Mamba |
NA MWANDISHI WETU-RUFIJI
Pamoja na kuwepo kwa tishio la mamba kwenye baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na mafuriko wilayani Rufiji, mkoani Pwani, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeruhusu wavuvi kuendelea na shughuli zao kwani imeimarisha ulinzi kwenye maeneo yote hatarishi.
Moja ya shughuli zinazowaingizia kipato wakazi wa Kata ya Utete wilayani Rufiji mkoani Pwani ni uvuvi, ambapo wamekuwa wakiutumia mto Lugongwe kuendesha shughuli zao hizo.
Hata hivyo tangu kutokea kwa mafuriko kumekuwa na tishio la kuongezeka kwa mamba kwenye mto huo hali iliyowafanya wavuvi wengi kusitisha shughuli zao kwa kuhofia kuliwa na mamba.
Hofu hiyo iliwekwa wazi na mmoja wa wavuvi kwenye mto huo Hamis Ipombo ambaye ni mkazi wa mamlaka ya mji mdogo Utete, amesema awali walikuwa na hofu ya kuingia mtoni kutokana na kuwapo kwa mamba.
Ipombo amesema uwepo wa TAWA kwenye eneo hilo pamoja na kuwapa elimu wavuvi imewapa faraja kwani wanaendelea na zoezi la uvuvi huku wakiwa hawana wasiwasi.
Kiboko |
“Elimu tuliyopewa na TAWA juu ya kujua namna sahihi ya kujiepusha na hatari za mamba imetusaidia kurejea kwenye shughuli zetu za uvuvi, lakini pia askari wa TAWA tuko nao muda wote, wanafanya doria, kwakweli hatuna hofu kabisa na ujio wao ni faraja kwetu.”
Ipombo anasema ni kweli kumekuwa na ongezeko la mamba kwenye mto Lugongwe na kama TAWA wasingeingilia kati kutoa elimu na kufanya doria ni wazi hali ingekuwa mbaya zaidi, kwani sasa wamejua namna ya kujikinga na mamba na viboko.
“Ni kweli kuna mamba wameingia kwenye mto Lugongwe wakiletwa na mafuriko kutoka kwenye mito mengine na mamba ndio hatari zaidi tofauti na viboko wao hawana madhara sana, tunashukuru uwepo wa TAWA umekuwa na faida kubwa, hatuna hofu tena,”alisema.
Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja |
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Utete, Hawa Mtopa, amesema TAWA wamewafanya kuishi kwa amani bila kuhofia wanyamapori hatari.
“Kilio chetu kikubwa kilikuwa ni ongezeko la wanyamapori hatari kwa binadamu kama vile mamba na viboko, lakini sasa pamoja na kuwepo kwa wanyama hao ila hali ni shwari, hatuna hofu tena, elimu iliyotolewa na TAWA imewaingia wananchi na doria inayofanywa na askari wa Wanyamapori imeleta tija kubwa,”alisema Diwani Mtopa.
Nae Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja alisema ni jambo la fedheha kwa TAWA kuona binadamu wanakufa kwa sababu ya kuuliwa na mamba, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha binadamu wanakuwa salama na shughuli zao zinaendelea kama kawaida.
0 Comments