NA MWANDISHI WETU
Utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya nchini umeonesha kuwa mkoa wa Lindi umeathirika kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa Vikope, ambapo wilaya ya Ruangwa na Nachingwea zinaongoza.
Katika wilaya hizo takribani watu 1770 wameathirika na ugonjwa huo, huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni uchafu kwani ugonjwa huo unasababishwa na bakteria aina ya ‘Chlamydia trachomatis’ wanaoenezwa na nzi.
Mratibu wa huduma za macho mkoani Lindi, Dkt. Mwita Machage amesema Wizara ya Afya na Shirika lisilo la kiserekali la Sightsavers walipiga kambi wilani Nachingwea ili kuendela kuwabaini na kuwatibu waathirika wa ugonjwa huo.
Dkt. Machage amesema utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya mwaka 2021-2022 ulionesha wilaya ya Ruangwa inaongoza kwa kuwa na wagonjwa 890 ikifuatiwa na Nachingwea yenye wagonjwa 885 na Liwale ikiwa na wagonjwa 128.
Alisema katika kuhakikisha wanautokomeza ugonjwa huo, hadi kufikia mwaka 2026 watahakikisha wanawafikia wagonjwa wote katika wilaya hizo ili kuwapatia huduma ya usawazishaji.
“Sightsavers linashirikiana na Serikali katika kuhakikisha wagonjwa wote wa Vikope waliofanyiwa utafiti hadi kufikia mwaka 2026 wote wanapata matibabu na kuondokana na upofu mkoani Lindi,”alisema Dkt. Mwita.
Meneja mradi wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka Sightsavers Tanzania, Peter Kivumbi, amasema ugonjwa wa Vikope unaweza kumsababishia mtu upofu.
Kivumbi amesema kitendo cha kope kukwaruza kioo cha jicho kila wakati kinatengeneza kovu linalosababisha upofu.
Alisema njia sahihi ya kujilinda na ugonjwa huo ni watu kuzingatia usafi wa mazingira, kunawa na maji safi na salama mara kwa mara.
0 Comments