Mkuu wa Kitengo cha Sera na Usimamizi wa Maliasili, Allen Mgaza, akitoa ufafanuzi juu ya masuala ya uhalifu dhidi ya Wanyamapori kwa Waandishi wa Habari za Mazingira (hawapo pichani)
Biashara ya usafirishaji haramu wa Wanyama pori inatajwa kuwa kwenye orodha ya biashara zinazoingiza fedha nyingi kwenye mitandao ya wafanyabiashara za magendo duniani.
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na wataalamu zimebaini kuwa kiasi cha dola za Marekani kati ya milioni 7-23 hupatikana kwa mwaka kutokana na biashara kuu nne haramu zikiongozwa na dawa za kulevya, madini, usafirishaji wa binadamu na wanyama pori (viumbe hai).
Kaka kuona ni miongoni mwa waathirika wakuu wa biashara hiyo haramu, anawindwa zaidi katika nchi nyingi duniani na Tanzania ikiwemo.
Wakati leo ikiwa ni siku ya maadhimisho ya Kakakuona duniani, ukweli ni kwamba mnyama huyo anashika nafasi ya kwanza katika orodha ya mamalia wanaosafirishwa kwa magendo duniani.
Taasisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Uhifadhi wa Mazingira ulibaini kuwa kati ya mwaka 2000 hadi 2019, karibu Kakakuona 900,000 walisafirishwa katika nchi mbalimbali dunini, huku China ikitajwa kuwa mnunuzi mkuu.
Mwaka 2009 mji wa Borneo nchini Malaysia zilikamatwa tani 27 za nyama ya Kakakuona iliyokadiriwa kuwa na thamani ya paundi milioni 1.6.
Kakakuona ambaye pia hujulikana kama "Scaly anteaters" ndiye mamalia pekee mwenye magamba duniani, chakula chao kikuu ni mchwa na wadudu ambao hufanikiwa kuwakamata kutokana na ulimi wao mrefu.
Kakakuona ni wanyama wadogo na mwenye mwili mkubwa hukadiriwa kuwa na urefu wa mita 1.8 na uzito wa kilo 30.
Mnyama huyu anaponzwa na magamba na nyama yake. Magamba yake hutumiwa zaidi kwenye dawa za jadi za Kichina, watumiaji wanaamini magamba na kucha zake husaidia kutibu magonjwa ya pumu na saratani na nyama yake inadaiwa kuongeza nguvu mwilini, ingawa hadi sasa hakuna tafiti za kitaalamu zilizothibitisha hayo.
Mhifadhi Wanyamapori Tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, Makene Ngoroma akiwa amemshika mmoja wa Kakakuona aliofanikiwa kuwaokoa. |
AFRINEWSSWAHILI iliongea na Mhifadhi Wanyamapori Tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, Makene Ngoroma ambae anajihusisha na uuokoaji wa wanyma walio kwenye hatari ya kutoweka.
Tangu mwaka 2011 hadi sasa Ngoroma ameweza kuokoa Kakakuona 15 waliokuwa kwenye hatari ya kuawawa, akizungumzia maadhimisho ya siku ya Kakakuona duniani, anasema serikali inapaswa kutilia mkazo eneo la kuhifadhi na kufanya tafiti za aina tatu za kakakuona wanaopatikana Tanzania ili wanyama hawa wasitoweke kwani ni urithi tulionao kwa vizazi vijavyo.
“Hivi karibuni tumeona NGO imeanzishwa ya utafiti na uhifadhi wanyamapori iliyoko Morogoro, imeanza kutafiti na kuhifadhi mnyama huyu anaekaribia kutoweka pia nilipata bahati ya kuhudhuria mafunzo yao ya jinsi ya kumhamisha mnyama huyu na kumuokoa kwa kumpa huduma ya kwanza.
“Inatia hamasa kuona ni jinsi gani wadau walivyoamua kumuokoa na kumhifadhi mnyama huyu kwa Tanzania, lakini pia nimeona TAWIRI wanaanza utafiti wa mnyama huyu Tanzania ili kumhifadhi kwa ajili ya kizazi kijacho, hata hivyo jitihada zinahitaji kuongezwa zaidi.
Kwa sasa adui mkubwa wa Kakakuona ni binadamu, upole wake unamfanya kukamatwa kwa urahisi, nje ya binadamu mnyama huyo hawezi kudhuriwa na mnyama yeyote mkali hata chui chui hawezi kumla Kakakuona kwa sababu ya magamba magumu kwenye miili yao.
Inaelezwa kuwa idadi ya Kakakuona inapungua kwa kasi kwenye ukanda wa nchi za Afrika ya Kati, hivyo juhudi zaidi zinahitajika katika kuwahifadhi ili wasitoweke kabisa.
SIKU YA KAKAKUONA DUNIANI
Februari 17 ya kila mwaka huwa ni siku ya Kakakuona Duniani, siku hii huwa ni fursa kwa wapenda Kakakuona kujumuika pamoja katika kukuza ufahamu kuhusu mamalia hawa wa kipekee na masaibu wanayokutana nayo.
Idadi ya Kakakuona inapungua kwa kasi katika bara la Asia na Afrika, kuna mahitaji makubwa ya magamba yake yanayotumiwa katika dawa za jadi, sanjari na nyama yake.
Ili kukilinda kiumbe hiki, jamii inatakiwa kuonesha upendo wao na kusaidia kuongeza ufahamu kwa jamii ili waondokane na imani potofu kuwa magamba yake ni dawa.
MRADI WA USAID TUHIFADHI MALIASILI
Shirika la Misaada la Marekani USAID kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili wamedhamiria kuwa sehemu ya kumlinda mnyama huyo na wanyama wengine walio kwenye tishio la kutoweka duniani.
Mkuu wa Kitengo cha Sera na Usimamizi wa Maliasili wa mradi wa USAID Tuhifadhi Malisili, Allen Mgaza anaweka wazi kuwa ipo haja ya jamii kushiriki kwa pamoja katika kuwalinda wanyama walio kwenye hatari ya kutoweka akiwemo Kakakuona na Tembo.
“Hawa wanyama wana umuhimu mkubwa sana katika maisha ya binadamu na viumbe wengine, kutoweka kwao kutatulazimisha kuja kutumia picha ili kuwaonesha watoto wetu aina za wanyama hawa, hawatakuwepo,”amesema.
Akitoa uelewa kwa Waandishi wa Habari za Mazingira juu ya namna ya kupambana na uhalifu dhidi ya Wanyamapori, Mgaza amekiri kuwa Kakakuona wamekuwa wakiwindwa sana hali inayotishia kutoweka kwao.
Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umelenga kulinda shoroba saba nchini zinazotumiwa na wanyama katika kusaka malisho na maji, lakini pia utatumika katika kutoa elimu ya kukabiliana na uhalifu dhidi ya Wanyamapori.
Washiriki wa mafunzo ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili wakiwa katika picha ya pamoja. |
0 Comments