Ticker

7/recent/ticker-posts

WAGONJWA WA VIKOPE 1627 MKOANI PWANI KUPATIWA MATIBABU BURE

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Bi. Regina Bieda (mwenye miwani akisikiliza maelezo ya ugonjwa wa Vikope)

 NA JIMMY KIANGO-AFRINEWSSWAHILI-PWANI

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Sightsavers wanatarajia kutoa matibabu ya bure ya ugonjwa wa vikope kwa wagonjwa 1,627 waliopo katika wilaya tatu za mkoa wa Pwani.

 

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele umeonesha kuwa tatizo la ugonjwa wa vikope kwenye mkoa wa Pwani katika Halmashauri za Kibaha DC, Chalinze na Bagamoyo ni kubwa.

 Akithibitisha hilo leo Februari 21,2024 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Bi. Regina Bieda alisema wilaya ya Kibaha DC inao wagonjwa 435, Chalinze wagonjwa 804 na Bagamoyo kuna wagonjwa 388.

 Bi. Bieda ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa kutokomeza ugonjwa wa macho (vikope) katika Halmashauri ya Kibaha, uliofanyika Kibaha mkoani Pwani. 

 

“Hali ya ugonjwa wa vikope si nzuri mkoani kwetu, kipekee kabisa ningependa kutoa shukurani kwa shirika la Sightsaver na timu ya uendeshaji wa Huduma za Afya mkoa wa Pwani na Halmashauri ya Kibaha kwa kufanikisha uzinduzi wa mradi wa kutokomeza ugonjwa wa macho wa vikope.

 “Dhamira kuu ya serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuthamini afya za wananchi wake na ndio maana inafanya jitihada mbalimbali za kushirikiana na wadau ili kuwasogezea huduma za afya karibu.”amesema.

 

Mkurugenzi huyo ambae amewataka wakazi wa mkoa wa Pwani kuweka mazingira yao safi na salama, amesema kuwa kauli mbiu ya mpango mkakati huo wa kutokomeza vikope mkoani Pwani ni Epuka upofu, ugonjwa wa vikope unatibika, wahi matibabu mapema.

 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Benedict Ngaiza

Akizungumza na AFRINEWSSWAHILI, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Benedict Ngaiza, alikiri kuwa hali ni mbaya na kwamba jitihada za makusudi zinahitajika ili kukabiliana na changamoto hiyo.

 

“Kama alivyosema Mkurugenzi kwenye hotuba yake ya ufunguzi, nikiri hali ni mbaya na kipekee tunaishukuru Sightsavers kwa hatua yake hii ya kutoa matibabu ya vikope bure, hii ni hatua nzuri kwetu katika kupambana na tatizo hili la vikope.”

 

Nae Mratibu wa Macho mkoa wa Pwani, Dkt. Eligreater Mnzava alisema ujio wa mpango huo wa kuwatibu wagonjwa wa vikope bure utasaidia kukabiliana na tatizo hilo mkoani Pwani.

 

Kwa upande wake Meneja wa mradi huo wa kutokomeza vikope kutoka Sightsavers Tanzania, Peter Kivumbi, amasema ugonjwa wa Vikope ni hatari kwani unaweza kumsababishia mtu upofu.

 

Kivumbi amesema kitendo cha kope kukwaruza kioo cha jicho kila wakati kinatengeneza kovu linalosababisha upofu.

 Alisema njia sahihi ya kujilinda na ugonjwa huo ni watu kuzingatia usafi wa mazingira, kunawa na maji safi na salama mara kwa mara. 

Kivumbi amebainisha kuwa kiasi cha shilingi milioni 755 zitatumika kwa ajili ya kutoa matibabu kwa waathirika wa ugonjwa huo.


Meneja wa mradi huo wa kutokomeza vikope kutoka Sightsavers Tanzania, Peter Kivumbi, 

UGONJWA WA VIKOPE NI NINI?

Ni ugonjwa wa maambukizi kwenye macho yatokanayo na kimelea kiitwacho Klamidia Trakomatis. Vimelea vya ugonjwa huu husambazwa na nchi wa majumbani kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwengine. 

 

Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na kope kulalia kioo cha jicho, maumivu ya macho,macho kutoa uchafu na machozi muda wote pamoja na kuanza kupoteza uwezo wa kuona mbali na hatimae mgonjwa kupata upofu wa kudumu kama atakuwa hajapata huduma ya matibabu mapema.

 MALENGO YA MRADI

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeweka mkakati wa kutokomeza ugonjwa wa vikope, mkakati huo unaitwa SAFI ukiwa na maana ya Sawazisha Vikope, Anza matibabu mapema kwa kutumia Antibiotic, Fanya usafi wa uso na Imarisha usafi wa mazingira.

 

Mradi huu upo mahususi kwa ajili ya upasuaji mdogo unaohusisha usawazishaji wa Kope. Wagonjwa watabainika kupitia wahudumu wa afya watakaopewa mafunzo ya awali ya kutambua wagonjwa wa vikope.

Mratibu wa Macho mkoa wa Pwani, Dkt. Eligreater Mnzava
Wahudumu hao watapita kwenye kila kaya katika Halmashauri husika na kufanya uchunguzi wa awali kwa kila kaya,wale watakaobainika kuwa na dalili za ugonjwa huo watafanyiwa uchunguzi wa kina na wataalam wa Afya na kupewa matibabu bila malipo kwa wale watakaothibitika kuwa na ugonjwa wa vikope.

Kwa Kibaha DC mradi huo umezinduliwa leo Februari 21,2024 na utakamilika Machi 2025. Ikumbukwe kuwa moja ya visababishi vya ugonjwa huo ni uchafu wa mazingira, hivyo wito unatolewa kwa watu kuweka mazingira yao safi.

 

Kivumbi akitoa ukielezea ubora wa mradi huo katika uhifadhi wa takwimu.

Mmoja wa maofisa wa Sightsavers akitoa maelekezo ya namna ya kutumia fomu zitakazotumiwa na wataalam
 

Post a Comment

0 Comments