Mama Pili Mtambalike akitoa maelezo ya namna ya kuandika habari za uhifadhi zenye mvuto. |
NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI,BAGAMOYO
Tasnia ya Habari nchini imebarikiwa kuwa na manguli wa uandishi, uhariri na uchambuzi wa kina wa masuala mbalimbali yanayoigusa jamii moja kwa moja.
Mmoja wao ni Mama Pili Mtambalike, huyu ni mwandishi wa habari, mkufunzi na mshauri wa masuala ya habari mkongwe.
Uwezo wake katika eneo hilo umemfanya kuwa na heshima ndani na nje ya nchi, si mwoga wa kusema, kuonekana wala kuandika popote atakapokuwa iwe nyuma ya kipaza sauti ndani ya studio za redio, kamera za Televisheni au nyuma ya kicharazio (Keyboard) cha kompyuta.
Mara zote amekuwa akiitumia kalamu yake kwa maslahi mapana ya nchi na wananchi wake.Maandiko yake kwenye kurasa za magazeti mbalimbali Tanzania yamekuwa ni suluhu ya changamoto kadhaa zinazowakabili wananchi.
Sauti yake popote inaposikika hupenya barabara masikioni mwa watoa maamuzi, kwa sababu mara zote kauli zake zinabeba maneno yanayochagiza na kuhitaji haki na usawa katika jamii.
Sauti na maandiko yake yamekuwa ni vugu vugu la kudai uhuru wa vyombo vya Habari nchini, hitaji lake mara zote limekuwa ni kutaka kuwepo kwa kuvumiliana baina ya waandikwa na waandishi.
Anaamini kufunguliwa mashtaka, kutekwa pamoja na vyombo vya habari kufungiwa na kutozwa faini kubwa kubwa yalikuwa ni moja ya mambo yaliyofifisha na kutowesha uhuru wa Habari nchini.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo wa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, wakimsikiliza mtoa mada Mama Pili Mtambalike (aliyesimama) |
“Tuyatafute. Tusisubiri tupewe. Kazi za kuongea na watu ambao wanahusika katika kufanya mabadiliko hasa ya sheria, kanuni ni ya kwetu. Na tuelewane kuwa sisi ni watu ambao ni wazalendo wa nchi hii, tunaipenda nchi yetu.”
Haya ni baadhi ya maneno aliyoyaongea Mama Mtambalike alipofanya mazungumzo madogo na AFRINEWS SWAHILI, Februari 15, 2024, Bagamoyo mkoani Pwani mara baada ya kutoa elimu nzito kwa Waandishi wa Habari za Mazingira juu ya namna sahihi ya kuandika Habari za mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaoendeshwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).
Katika dakika 60 alizosimama mbele ya waandishi wa Habari kuwasilisha mada yake hakuna hata sekunde moja iliyokosa kubeba ujumbe mahsusi wa namna ya kuandika Habari ama Makala inayomvutia msomaji.
Nguli huyu wa Habari anakataa dhana ya kuwa watu hawapendi kusoma, yeye anaamini watu wanapenda kusoma sana isipokuwa hawapendi kusoma vitu visivyowavutia.
“Nakwambieni, hakuna mtu asiyependa kusoma, ila sisi waandishi ndio tunawafanya wasisome kwa sababu hatuandiki maandiko yanayomvutia msomaji.
“Andikeni maandiko yanayovutia wasomaji, yaliyojaa taarifa za kweli na takwimu sahihi kisha muone kama mtu hajasoma andiko lako kuanzia mwanzo hadi mwisho.”amesema Mtambalike.
Kuhusu Waandishi wa Habari kuitumia kwa usahihi mitandao ya kijamii, Mama Mtambalike amesema bado hilo halijafanyika kwa usahihi na ikitokea likafanyika basi Waandishi watakuwa chachu ya mabadiliko kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Amesema Habari za uhifadhi zina tija kubwa kwa nchi na ni jukumu la Waandishi wa Habari za Mazingira kuhakikisha wanaandika Makala nzuri ili zisaidie kuleta tija kwenye uhifadhi na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mkongwe huyu wa Habari anaamini Waandishi wa Mazingira wanapaswa kuwa na utayari wa kuandika Habari na Makala zilizobeba chachu ya mabadiliko kwa jamii.
0 Comments