Mfanyakazi wa Benki ya NMB, Idara ya Mikopo Tawi la Clock Tower jijini Arusha ,George Kifaruka (43) mkazi wa Kijenge Suye, Kata ya Kimandolu Arusha amepandishwa mahakamani na kusomewa shitaka la kumlawiti mwanafunzi wa miaka 17 wa shule ya sekondari Olasiti ya jijini hapa.
Akisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa serikali, Grace Medikenya mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Heriet Marando, amedai kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Julai 8 hadi 10, 2023 nyumbani kwake Kijenge Suye.
Medikenya alidai mwathirika wa tukio hilo ambaye kwa sasa anahifadhiwa jina ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Olasiti, kidato cha pili na alikuwa akiishi na mtuhumiwa Kifaruka kwa malengo ya kusomeshwa, lakini lazima atoe fadhila ya kulawitiwa kila mtuhumiwa anapohitaji huduma hiyo.
Mtuhumiwa alikana shitaka hilo na mwendesha mashitaka alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na aliiomba mahakama kumsomea maelezo ya awali mtuhumiwa huyo.
Katika maelezo ya awali yaliyosomwa na Medikenya, ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alikuwa akiishi na mvulana huyo na alichukuliwa kwa lengo la kufadhiliwa kwa kusomeshwa sekondari kwa ajira ya kulawitiwa na mtuhumiwa.
Mwendesha mashitaka aliendelea kudai kuwa kabla ya kulawitiwa, alikuwa akioneshwa picha za video za ngono katika simu ya kiganjani ya mtuhumiwa na baada ya hapo ndipo tukio lilikuwa likifanyika mara kwa mara.
Medikenya alidai katika maelezo yake kuwa mvulana huyo alipofika shuleni Olasiti, alipokuwa akipewa adhabu alimwambia mwalimu kuwa anaishi katika mazingira magumu, kwani mfadhili wake humlawiti na ndio maana anashindwa kuwahi shule.
Alidai baada ya kauli hiyo Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, aliamua kumchunguza na kumpeleka polisi na baada ya polisi alipelekwa hospital kwa uchunguzi wa daktari ambao ulibainisha kuwa kijana aliharibiwa kwa kitendo hicho.
0 Comments