Ticker

7/recent/ticker-posts

WAKULIMA WA MKONGE TANGA WALIA NA SOKO

​Jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kutaka kukirejeshea uhai kilimo cha Mkonge nchini ni kama zinadidimizwa na baadhi ya wadau wa zao hilo la biashara hasa wanunuzi. 

Wakulima kwa upande wao wameamua kumuunga mkono Rais Samia kwa kuhakikisha wanayafufua mashamba yao, hata hivyo wanajikuta wakiishia hamu ya kuendelea kulima mkonge kutokana na kukosekana kwa soko la uhakika. 

Hadi sasa ndani ya mkoa wa Tanga yapo mashamba matano makubwa yenye katani za kutosha ambayo ni Magoma, Mgombezi, Hale, Mwelya na Magunga, lakini hakuna wa kuzinunua. 

Kukosekana kwa mnunuzi kumewaibua wakulima kulalamika, malalamiko yao wanayaelekeza kwa mnunuzi wanaemtegemea ambae ni kampuni ya WEFARM. 

 WEFARM ameshindwa kununua katani yote iliyopo ghalani kwa zaidi ya mwezi sasa na Bodi ya Mkonge haioneshi jitihada zozote za kumshinikiza mnunuzi huyo kufuata matakwa ya kisheria, badala yake mnunuzi huyo amekuwa akinunua katani kidogo. 

 Katika kudhihirisha kuwa si mnunuzi wa uhakika, WEFARM amefikia hatua ya kubagua madaraja ‘Grade’ za Mkonge. Kampuni ya WEFARM licha ya kushinda tenda, ya kununua Katani, lakini imeshindwa kutimiza matakwa ya tenda hiyo hali inayowasababishia mateso wakulima pamoja na Vyama vya Ushirika wa Mkonge (AMCOS). 

Mmoja wa wawakilishi wa WEFARM aliyejulikana kwa jina moja la Revocatus, alishindwa kujibu na kumtaka mwandishi wetu akaiulize Bodi ya Mkonge.

“Hayo mambo waulize Bodi ya Mkonge.” Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge, Saddy H. Kambona, amesema hajapata taarifa zaidi kwa kuwa alikuwa likizo. 

 “Sijajua kwa sababu mimi nilikuwa likizo. Kuhusu kuwa na taarifa za mwenendo wa mnunuzi, Kambona alisema ni mpaka akae na wenzake ndio ayajua. 

 “Mkataba wa sasa siufahamu kwani mkataba wa awali, ulimtaka mnunuzi kulipa ‘invoice’ ndani ya siku saba, sijui ni siku ngapi, lakini mkataba wa awali mnunuzi alitakiwa kulipa invoice ndani ya siku saba, akishindwa inatakiwa AMCOS wapeleke taarifa tena, na akishindwa ndio tunaangalia cha kufanya,” alisema.  

Kambona alipoulizwa sababu za ofisi yake kushindwa kumchukulia hatua mnunuzi huyo, alisema “taarifa kwetu hazijafika, vyama havileti taarifa. Sisi tunahudumia mashamba mengi, kwa hiyo ni lazima tuletewe taarifa.” 

 Alisema, suala la kununua katani kwa haraka linatokana na maghala kutokuwa na Bima, “hivyo pakitokea cheche tu, kunakuwa na hasara kubwa.” 

Hata hivyo, Kambona alisema, ni kosa kwa AMCOS kuamriwa kuandika ‘invoice’ za baadhi ya katani iliyopo, kwa kuwa mnunuzi anapaswa kununua katani yote kwa mujibu wa mkataba. 

Alipoambiwa mnunuzi hafanyi hivyo, alisema “hilo ni kosa.” Kuhusu hatua zaidi dhidi ya WEFARM endapo taarifa ya kushindwa kununua katani itathibiti alisema, “sio jambo rahisi kuchukua hatua haraka, tunaweza kufanya hivyo tukaingia hasara. 

“Huko nyuma tuliwahi kufanya hivyo, lakini sasa lazima taratibu kadhaa zipitiwe ili kufikia hatua hiyo,” alisema. WEFARM imekuwa ikiwataka wenyeviti wa AMCOS kuandika ‘invoice’ kwa baadhi ya ‘grade’ za katani pekee huku ikipuuza grade zingine. 

 “Hapa alisema tuandike invoice ya SSUG pakee, lakini wenyeviti wenzangu wakasema tuandike invoice za mzigo wote uliopo ghalani maana ndio taratibu zinataka.

 “Matokeo yake wiki iliyopita kalipa SSUG pekee, tena kwa mashamba yaliyo na invoice ya kiwango kidogo cha pesa yale mashamba yenye kiwango kikubwa cha pesa kashindwa kulipa. Sijui bodi ilitumia kigezo gani kumpitisha?,” alihoji. 

 Nae Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Mgombezi (Mgombezi Amcos), Rashid Msemo alikiri kuwepo kwa tatizo la ununuzi wa katani. 

“Ni kweli kuna kikubwa cha wakulima, kukataa hili nitakuwa nimesema uongo. Tatizo hilo limesababisha kazi za vyama kusimama. 

 “Marobota yamejaa kwenye maghala, hivi karibuni alinunua katani chache mno n ahata pesa aliyotoa haikukidhi kuendelea na kazi za vyama vyetu, hatuelezwi shida ni nini,” alisema. 

Msemo alisema, katani ilionunuliwa ni grade ya kwanza ya UG ambayo ni kidogo na hapa juzi kanunua SSUG kidogo na zingine kaacha,” alisema na kuongeza; “Mnunuzi kama ataendelea kubagua grade za katani, hili jambo litakuwa baya zaidi, linaweza kusababisha vyama kufa. Mkataba unamtaka mnunuzi kununua katani yote,” alisema. 

Ofisa mmoja kutoka Hale alisema, waliongea na Bodi ya Mkonge kuhusu hatua ya WEFARM kubagua grade za kununua, na kwamba walijibiwa ‘acha tumuangalie kwanza.” “Awali kutokana na mashaka, tulikuwa tukiuliza mbona mnunuzi mwenywe hanunui, tukatahadharisha yasije kutokea yale ya Dk. Shika. 

Bodi ilitueleza kwamba, imefanya utafiti na kampuni ni halisia. Bado tunasubiri,” alisema. Mwenyekiti wa wenyeviti wa vyama vya ushirika vya mkonge Tanga, Shadrack Lugendo alisema kuwa, bado wanasubiri mnunuzi aendelee kununua katani uliopo kwa sasa. 

 “Nami najua kuna kilio kwa wakulima lakini ujue huyu ni mnunuzi mpya, ni tofauti na mnunuzi anayeendelea kwa maana taratibu zake zote zinakuwa sawa na anaendelea nazo. Huyu wa sasa ni mpya,” alisema. 

 Akizungumzia hatua ya WEFARM kununua katani kwa kubagua grade, alisema mkataba unamtaka kununua mkonge wote, hivyo anapaswa kutafanya hivyo. Serikali ya Rais Samia mara kadhaa imekuwa ikifanya juhudi kuhakikisha, zao la katani linaboreshwa na kuhakikisha dhana ya ‘dhababu ya kijani’ inatimia. 

 Kupitia Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe serikali iliagiza kuchukuliwa hatua kwa mtu yeyote anayefanya vitendo vya kuhujumu zao hilo. 

 Desemba 12,2023, Waziri Bashe aliagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama Tanga kuchunguza kwa kina ili kubaini kampuni iliyosafirisha nyuzi za katani zilizochanganyika na uchafu na kumchukulia hatua. 

 Katika kikao kilichofanyika 16 Julai 2022, Morogoro, Waziri aliagiza kuhakikisha kuwa, kilimo cha mkonge kinakuwa bora na kwamba, serikali ilianza kuchukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha zao hizlo linapata thamani. 

 Serikali iliweka malengo kuwa, katika kipindi cha 2020-2025, Bodi ya Mkonge ihakikishe inaongeza uzalishaji wa mkonge hadi kufikia tani 120,000 kwa mwaka.

Post a Comment

0 Comments