAWA(Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania) na vingine,” amesema Mgaza.

 


TAKWIMU

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa Ofisi ya kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) ya mwaka 2020 iliyopewa jina la “Uhalifu wa Wanyama pori duniani ya mwaka 2020” inabainisha kuwa, Ghada Waly amesema “Mitandao ya uhalifu wa kimataifa wa kupangwa inajipatia faida kutokana na biashara haramu ya wanyama pori, lakini watu masikini ndio wanaolipa gharama ya uhalifu huo,”.

 

KAKAKUONA ANASAFIRISHWA ZAIDI

Pamoja na kuwepo kwa jitihada mbalimbali za kukabiliana na biashara hiyo, hata hivyo ripoti mbalimbali zinazoangazia biashara haramu ya viumbe pori inaweka inabainisha kuwa kati ya mwaka 2014 na 2018 kulikuwa na ongezeko kubwa la mara 10 la ukamatwaji wa magamba ya kakakuona yaliyokuwa yakisafirishwa kiharamu na hivyo kufanya wanyama hao kuwa ndio wanyama pori wanaosafirishwa zaidi kiharamu duniani.

 

Pia imesema karibu aina 6,000 za viumbe vilikamatwa katika muongo uliopita vikisafirishwa kiharamu wakiwemo wanyama, lakini pia mijusi, matumbawe, ndege na samaki


Hata hivyo haikutaja nchi yoyote kuwa ndio chanzo cha zaidi ya asilimia 9 ya idadi yote ya wanyama pori na mimea iliyokamatwa ikisafirishwa kiharamu, huku washukiwa wa usafirishaji huo haramu wakiwa ni kutoka mataifa 150 na hivyo kudhihirisha kuwa uhalifu huo ni wa kidunia.

 


BIASHARA HARAMU YA MITI

 Ripoti hiyo pia imeilinisha na kutathimini masoko ya usafirishaji haramu wa mbao, pembe za ndovu, pembe za vifaru, magamba ya kakakuona, jamii ya mijusi, paka shume na aina ya samaki kutoka Ulaya wanaofanana na nyoka.

Mwenendo unaonyesha kwamba mahitaji ya pembe za ndovu na za vifaru kutoka Afrika yanapungua ikimaanisha kwamba masoko ya bidhaa hizo ni madogo kuliko ilivyopendekezwa hapo awali.  

 

Inakadiria kwamba bidhaa hizi mbili zilitengeneza zaidi ya dola milioni 600 kila mwaka kati ya mwaka 2016 na 2018 huku kwa mwaka 2023 kiwango hicho kikipaa na kufikia dola bilioni 23. Wakati huohuo mahitaji ya bidhaa za mbao yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika miongo miwili iliyopita.

Na biashara haramu ya mbao kutoka Afrika imeingia kwenye mnyororo halali kwa ajili ya biashara ya samani. 

 

Pia ukamatwaji wa bidhaa za chui umeongezeka lakini wasafirishaji haramu wanania ya bidhaa za aina nyingine ya paka wakubwa ili watumike kama mbadala wa chui.


Mbali ya aina iliyozoeleka ya biashara sasa biashara hiyo imeingia katika njia ya kidijitali na wasafirishaji haramu wamekuwa wakiuza mtandaoni na kupitia program tumishi mbalimbali wanyama walio hai na jamii ya mijusi kama nyoka na pia mifupa ya chui miongoni mwa vitu vingine.

Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru akiongoza mdahalo huo.

KAULI YA JET

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo amebainisha kuwa mdahalo huo ni sehemu ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na kwamba lengo lake ni kuendelea kuihabarisha jamii juu ya umuhimu wa kutunza na kuhifadhi maliasili zetu.

 

Mradi wa Tuhifadhi Maliasili ni wa miaka mitano na unalenga zaidi kushughulikia tishio la kutoweka kwa wanyamapori na viumbe hai nchini Tanzania.

 

Kupitia mdahalo huu, wananchi wanapata maarifa, uelewa na  mtazamo chanya wa namna ya kupambana na biashara haramu ya viumbe pori

 

 

 

Post a Comment

0 Comments