Afisa Mtendaji Mkuu wa Hoteli ya MAKMar iliyoko Msata mkoani Pwani,Bregadia Jenerali mstaafu Martin Amos Kemwaga akizinguzungumza wakati wa Bonanza la Rudisha Kijani, ambalo lilishirikisha vikundi mbalimbali vya Jogging, vilivyoshiriki kupanda miti 200 kwenye eneo la Hoteli ya MAKMar, iliyopo Msata,Bagamoyo mkoani Pwani.
Na. MWANDISHI WETU -PWANI
‘Bila Miti Hakuna Dunia, kampeni ya Mti kwa Umri inayoendeshwa na Hotel ya MAKMar iliyopo Msata, Bagamoyo mkoani Pwani inahamasisha upandaji miti.’
Umewahi kufikiria gharama unayotumia kusherehekea siku yako ya kuzaliwa! Picha unazopiga, keki, vinywaji na vitu vingine.
Hata hivyo, kumbukumbu hizo hufutika pindi tu siku husika inapotamatika. Vipi kama ungetumia siku hiyo kuweka kumbukumbu ya kudumu kwa kupanda mti!
Kitendo cha kupanda mti kitakusaidia kujitengenezea Tanzania njema ya kesho na hili linawezekana.
Hiyo ndiyo kampeni inayotekelezwa na Brigedia Jenerali Mstaafu, Martin Amos Kemwaga katika eneo la Msata, mkoani Pwani nchini Tanzania.
Brigedia Jen. Kemwaga pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Hoteli ya MAKMar iliyoko Msata mkoani Pwani iliyozinduliwa Oktoba 7,2019 na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete.
Brigedia Jen. Kemwaga akiotesha mti.
Juni 15, mwaka huu akizungumzia kampeni hiyo aliyoipa jina la "Mti kwa Umri," Brigedia Jen. rtd, Kemwaga anasema alitafakari kwa kina kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kubaini kuwa miti ni mapafu ya dunia na ni muhimu kwa maisha ya kila siku.
"Kwa kuzingatia kuwa kila siku kuna Mtanzania anayezaliwa, niliona fursa ya kuunganisha sherehe za siku za kuzaliwa na upandaji miti. Watu hushirikisha ndugu na marafiki kusherehekea siku hizi. Sasa, kama tutasherehekea kwa kupanda miti, tutakuwa na sababu nyingi za kuitunza," anasema Brigedia Jen. Kemwaga.
Anasema ni vema Watanzania wakaadhimisha siku zao za kuzaliwa kwa kuhakikisha wanapanda mti mmoja popte atakapokuwepo kila mwaka.
Brigedia Jen mstaafu,Kemwaga ambaye hadi sasa amepanda miti zaidi ya 500, anaeleza kuwa kupanda mti kwenye siku yako ya kuzaliwa ina maana zaidi kuliko kusherehekea kwa kula na kunywa pombe.
"Inamaanisha utautunza mti huo kwa sababu uliupanda kwenye siku yako maalum. Kama ni mti wa matunda, wewe na watoto wako mtafurahia matunda yake. Kama ni mti wa mbao, vizazi vijavyo vitaendelea kufaidika na rasilimali hiyo," anasema.
Anafafanua zaidi kuwa kampeni hii inaweza kuchochea urejeshwaji wa uoto wa asili uliopotea kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa katika maeneo mengi nchini.
"Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2023, Watanzania wapo zaidi ya milioni 64. Kama kila Mtanzania atapanda mti siku ya kuzaliwa kwake, tutakuwa tumepanda miti milioni 64 kwa mwaka mmoja," anasema.
KUPANDA MITI KILA MAHALI
Brigedia Jen. Kemwaga anasema jamii na wadau mbalimbali wamekuwa wakijikita zaidi kupanda miti katika maeneo ya shule na kusahau kwamba kuna sehemu nyingine muhimu.
"Kama hauna sehemu ya kupanda mti, ni bora ukapanda hata kwa jirani yako kwani utaleta manufaa kwako baadaye. Hata kama una shamba, unaweza kuligawa sehemu nyingine na kupanda miti," anasema.
MTI KWA UMRI
Akizungumzia kampeni ya "Mti kwa Umri," Brigedia Jen. Kemwaga anasema kampeni hiyo inalenga kurejesha uoto wa asili kwa kupanda miti kulingana na umri wa mtu anaposherehekea siku yake ya kuzaliwa. "Ukiangalia kwenye kalenda, kila siku kuna Mtanzania anazaliwa. Hii inamaanisha kuwa kila siku kuna mti utakaopandwa. Tukijizatiti kwenye hili, Tanzania itakuwa na uoto mzuri na wa kuvutia tena," anasema.
HAMASA
Amesema mwitikio wa kampeni hiyo umekuwa na mafanikio makubwa. Watu wameanza kuiga utaratibu huo na hata baadhi wamekuwa wakifika kujifunza.
"Hata wageni wanaofika kulala katika hoteli hii ya MAKMar wamekuwa wakishiriki kampeni hii na zaidi ya watu kutoka nchi 10 tofauti wamepanda miti hapa," amesema.
VIKUNDI VYA JOGGING
Katika kuhakikisha kampeni hiyo inakuwa shirikishi Brigedia Jen. Kemwaga amesema wameamua kushirikisha vikundi vya jogging kwa kuwa itakuwa rahisi kueneza kampeni ya "Mti kwa Umri" kupitia mabonanza mengi. "Vikundi vya jogging kutoka mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam, na Morogoro vimeshiriki kupanda jumla ya miti 200 katika eneo hili la MAKMar, miti ambayo tumeipata kutoka TFS," amesema.
KAMPENI NCHI NZIMA
Amesema mipango iliyopo sasa ni kuhakikisha kampeni hii inafika kila kona ya nchi ili kuhamasisha utunzaji wa mazingira na uoto wa asili.
"Hatutaishia hapa. Tutahakikisha kuwa kampeni hii inakuwa endelevu na inafika nchi nzima. Pia tunapaswa kubadilisha usemi uliozoeleka wa 'kata mti panda mti'. Mti unaandaliwa kwa muda mrefu lakini unakatwa ndani ya dakika moja tu. Hii siyo sawa," amesema.
MCHANGO WA TFS
Afisa Misitu kutoka Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (TFS) mkoa wa Pwani, Lenin Festo Paul, amesema wanaunga mkono kampeni hiyo kwa sababu inachochea utunzaji wa mazingira na kuimarisha misitu nchini. "Hii ni kampeni ya kuigwa kwani inachochea utunzaji wa mazingira. TFS tumetoa miche 200 bure kwa ajili ya kupandwa hapa kama kielelezo cha kuunga mkono kampeni hii. Watanzania wengine waige kampeni hii kwani itasaidia kutunza mazingira," amesema Paul.
Mmoja wa wananchi walioshiriki kampeni hiyo, ambaye pia ni mdau wa mazingira katika eneo hilo la Msata, Selestine Semeni, amesema kuwa "Mti kwa Umri" ni kampeni inayopaswa kuwa endelevu kwani inachochea hali nzuri ya hewa. "Kampeni hii inapaswa kuwa ya kitaifa kwani inamgusa kila mtu.
Tunampongeza sana Brigedia Jen. Kemwaga kwa kuja na kampeni hii kwani tunasherehekea siku za kuzaliwa kila mwaka. Ikiwa tutachukua mtazamo huu wa kupanda miti kulingana na umri unaofikisha, itasaidia jamii yetu kutunza mazingira," amesema Semeni.
Kampeni ya "Mti kwa Umri" ni njia bora ya kuunganisha sherehe za siku ya kuzaliwa na jitihada za kulinda mazingira.
Kwa kupanda mti kila unapotimiza mwaka mmoja zaidi, tunachangia katika kutunza mazingira na kuacha urithi mzuri kwa vizazi vijavyo. Hii ni njia ya kipekee ya kuadhimisha maisha yetu huku tukitunza dunia.
0 Comments