NA ELIAS SHADRACKMichezo ya Ligi Kuu ya NBC inaendelea, Simba, Yanga na Azam zimeanza kuhitimisha michezo yao ya viporo.
Tayari Simba na Yanga hadi kufikia Februari 7,2024 kila moja ilikuwa imeshacheza michezo miwili hii ni mara baada ya kurejea kwa michezo ya ligi hiyo iliyokuwa imesimama ili kuipisha timu ya taifa, Taifa Stars kushirki fainali za AFCON zinazoendelea nchini Ivory Coast.
Bahati mbaya Stars imetolewa kwenye hatua ya makundi, hivyo ligi inaendelea na ni Simba pekee ndio imeweza kushinda michezo yake miwili ambayo imeshacheza huku Yanga ikishinda mchezo mmoja na kutoka sare mchezo mmoja.
Simba imeshinda ugenini michezo yake yote, ambapo ilianzia Kigoma mbele ya Mashujaa ikaichapa bao 1-0 kisha ikaelekea Tabora mbele ya Tabora United, huko ikachapa timu hiyo bao 4-0.
Matokeo hayo yanatazamwa na wachambuzi wa soka kama kasi mpya iliyorejea nayo Simba, ikiwa na lengo moja tu la kukwea kileleni.
Ikumbukwe kuwa kwa sasa Simba inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 29, nyuma ya Azam yenye pointi 31 na Yanga yenye pointi 34 kileleni.
Kiufundi katika michezo miwili waliyocheza wababe hao wa soka Tanzania, Simba imeonekana kuwa bora kuliko Yanga.
Usajili mdogo uliofanywa na Simba wakati wa dirisha dogo, umeonesha kuwa na faida tofauti na ilivyo kwa wapinzani wao, ingawa bado ni mapema kuwasakama wachezaji wapya wa Yanga, lakini waswahili wanasema nyota njema huonekana asubuhi.
Hoja hii inasukumwa na kile kilichofanywa na wachezaji wapya wa Simba, kwa kiasi kikubwa kwenye michezo miwili waliyopata nafasi kila mmoja kaonesha mchango wake kwa timu.
Omar Jobe, akiwa kwenye mchezo wake wa pili ameweza kupachika bao kama ilivyokuwa kwa Fredy Michael.
Wachezaji hawa wawili Jobe na Fred ni usajili mpya ndani ya kioosi cha Simba.
Mwanzo wao huo unadhihirisha ubora wao na pengine wanaweza kuwa msaada mkubwa kwa Simba kuwania ubingwa waa ligi hiyo ambao imeupoteza kwa misimu miwili mfululizo.
Hata hivyo wachezaji hao kama ilivyo kwa wale wa Yanga bado wanahitaji muda zaidi na uwezo wao utapimwa zaidi kwenye michezo ijayo kama ule wa kesho Ijumaa Februari 9,2024 dhidi ya Azam utakaochezwa ndani ya dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza.
0 Comments