Ticker

7/recent/ticker-posts

BUNGE LARIDHIA TANZANIA KUJIUNGA NA TAASISI YA DAWA AFRIKA

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeridhia Tanzania kujiunga na Mkataba wa Kuanzisha Taasisi ya Dawa ya Afrika (AMA).

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuridhiwa kwa Mkataba huo kutaisaidia Tanzania kupambana na bidhaa tiba duni na bandia pamoja na kukuza soko la bidhaa tiba zinazozalishwa nchini.

Amefafanua kuwa kuridhiwa kwa Mkataba huo kutaiwezesha Tanzania pamoja na nchi nyingine za Afrika kufungamanisha na kuimarisha mifumo na uwezo wa nchi katika kudhibiti dawa, vifaa tiba, vitenganishi na bidhaa nyingine za afya.


Waziri Ummy ameongeza kuwa kwa Tanzania kuridhia kujiunga na Mkataba huo wa AMA kutawezesha kuvutia wawekezaji pamoja na wafanyabiashara nchini kwa kuwa nchi wanachama watakuwa na soko kubwa zaidi ya sasa na muwekezaji ataweza kuuza katika nchi nyingine za afrika bila ya kulazimika kusajili bidhaa zao katika nchi nyingine za afrika mwanachama wa mkataba huo.

Katika kutekeleza jitihada za pamoja za nchi za Afrika katika kupambana na bidhaa tiba duni na bandia kuwepo katika soko, Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Afrika (AU) katika Mkutano wa kawaida wa 32 uliofanyika Ethiopia mwaka 2019 walikubaliana kuanzishwa kwa Taasisi ya Dawa ya Afrika (AMA) ikiwa na lengo la kuratibu na kusaidia nchi Wananchama wa umoja Afrika katika kuboresha uwezo wa kudhibiti ubora wa bidhaa tiba hususani katika maeneo ambayo ni changamoto kwa nchi nyingi Barani Afrika.

Kwa mwaka huu tayari jumla ya nchi 30 zimesaini na kati ya hizo nchi 23 zimeridhia Mkataba huo zikiwemo Rwanda na Uganda. Tanzania ilisaini mkataba huo Agosti, 2021 na kwa hatua ya leo ya Bunge kuridhia Mkataba huo, ni rasmi sasa Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi wanachama wa Mtaba huo.


Post a Comment

0 Comments