Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimelimaliza sakata la uwekezaji Bandarini kwa kusema kuwa kamwe hawatarudi nyuma.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Daniel Chongolo alipowaambia maelfu ya wananchi wa Kanda ya Kaskazini jana.
Amesema uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam hawatarudi nyuma kwa kuwa lina tija kwa Watanzania.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliohusisha wananchi wa Mkoa wa Arusha, Manyara na Kilimanjaro, katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid,Chongolo amewaomba wananchi waiamini Serikali ya Chama Cha Mapinduzi(CCM).
"Sisi Chama Cha Mapinduzi tutakuwa wa mwisho kutetea jambo ambalo halijakaa sawa kwasababu tunajua ikifika wakati wa kuomba kura sisi ndio tutakuja kwa wananchi, kwanini kujitetea kama tunajua jambo haliko sawa.
"Tunasema haya tukiwa na nguvu tukiwa kifua mbele kwamba jambo hili linatija kwa nchi, lina tija kwa maendeleo ya nchi na tuliahidi wenyewe na kwa hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama na sisi ni sehemu ya Watanzania na ni Watanzania
"Tuna haki ya kusimamia mambo mazuri yatokeee na hili haturudi nyuma , nisisitize watalaam na wajuzi wa sheria ambao wana maoni na ushauri wa namna ya kurekebisha baadhi ya vipengele vikaleta tija zaidi ya ilivyosasa...
"Waje mezani wajadili washauri ili tuboreshe zaidi tutoke tukiwa na kitu ambacho kinaenda kuongeza tija kwa nchi yetu lakini sio vinginevyo,sio kutunga uongo, sio kuchonganisha wananchi na serikali yao ,hatuko tayari, hatutavumilia na hatuko tayari kukaaa kimya kuacha hayo yakitokea."
Akieleza zaidi mbele ya maelfu ya wananchi hao Chongolo amesema uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam lengo kwa ujumla wake linalenga kuongeza tija , kwani kwa sasa kiwango kinachokusanywa kwa asilimia 99 kinatumika pale pale kwenye uendeshaji.
"Maana yake sisi kama nchi hatunufaiki , kuongeza kwenye mfuko wa Serikali kutatua changamoto za wananchi kupitia uzalishaji au mapato yanayotokana na bandari, " amesema Chongolo alipokuwa akizungumzia faida za uwekezaji utakaofanyika bandari ya Dar es Salaam.
0 Comments