Ticker

7/recent/ticker-posts

BALOZI KARUME AWEKWA MTEGONI NDANI YA CCM

Mwenendo na tabia ya kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Ally Karume ya kumsema na kumkosoa hadharani Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi imemuingiza kwenye mtego wa kusalia au kuondolewa ndani ya chama hicho.

Tayari Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Kusini Unguja, imeshapendekeza mwanachama huyo avuliwe uanachama wake.

Hata hivyo pendekezo hili litahalalishwa ama kubatilishwa na vikao vya juu vya chama hicho vitakavyoongozwa na  Mwenyekiti wa chama hicho Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Vikao hivyo vinavyohusisha vigogo wa CCM  vinaanza leo Julai 8, 2023 jijini Dodoma.

Kikao cha leo kilitanguliwa na kikao cha Kamati Maalum ya CCM Zanzibar, kilichoketi jana Julai 7, 2023 chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Balozi Karume amefika hapo alipofika ndani ya chama baada ya Juni 18, 2023 kutoa matamshi tata kwa kudai kuwa alijaribu kuitumia kadi ya CCM kwenye ATM, lakini haikufanya kazi hivyo kwake American Express na Viza ni muhimu kuliko kadi ya chama hicho.


Kwa mujibu wa taarifa iliyosambaa leo Julai 8, 2023 asubuhi ilieleza kuwa kikao cha kupendekeza kumfuta uanachama Balozi Karume kimefanyika saa saba usiku chini ya Katibu wa Mkoa wa CCM, Amina Mnacho.

Taarifa ya kumfuta uanachama ilitolewa na Katibu Mwenezi wa Mkoa huo, Ali Timamu Haji.

Hatua hiyo inakuja baada ya chama hicho kumpa onyo kutokana na kauli zake akidaiwa kukidhalilisha chama na kuwatukana viongozi wakuu hadharani.

Juni mwaka huu,Balozi Ali Abeid Karume alihojiwa na Kamati ya Maadili ya chama hicho huku akiweka wazi kwamba yupo tayari kupokea uamuzi wowote dhidi yake.

Hatua ya kuitwa kwenye vikao vya maadili ya chama imekuja baada ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar kuwaonya baadhi ya wanachama wao kuvunja maadili na utamaduni wa chama hicho kwa kuzusha mambo ambayo yanahatarisha uhai wa CCM na kuwapo kwa mgawanyiko.

Hivi karibuni Balozi Karume alinukuliwa na baadhi ya mitandao ya kijamii akisema CCM kipo madarakani si kwa sababu kilishinda uchaguzi, bali kwa sababu ya uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Kada huyo pamoja na hali hilo pia alikosoa uamuzi wa Rais  wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi wa kukodisha visiwa vilivyopo Zanzibar kwa wawekezaji.

Kutokana na hali hiyo  Rais Dkt. Mwinyi aliagiza wanachama wote wanaotoa kauli za kuwagawa na kukiyumbisha chama wasiachwe hadi nyakati za uchaguzi, bali wachukuliwe hatua mapema.

Kauli hizo ziliisukuma Kamati ya Maadili  ya chama ya  Tawi la Mwera, lililopo ndani ya Jimbo  la Tunguu mkoa wa Kusini Unguja kumuhoji Balozi Karume, Juni 15, 2023.


Pia alihojiwa Juni 16, 2023 na Kamati ya Maadili Wilaya ya Kati, mkoani humo.

Balozi Karume amesema kikao hicho kilidumu kwa saa moja, akidai nusu saa ilikuwa ya mazungumzo maalumu na nusu saa nyingine ilikuwa ya kutaniana na kuwapa hadithi.

Alipoulizwa atahamia chama gani iwapo atafukuzwa CCM, alijibu kuwa hajajiandaa kufukuzwa uanachama na ikitokea hawezi kuhamia chama kingine chochote cha siasa, kwa sababu moyo na mapenzi yake bado yapo ndani ya CCM.

Amesema katika vikao vyote alivyoitwa mazungumzo yalikuwa mazuri na zaidi yalilenga kuhoji masuala ya uchaguzi ndani ya CCM.

Kuhusu taarifa zilizosambaa mtandaoni zikionyesha amesema kadi yake ya American Express na Viza ni muhimu kuliko kadi ya CCM,  alisema, “Ndiyo nimesema kwa sababu kadi ya CCM mara ya mwisho nilijaribu kuitumia kwenye ATM lakini haikufanya kazi.”

Hata hivyo alisisitiza kuwa kwa Zanzibar kama unafanyika uchaguzi wa haki na wazi mgombea wa CCM hawezi kushinda kwa sababu wagombea huletwa kutoka CCM Taifa na hawafuati ushauri au kuzingatia matakwa ya wanachama wake, hili nililisema na ninaweza kulirejea tena.”

“Pia mtu akiulizia mchakato wa uchaguzi haina maana kwamba anapinga mgombea wa CCM kushindwa, nia yangu ni kujenga tujipange vizuri ili tushinde katika uchaguzi mkuu ujao,” amesema Balozi Karume

Balozi Karume atawajibishwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM ambayo inaelekeza kuwa Halmashauri Kuu ya CCM ndiyo chombo cha mwisho cha maamuzi dhidi ya hatua yoyote ya chama au mwana chama.

Hivyo basi ikiwa maamuzi hayo yatafikishwa mbele ya vikao hivyo vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ni wazi vikao hivyo ndio vitahitimisha sakata hilo. 

Taarifa iliyotolewa na CCM juzi inaeleza kwamba vikao vya Kamati Kuu ya chama hicho (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) chini ya Mwenyekiwa wake Rais Dk. Samia Suluhu Hassan vitaanza kuketi kesho Julai 9, 2013 Jijini Dodoma.

“Vikao hivyo vya kawaida vya uongozi wa chama ngazi ya Taifa, vitafanyika kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya Mwaka 1977, Toleo la 2023 na vikitanguliwa na kikoa cha Sekreterietyi ya Halmashauri Kuu ya CCM itakayoketi Julai 8 (leo) 2023,” ilieleza taarifa ya CCM iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi Sophia Mjema.

Post a Comment

0 Comments