COUP D’ETAT ILIVYOIWAHI SELF-COUP GABON
TUPO Gabon. Rais Ali Bongo amepinduliwa jana (Agosti 30, 2023). Wapo wanaotafsiri kuwa mwisho wa zama za familia moja kuongoza nchi kwa miaka 56. Binafsi naiona hatima dhalili ya superstar wa muziki.
Dunia inamfahamu kama Ali Bongo Ondimba. Alipozaliwa, alipewa jina “Alain Bernado”. Gabon alijulikana kwa majina ya “Ali B" na “ABO", yote ni kifupisho cha “Alain Bongo" na “Ali Bongo". Sababu ni uhusika wake katika popular culture.
Mwaka 1977, Ali aliishika Gabon alipotoa albamu “A Brand New Man". Ikiwa na nyimbo “I Wanna Stay With You", “Gonna Fly Now" na nyingine. Role model wake alikuwa gwiji wa Funk, James Brown.
Ali ni mtoto wa Rais wa Pili wa Gabon, Omar Bongo Ondimba, ambaye kabla aliitwa Albert Bernard Bongo. Mwaka 1973, alibadili dini kuwa Muislam. Jina pia alibadili, akaitwa Omar.
Msimamo wa kidini wa Omar, ulimlazimisha Ali aache muziki mwaka 1980. Si hivyo tu, naye alibadili dini. Akaachana na jina la Alain, akaitwa Ali.
Mama mzazi wa Ali, Patience Dabany, ni mwanamuziki veterani Afrika. Patience alikuwa First Lady wa Gabon kati ya mwaka 1967 na 1987, alipotalikiana na Omar.
Haikuwa ajabu, mwaka 2009, Ali alipogombea urais kwa mara ya kwanza, kufuatia kifo cha Omar, alikuwa akirap jukwaani kwa umahiri kwenye mdundo wa Hip Hop, akiomba kura. Ali ni kipaji kikubwa cha muziki, kilichozuiwa na dini, siasa zikamteka.
Ilipata kuvumishwa kuwa Ali hakuwa biological son wa Omar, bali alimu-adopt. Omar alikuwa mbogo. Alisisitiza kuwa ni mwanaye wa damu, kisha akamuandaa kisiasa kuwa mrithi wake.
Ali, alipokuwa na umri wa miaka 30, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje. Kisha akawa Waziri wa Ulinzi kwa miaka 10, kabla ya kuwa Rais. Omar aliiongoza Gabon miaka 42, kabla kifo hakijamtwaa. Ali miaka 14, kabla mapinduzi hayajamwondoa.
Mapinduzi ya uasi wa kijeshi (coup d'etat), ndio yamemwondoa Ali. Ni timing ya mbwa kula mbwa, kwani Ali naye alikuwa kwenye mchakato wa kukaa madarakani kwa nguvu (self-coup).
Kung'ang'ania madaraka ni mapinduzi. Kiongozi kuvunja Katiba au kunyamazisha mifumo ya nchi, ikiwemo kulifanya Bunge kukosa makali ni mapinduzi. Yanaitwa self-coup au coup from the top.
Gabon, nchi ya watu milioni 2.9. Wapigakura ni 800,000. Uchaguzi ulifanyika Jumamosi (Agosti 26, 2023), zilipita siku nne, matokeo hayakutangazwa. Mgombea wa upinzani, Albert Ossa, alijitangaza mshindi Agosti 28 (Jumatatu).
Jumatano (Agosti 30, 2023), Tume ya Uchaguzi Gabon (Cenap), ilimtangaza Ali kushinda urais kwa muhula wa tatu kwa kura asilimia 64, akimshinda Ossa kwa mkupuo mmoja, aliyepata kura asilimia 30.
Hazikufika saa mbili baada ya tangazo la Cenap kuhusu ushindi wa Ali, wanajeshi waliovaa sare za Jeshi la Gabon, walivamia Televisheni ya Taifa na kutangaza mamlaka ya nchi kuwa chini ya jeshi.
Mwanajeshi aliyetoa tangazo hilo, alisema Ali amewekwa kizuizini nyumbani kwake, kisha akamtangaza Kiongozi wa Mpito wa Gabon kuwa ni Jenerali Brice Nguema.
Mbwa anakula mbwa. Jenerali Nguema, kwa muda mrefu amekuwa mtuhumiwa wa ufisadi wa mali za Gabon na kiungo wa mtandao wa kuuza dawa za kulevya Afrika Magharibi na Latini America.
Aprili 2020, Nguema, aliteuliwa kuwa Amiri Mkuu wa Jeshi la Ulinzi wa Umma Gabon. Ripoti ya mwaka 2020 ya Mtandao wa Kimataifa wa Waandishi wa Habari kuhusu Uhalifu wa Kupangwa na Rushwa (OCCRP), ilionesha kuwa Nguema anamiliki utajiri mkubwa Ulaya na Marekani.
Nguema pia alikuwa mtiifu hasa kwa Ali. Tuhuma nyingine kwa Nguema ni kuwa ndiye amekuwa mlinzi na mtetezi wa biashara na uwekezaji wa Ali nje ya nchi. Nguema pia alirekodi wimbo ambao aliimba “Nitamlinda rais wangu kwa heshima na utiifu.”
Zaidi, Nguema amekuwa mtu wa karibu na familia ya Bongo tangu zamani. Wakati Omar (Baba Ali) akiwa Rais, Nguema alikuwa mlinzi wa Rais (Aide De Camp ‘ADC'). Ukiona mzunguko, unaweza tu kusema, Nguema alikuwa bodyguard wa Omar.
Hali ikiwa hivyo, mtoto wa Ali, Noureddin pamoja na maofisa wa ngazi za juu wa Serikali ya Ali, wamekamatwa kwa tuhuma za uhaini na ufisadim
Ali hakupaswa kufika huku; mwaka 2018, aliumwa sana. Alipatwa na kiharusi. Alipotea kwenye uso wa jamii kwa zaidi ya miezi 10. Hata baada ya kupona, afya yake haijarejea kuwa kama zamani.
Kuongea kwake ni kwa tabu. Kutembea shida, mikono pia haina nguvu. Video iliyomwonesha akiomba dunia “ipaze sauti" dhidi ya matendo anayotendewa yeye, mwanaye na mkewe, Sylvia, inadhihirisha Ali bado si timamu.
Angeweza kupumzika, miaka 14 madarakani si michache. Hakupaswa kuwa mshamba wa madaraka. Amekulia katika familia namba moja, amepata kila kitu tangu akiwa mtoto. Masomo Ulaya (Ufaransa zaidi) na Marekani. Lugha zake ni Kifaransa na Kiingereza tu, hajui lugha yoyote ya asili ya Gabon.
KUNANI FRANCAFRIQUE?
Machi 2022, gazeti la New York Times, liliandika kuwa nguvu ya Ufaransa inaundwa na nguzo tatu; Mosi, ushawishi wake kwa makoloni yake ya zamani Afrika (nchi za Francafrique), pili, umiliki wa silaha za nyuklia, tatu, kiti chake Umoja wa Taifa (Veto).
Katika miaka mitatu iliyopita, nchi sita za Francafrique zimekumbana na mapinduzi; Mali (Agosti 2020), Chad (Apirili 2021), Guinea (Septemba 2021), Burkina Faso (Januari 2022), Niger (Julai 2023) na sasa ni Gabon.
Kipigo kikubwa kwa Ufaransa ni kuwa sehemu kubwa ya nchi zilizofanya mapinduzi, wanamapinduzi hawataki ushirikiano nayo. Hivyo, kama tathmini ya New York Times ni sahihi, nguzo moja ya Ufaransa imebaki dhaifu. Nchi za Francafrique zinakaribisha zama mpya.
Urusi ya Vladimir Putin, ipo macho muda wote, tena kwa vitendo, kuingiza ushawishi wake Francafrique. Ni pigo kubwa kwa Emmanuel Macron na Ufaransa yake.
Ndimi Luqman MALOTO
0 Comments