Ticker

7/recent/ticker-posts

YONDO SISTER KUTOKA KUMBI ZA STAREHE HADI MADHABAHUNI

MOJA ya wanamuziki wa kike waliokuwa na uwezo mkubwa wa kuliteka na kulinyanyasa jukwaa ni Yondo Kusala Denise, binti mrembo wa Kikongomani, maarufu kama Yondo Sister.

Yondo Kusala alibeba urembo wa asili pamoja na ule wa kujiongeza, hakuwa mwanamuziki tu, lakini alikuwa ni mwanamuziki mrembo.

Urembo wake uliwasukuma mashabiki wake kumpachika jina la Yondo Sister, hakuna aliyekerwa na muziki wake, alikuwa bingwa wa kustarehesha kwa kuimba n ahata kunengua.

Yondo Sister alilitikisa jukwaa la muziki wa Sokouss kwa zaidi ya miongo miwili, uwezo wake uliwavutiwa mabinti wengi kujiingiza kwenye muziki.  

Alizaliwa Januari 1,1958, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wakati huo ikijulikana kama Belgian Congo.

Alianza kujihusisha na heka heka za muziki mwaka 1970 kama mnenguaji wa bendi ya Rocherettes iliyokuwa chini ya guru la muziki wa dansi Afrika, Tabu Ley.

Yondo aliitumikia pia Zaiko Langa Langa na L'Afrisa International, kote huku akiwa ni mnenguaji.

Pamoja na mambo mengine mwenyewe anaweka wazi kuwa mmoja wa watu waliomvutia zaidi kujiingiza kwenye muziki alikuwa ni dada yake Yondo Nyota Chantal, ambae waliimba pamoja kwenye bendi hiyo.

Akiwa mnenguaji kinara wa bendi hiyo, kamwe hakujua kama anaweza kuimba hadi pale Rachid King mlezi wa vipaji alipokuja kukiona kipaji chake cha kuimba na kumpa nafasi.

King alianza kumuonesha njia sahihi za namna ya kuimba na kuweza kukonga nyoyo za mashabiki wa muziki popote pale duniani.

Uwezo wa kuimba wa Yondo Sister ambae alifikiwa hatua ya kufananishwa na Tina Turner uliongezewa ladha na uwezo zaidi na Lutu Mabangu.

Mabangu alimuongezea uwezo wa kujiamini jukwaani, hivyo basi pamoja na kunengua, lakini alikuwa akiisaka nafasi ya kuimba mbele ya gwiji Tabu Ley. 


Taratibu alianza kuimba kama ‘back up singer’ kwenye bendi ya Lafrisa International, hatimae mwaka 1989 alijiunga na bendi ya  Soukouss Stars.

Uwezo wake wa kuimba uliwalazimisha wenzake kupenda kumuita "Le reine de la Soukouss" wakiwa na maana ya Malkia wa Soukouss.

Baada ya kuona anaweza kusimama mwenyewe  aliondoka ndani ya bendi ya Soukouss na kuanza kufanya muziki wake binafsi.

Hapo ndipo alipoanza kuziteka zaidia nyoyo za wapenzi wa muziki wa dansi na Sokouss Afrika na duniani kwa ujumla. 

Mwaka 1991 alitoa albamu yake ya kwanza aliyoipa jina la "Deviation Bazo", albamu hii ilimtambulisha vilivyo kwenye dunia ya muziki, ilimpa nafasi ya kuzunguka kwenye nchi mbalimbali duniani.

Katika kipindi hichao hakuna mpenda muziki ambaye hakuacha kumfuatilia Yondo Sister, alikuwa ni nuru ya furaha kwenye mioyo ya wapenda dansi.

Ukiiondoa albamu yake ya Bazzo ambayo ndio ilimuingiza mjini, albamu zake nyingine ni pamoja na Derniere Minute aliyoitoa mwaka 1995,  Planete aliyoitoa mwaka 1999, FBI aliyoitoa mwaka 2001 na albamu yake ya mwisho wa Sokouss ni Agenda ambayo aliitoa mwaka 2002.

FBI aliyoitoa mwaka 2001 na albamu yake ya mwisho wa Sokouss ni Agenda ambayo aliitoa mwaka 2002.

Kimsingi Yondo Sister ni kama alifuata nyayo za Mbilia Bel na Tshala Muana ambao na wenyewe walianza kama wanenguaji na baadae wakaja kuwa waimbaji wazuri.

Mwanamuziki huyo ambaye likuwa na uwezo wa kulisakama jukwaa kwa sasa anaishi kwenye jiji la Paris, nchini Ufaransa na ameamua kabisa kuachana na muziki wa dunia na kujikita madhabahuni, ambapo sasa anahudumu kama mtumishi wa Mungu.

Katika mahojiano yake ya hivi karibuni na moja ya chombo cha Habari cha Ufaransa, Yondo alisema anaamini upande aliopo sasa ni sahihi kwake kwani haoni kama kuna sababu ya kuendelea na muziki wa dunia.

“Nahitaji kuiona rehema ya Mungu katika maisha yangu, huko nilikokuwa nimeshamalizana nako, sasa nimemrejea Mungu na sitarajii kubadilika tena, huku niliko ni salama zaidi,”alisema.

Post a Comment

0 Comments