Ticker

7/recent/ticker-posts

MWENZA WA RAIS MSTAAFU KULIPWA KIINUA MGONGO

Bunge limepitisha muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali Namba 4 wa mwaka 2023 ambapo moja ya marekebisho katika sheria ya Mafao ya Kustaafu katika Utumishi wa kisiasa inapendekezwa wenza wa Rais Mstaafu, Makamu wa Rais Mstaafu na Waziri Mkuu Mstaafu kulipwa kiinua mgongo kwa kipindi cha uongozi wa wenza wao.

Muswada huo uliopitishwa utawasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ili aweze kuusaini na kufanya muswada huo kuwa Sheria.

Akiwasilisha marekebisho hayo leo Oktoba 31 wakati wa kikao cha Bunge Mjini Dodoma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dk. Eliezer Feleshi amesema kuwa vifungu vipya vya 9A, 12A na 14A vinapendekezwa kuongezwa katika Sheria ya Mafao ya Kustaafu katika Utumishi wa Kisiasa, Sura ya 225.

Sambamba na marekebisho hayo, vifungu vya 11, 13 na 15 vinapendekezwa kurekebishwa ili kuweka utaratibu wa malipo ya fadhila kwa wenza wa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu endapo watafariki wakiwa madarakani au baada ya kumaliza muda wao na kufariki kabla ya kulipwa mafao au stahiki zao.

Kifungu cha 18 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuweka utaratibu wa wenza wa Spika Mstaafu aliyefariki kupokea mafao ya pensheni ya kila mwezi.



Post a Comment

0 Comments