Ticker

7/recent/ticker-posts

DKT. BITEKO: BWAWA LA NYERERE LIKO SALAMA,AWAPA POLE WAATHIRIKA WOTE WA MAFURIKO

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko

NA. MWANDISHI WETU

Pamoja na mvua kubwa kunyesha kwenye maeneo mbalimbali nchini na kuleta athari mbalimbali, Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) liko salama na ndilo limekuwa msaada mkubwa wa kupunguza athari za mafuriko kwenye maeneo ya karibu.

 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko Aprili 18, 2024  jijini Dodoma  katika mahojiano ya moja kwa moja katika kipindi cha  Jambo Tanzania cha TBC.

 

Mahojiano hayo yalilenga Maonesho ya Wiki ya Nishati 2024 yanayoendelea katika Viwanja vya

Bunge, jijini Dodoma. Dkt. Biteko amesema JNHPP lipo salama kutokana na kujengwa kisayansi na

hivyo kuendelea kuzalisha umeme kupitia mtambo namba tisa huku mitambo

mingine miwili ikiwa ukingoni kukamilika.

 

“Bwawa letu lipo salama kwani limejengwa kisayansi, ujazo wake wa maji ni mita za ujazo 183 na kwa takwimu za leo  ni mita za ujazo 183.4, huko nyuma maji yalikuwa yakiingia mengi sana kwa kiasi cha

mita za ujazo 8400 kwa sekunde hivyo yalipaswa kupunguzwa ili kuendana na ujazo wa bwawa,” amesema Dkt. Biteko.

 

Kuhusu Bwawa hilo kupunguza athari, amesema  bila ya  kuwepo kwa Bwawa hilo athari za mvua zingeanza kuonekana tangu mwezi Oktoba mwaka jana, lakini hali hiyo haikutokea mapema kwa sababu maji yalikuwa yakiijazwa katika bwawa kwa ajili ya kuzalisha umeme.

 

Ameongeza kuwa, Wizara ya Nishati na TANESCO ilishabaini uongezekaji

wa maji katika mto Rufiji kuanzia mwezi Februari, mwaka huu na tahadhari ilianza kutolewa kuhusu  kasi hiyo ya maji ili kuanza

kuchukua hatua  stahiki.

 

ATOA POLE WA WAATHIRIKA WA MAFURIKO

Dkt. Biteko ameeleza kusikitishwa kwake na athari zilizotokea kutokana na mafuriko yaliyosababisha athari katika maisha ya watu na mali zao na kueleza kuwa  Serikali inafanya kila jitihada kurejesha hali ya kawaida  kwa wananchi waliokumbwa na maafa hayo.

 

NISHATI SAFI

Kuhusu utekelezaji wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia nchini, Dkt. Biteko amesema kuwa, watu wengi bado wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia kama vile mkaa na kuni na wananchi wachache wanatumia gesi na

nishati nyingine kama vile umeme.

 

Hata hivyo ameweka wazi kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha ndani ya miaka 10 ijayo, 

asilimia  80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia na tayari Serikali imepitisha Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ikiwa

ni moja ya njia za utekelezaji wa ajenda hiyo ambayo inanadiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ameongeza kuwa, katika kutekeleza mpango huo wa Nishati Safi ya Kupikia, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, imeshatoa waraka wa kutotumia kuni na mkaa kwa taasisi  zinazolisha watu kuanzia 100 na

zaidi kama vile Shule na Magereza.

 

UMEME WA UHAKIKA

Kuhusu upatikanaji wa umeme wa uhakika Dkt. Biteko amesema kuwa kwa sasa uzalishaji umezidi mahitaji hivyo kinachofanyika sasa ni kuboresha miundombinu ya umeme ikiwemo ya kusafirisha umeme kwani baadhi ya sehemu laini za umeme ni ndefu sana hivyo vitajengwa vituo vya kupoza umeme takriban 83 nchini ili kuondoa athari za watu wengi kutopata umeme pale laini inapopata hitilafu.

 

BEI YA GESI

Akiongelea bei ya Gesi, Dkt. Biteko amekiri kuwa  bei ni kubwa  na kueleza kuwa, Serikali inaangalia kwa karibu sana suala hilo ili kuweza kupunguza gharama na hii haiishii kwenye gesi pekee bali kwenye majiko banifu na katika mwaka huu wa fedha Serikali itaanza kutengeneza majiko ya Bayogesi kwenye nyumba za wananchi wanaofuga ili watumie nishati hiyo kwa ajili ya kupikia.

 

 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments