Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb), ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kufikisha asilimia 95 ya ujenzi wa jengo la ofisi ya wizara unaoendelea katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ikiwa ni hatua ya juu zaidi kufikiaa kuliko wizara nyingine.
Akitoa pongezi hizo leo mjini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa amezitaka wizara nyingine kuiga mfano wa wizara hiyo ili kukamilisha ujenzi kwa muda ulipangwa.
“Hongera sana Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri , hongera mkandarasi kwa kufikia hatua hii na usimamizi mzuri.Tunaamini wizara nyingine watakimbia mbio kama nyinyi ambavyo mmefanya.”
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii limefikia asilimia 95 ambapo gharama yake ilipangwa kuwa shilingi bilioni 17 na hadi sasa Wizara imeshamlipa mkandarasi shilingi bilioni 13.6.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kamishna Benedict Wakulyamba amesema zimebaki kazi chache sana kwenye ujenzi huo ikiwa ni pamoja na kukamilisha baadhi ya mifumo ya umeme na mifumo ya mawasiliano na kupaka rangi baadhi ya maeneo.Ameongeza kuwa Wizara inatarajia mkandarasi akamilishe kazi ya ujenzi huo hadi kufika Agosti 10,2023 na kulikabidhi jengo.
0 Comments