Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) Dastan Kamanzi,akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari za Mazingira (hawapo pichani) |
NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI-BAGAMOYO
Mara zote ukweli huwa ni mchungu pale unaposemwa, hata hivyo ukweli huwa ni tiba kwa aambiwae hasa akiamua kuupa sura na mtazamo chanya.
Ukweli unaweza kuzalisha maumivu na kutengeneza chuki kwa mtu anaeuambiwa na kuukataa kwa kudhani anaonewa ama anabagazwa kwa namna moja ama nyengine.
Mtazamo hasi unaweza kumsukuma anaeambiwa ukweli kupotea kabisa badala ya kubadilika na hili ndilo tatizo linalowakumba wengi waukataao ukweli, badala ya kubadilika wao hubeba hinda mioyoni mwao.
Katika maisha yangu ndani ya tasnia ya Habari, nimekutana na watu wachache ambao sura, vinywa, mioyo, matendo na maneno yao yamejaa ukweli mchungu, ukweli unaokulazimisha kujitafakari upya.
Miongoni mwa hao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) Dastan Kamanzi, huyu jamaa haoni haya kuusema ukweli katikati ya maumivu.
‘Mwamba’ hatafuni maneno, kama unanuka atakwambia unanuka na kama ni masikini wa mawazo ya Habari hatakuficha, atakueleza ukweli, uamuzi utabaki kwako, uukubali ukweli wake ili ubadilike au uukatae na kubaki na umasikini wako.
Kamanzi anasema kama wewe ni masikini wa mawazo ya Habari huwezi ‘kutoboa’ kwenye tasnia hiyo, badala yake utaishia kuandika vitu vyepesi vyepesi visivyo na tija kwa jamii.
Anaamini kama wewe ni mwandishi wa Habari na unaweza kulala usiku kucha bila hata ya kusumbuliwa na wazo la Habari litakalouondolea usingizi wako na kukufanya uamke kuliandika mahali, basi jua wewe ni mwandishi wa habari masikini wa mawazo.
Kwamba kwake mwandishi wa Habari makini ni yule mwenye utajiri wa mawazo ya Habari anaeweza kuukosa usingizi kwa sababu hiyo.
Anasema mara zote mwandishi wa Habari ni yule anaeandika mambo yanayochochea matokeo chanya kwenye jamii na ana nafasi kubwa ya kuwa tajiri wa mawazo na fedha.
“Mwandishi wa vitu vyepesi vyepesi asiye na mawazo chanya ya habari huyo ataishia kusaka hela ya kula tu.” Haya ni maneno magumu yanayogusa sehemu ya ndani ya moyo, ingawa huo ndio ukweli.
Unapomsikiliza Kamanzi kwa mara ya kwanza na pengine kwa jicho la wasiwasi anapozungumza unaweza kudhani huyu jamaa ni mjivuni anaesema mambo yasiyowezekana ndani ya tasnia ya Habari,fikra ambazo ni batili.
Bahati mbaya ukisalia na mawazo yako hayo, kwakweli hutoweza kufanya hata theluthi ya anachokisema, lakini ukifungua bongo na kuutazama ukweli wake kama chachu ya mabadiliko, amini hakuna jambo linaloshindikana chini ya jua.
“Mwandishi wa Habari makini anapaswa kuitambua thamani yake, anapaswa kuwa na uwezo wa kuandika kitu chenye kugusa maslahi ya jamii, hana muda wa kupoteza kuandika vitu vyepesi, muda wake ni mali.”
Kamanzi anasema Waandishi wa Habari wamegawanyika katika makundi makuu matatu, kundi la kwanza ambalo linabeba idadi kubwa ya watu amelipa jina la (SC&IS -Social Communication and Information Sharing) ikiwa na maana kuwa kundi hili lenyewe linahusisha jamii inayosambaziana taarifa za kawaida ambazo nyingi hazina tija yeyote kwa jamii.
Kundi la pili ni lile alilolipa jina la (PR&PC-Public Relation and Public Communication), hili linahusisha watu wanaotoa taarifa zinazogusa maslahi ya moja kwa moja ya taasisi ama mambo yao.
Eneo hili haligusi maslahi mapana ya umma, na lenyewe linahusisha idadi kubwa ya waandishi wa Habari ambao wanafanya kazi ya kusifia kwa kujua ama kutokujua.
Kundi la tatu linagusa watu wachache na hawa wanajulikana kama (PIJ-Public Interest Journalism), hawa wanabeba maslahi mapana ya jamii.
Kazi za jamii hii ya PIJ, zina tija ya moja kwa moja kwa jamii, maandiko yao yameegemea kutatua changamoto zinazowakabili watu wengi, kundi hili haliangalii maslahi binafsi ama kuandika kwa kujifurahisha.
Kwa mujibu wa Kamanzi, kundi hili limebarikiwa utajiri wa mawazo sanjari na fedha, uwezo wao wa kufukunyua mambo unawapa nafasi kubwa ya kuheshimika mbele ya jamii kubwa huku ikichukiwa na jamii ndogo ya wanyonyaji.
Matamanio ya Kamanzi ni kuona kundi kubwa la Waandishi wa Habari wa Tanzania wanatoka kwenye makundi mawili ya kwanza na kuangukia kwenye kundi la tatu la PIJ.
“Waandishi wa Habari wakiondoka kwenye utamaduni wa kuandika Habari nyepesi nyepesi na kujikita kwenye kundika Habari zinazogusa maslahi ya jamii, ni wazi wao watakuwa chachu ya mabadiliko ya nchi na maisha yao kwa ujumla.”
Kamanzi ameyasema hayo Februari 16,2024 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, alipokuwa akiwanoa waandishi wa Habari za Mazingira kwenye mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Waandishi hao kuandika Habari zenye tija zinazohusu masuala ya Uhifadhi.
Takribani waandishi 20 wanatarajia kuwa chachu ya mabadiliko kwenye masuala ya uhifadhi na uhalifu dhidi ya wanyama pori kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID).
Kamanzi akitoa mafunzo kwa Waandishi wa Habari za Mazingira waliohudhuria mafunzo ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili. |
0 Comments