Ticker

7/recent/ticker-posts

USAID KUTUMIA DOLA MILIONI 25 KUIMARISHA MAZINGIRA YA BAHARI TANZANIA

Mkurugenzi Mkazi wa USAID Tanzania, Craig Hart 


Na. MWANDISHI WETU-Afrinews ZANZIBAR

Serikali ya Marekani kupitia Shirika la misaada la Kimataifa la Marekani (USAID) limewekeza kiasi cha Dola za Marekani milioni 25, kwenye mradi wa Heshimu Bahari.


Mradi huo umelenga kuimarisha mazingira ya bahari na viumbe vyake katika maeneo ya hifadhi, lengo likiwa ni kukuza hifadhi ya bahari na kuongeza uzalishaji katika rasilimali za baharini na mazalia ya samaki.
Maeneo yaliyolengwa kwenye mradi huo ni mikoa ya Tanga, Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es salaam pamoja na  mikoa yote ya Unguja na Pemba iliyopo visiwani Zanzibar.


Tayari USAID imeanza kazi hiyo kwa kutembelea baadhi ya maeneo visiwani Zanzibar, ambapo shirika hilo limewahakikishia Wavuvi na Wakulima wa zao la Mwani kuwa linaiunga mkono serikali ya muungano pamoja nay a Zanzibar.


Juzi Mkurugenzi Mkazi wa USAID nchini Tanzania, Craig Hart, aliwaambia Wavuvi, wakulima wa Mwani na Kamati za Uvuvi na wanajamii wa Kiijji cha Chwaka Mkoa wa Kusini Unguja kuwa wanaunga mkono shughuli zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kuwaletea maendeleo wananchi.


Amesema anapenda kuonana na jamii iliyopo katika maeneo ambayo USAID inafanya kazi nao kwa karibu kupitia mradi wa Heshimu Bahari katika kusaidia sekta ya Afya, Elimu na shughuli zingine za kiuchumi na kijamii.

Craig Hart amesema amejifunza mambo mengi katika ziara yake hiyo ikiwemo changamoto za bahari hasa uvuvi haramu na kuweka wazi kuwa changamoto hiyo inaikabili dunia.


“Hili si tatizo la Tanzania pekee, ni suala linalozikabili nchi nyingi duniani, muhimu kwetu ni kuidhibiti ili dunia iwe salama na kujihakikishia uvuvi endelevu wenye faida.”

Mwakilishi huyo wa USAID nchini pia amevutiwa na mandhari ya Zanzibar ambayo yamezungukwa na bahari na kuweka wazi kuwa ili yaendelee kuwa bora ni lazima yalindwe ili wananchi kuendelea kufaidika na rasilimali zilizomo baharini ikiwemo Uvuvi na ukulima wa Mwani.

“Mimi napenda  Samaki na mke wangu anapenda  mwani,  kama hatutoilinda Bahari, samaki watakosekana na Mwani utapotea, tukumbuke Mwani ni muhimu  na unafaida nyingi mwilini,”alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mradi wa USAID Tanzania, Heshimu Bahari, Sadiki Laiser alisema mradi huo umejikita katika kuimarisha sera zitakazosaidia serikali, sekta binafsi na jamii, kwenye kuhifadhi na kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.

Alisema mradi huo ni wa muda wa miaka mitano ambapo sasa unaelekea katika utekelezaji wake kwa awamu ya pili ili kuboresha ustawi wa kiikolojia na uzalishaji wa maeneo ya viumbe hai wa baharini nchini Tanzania.

Mratibu huyo, alieleza kuwa mradi huo pia unalenga kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi wakiwemo wakulima wa mwani, wafugaji wa majongoo bahari na wavuvi ili kuheshimu kuheshimu bahari na rasiliamli hiyo kuwa endelevu.

Wakizungumza katika mkutano huo, wakulima wa mwani wa kijiji hicho, walisema wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa nyenzo zitakazowawezesha kufika katika mashamba yao ya mwani ambapo sasa wanalima katika kina kirefu cha maji ya bahari.

“Hatuna usafiri wa uhakika wa kutufikisha katika mashamba yetu bahari, tunaomba msaada kwa wavuvi watupakie katika boti zao za uvuvi na kutupelekea katika mashamba yetu, ingawa wapo  baadhi yao wanakubali kutuchukua  kwa kulipia au kutupa msaada, lakini si uhakika,”alisema Khadija Juma Ame.

Mkulima huyo wa mwani alisema wanahitaji nyenzo za kisasa kwa ajili ya kuendeleza kilimo hicho ambacho sasa kinakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa yaliyotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo alisema bado bei ya mwani ni ndogo ambapo kwa kilo moja kwa sasa ni shilingi 1000 hivyo wanahitaji kuongezewa bei kwa sababu kilimo cha mwani ni kigumu na wakulima  wengi wa zao hilo ni wanawake.

Khadija aliliomba shirika na USAID kusadia masoko ya nje ya zao hilo la mwani ili kuongeza thamani kwani zao hilo ni mkombozi mkubwa wa wananchi hasa wanawake.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments