Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania, akitoa pongezi kwa Rais Samia |
NA JIMMY KIANGO, DODOMA
Jumuiya ya Shia Inthna'ashariyyah Tanzania (T.I.C) imeipongeza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa hatua yake ya kuwapa nafasi viongozi wa Dini na Watanzania kwa ujumla kutoa maoni yao kwenye rasimu ya Kanuni za Uchaguzi wa Mitaa wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa.
Pongezi hizo zimetolewa leo na Sheikh Mkuu wa Jumuiya hiyo, Maulana Sheikh Hemed Jalala, alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma.
Sheikh Jalala, amesema hatua ya kutoa maoni kwenye Kanuni za uchaguzi wa Serikali za mitaa ni kubwa na inapaswa kutumiwa vizuri na wananchi watakaopata mafasi hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa haijawahi kupatikana nafasi kama hiyo.
Amesema kinachofanywa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kina lengo jema la kuidhihirishia dunia kuwa Tanzania ina demokrasia ya kweli.
Naibu Waziri OR-TAMISEMI Dkt.Festo Ndugange akifungua mkutano wa wadau kutoa maoni kwenye Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa |
"Hili si jambo dogo, binafsi sijawahi kuona watu wakipewa nafasi ya kutoa maoni yao kwenye kanuni za uchaguzi, nampingeza Rais Dkt. Samia na serikali yake kwa hatua hii.
"Ameonesha dhahiri nia yake njema ya kuleta demokrasia ya kweli nchini, kuruhusu uchaguzi wa uwazi na haki, Watanzania tunapaswa kuitumia nafasi hii vizuri."
Ameongeza kuwa yeye akiwa ndio kiongozi mkuu wa Shia Tanzania, atahakikisha anaitumia nafasi hiyo kuwaelemisha waumini wake ili kuujua umuhimu wa kutoa maoni pale watakapopata nafasi na kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Aidha Sheikh Jalala, amewataka wanasiasa hasa wale wanaotaka uongozi wa kuchaguliwa kuepuka kutumia lugha zenye sura ya kuligawa taifa na matusi, badala yake wabebe hoja kwenye kampeni zao, lakini kubwa zaidi wawe tayari kutoa maoni yao pale watakapopata nafasi hiyo.
Serikali kupitia TAMISEMI imeitisha mkutano wa wadau ili kutoa maoni yao juu ya maboresho ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akifungua mkutano huo leo, jijini Dodoma, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Dkt.Festo Ndugange amesema serikali ya Rais Dkt. Samia imedhamiria kuweka uwanja sawa wa kisiasa kwa vyama vyote vilivyosajiliwa nchini.
Wadau wakifuatilia ufunguzi wa Mkutano |
Dkt.Dugange alisema maoni yote yatakayotolewa yatapokelewa na kufanyiwa kazi na kwamba watu wasiogope kutoa maoni kwani hakuna maoni madogo wala makubwa.
0 Comments