Ticker

7/recent/ticker-posts

WWF KUVIPANGA VIJIJI VITANO MKINGA MKOANI TANGA

 

Wanakijiji wa kijiji cha Mbuta wakiwa kwenye kikao cha kijiji cha kupitisha mpango wa matumizi bora ya ardhi.

NA JIMMY KIANGO-AFRINEWS MKINGA

SHIRIKA la Kimataifa la WWF kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, linaendelea na zoezi la kuvipanga vijiji vitano vilivyopo wilani humo.

Vijiji hivyo ni Mbuta, Bima, Mazola Kilifi, Mwanyumba na Mwakikonge vimeingizwa kwenye Mradi wa Uongoaji wa Misitu ya Usambara Mashariki pamoja na Uandaaji wa mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi unaofadhiliwa na WWF.

Mwanyumba kipo kata ya Bwiti, kijiji cha Mazola kipo kata ya Doda, kijiji cha Bima kipo Kata ya Gombero, kijiji cha Mwakikonge kipo kata ya Duga pamoja na kijiji cha Mbuta kilichopo kata ya Mwakijembe.


Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Zaituni Mkubwa akiwapitisha wanakijiji wa kijiji cha Mbuta kwenye kukubali sheria ndogondogo.

Mradi huo umelenga kuviweka vijiji hivyo kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao pamoja na mambo mengine unasaidia kuondoa migogoro ya ardhi pamoja na kulinda vyanzo vya maji na hifadhi.

Tayari Kijiji cha Mbuta kilichopo Kata ya Mwakijembe, kimeshapitiwa na mradi huo na wanakijiji wameuridhia na kuupitisha sanjari na sheria ndogo ndogo za kuilinda hatua hiyo ambayo inagharimu zaidi ya milioni 10 kuikamilisha kwa Kijiji kimoja.

Shirika la WWF kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga ndio wawezeshaji wakuu wa mradi huo na malengo yao ni kuhakikisha ardhi ya vijiji hivyo inawanufaisha wananchi na kuwaondolea migogoro.

Viongozi wa kijiji cha Mbuta wakiwa kwenye kikao cha kijiji cha kupitisha mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Matunda ya mradi huo yameonekana katika Kijiji cha Mbuta, tayari mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Mbuta na Perani umekwisha hatua inayowafanya watu waishi kwa amani na upendo kama ilivyokuwa awali kabla Kijiji cha Mbuta hakijagawanywa.

Pia mpango huo umekisaidia Kijiji cha Mbuta kupata sheria ndogo ndogo ambazo zitakuwa ndio mwongozo wao katika kuilinda kazi hiyo.

Mwanasheria wa Halmashauri ya Mkinga, Zaituni Bwana yeye ndie aliyewaongoza wanakijiji wa Mbuta kuridhia sheria hizo ambazo pamoja na mambo mengine zinakwenda pamoja na adhabu zake.

Thomas Sawe, afisa wa WWF, amewaomba wanakijiji wanaofikiwa na mradi huo ni vema wakawa mstari wa mbele kufuata sheria na taratibu wanazozikubali.

Diwani wa Kata ya Mwakijembe, Letinga Matagi akiongea na wanakijiji wa kijiji cha Mbuta.

“Ni gharama sana kuendesha hii miradi, fikiria katika Kijiji kimoja kinatumika kiasi cha zaidi ya milioni 15, kwa hali ya kawaida wananchi wenyewe hawawezi, sasa linapojitokeza shirika la kusaidia ni vema wakalinda miradi hiyo ili kuepusha migogoro na uharibifu wa mazingira.”

Sawe anasema kinachofanywa na WWF na Halmashauri ni kupanga maeneo ya kilimo, malisho, hifadhi, huduma za jamii na kulinda mito na vyanzo vya maji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Zahara Msangi ameipongeza WWF kwa kuufadhili mradi huo, ambapo pamoja na mambo mengine ameahidi kuhakikisha unalindwa.

Post a Comment

0 Comments