Serikali imeridhia kusitisha kwa sasa kuufunga uwanja wa Mkapa ili kufanya ukarabati mkubwa na badala yake imeipa nafasi timu ya Yanga iendelee kuutumia uwanja huo kwa ajili ya mchezo wao wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.
Yanga imetinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya CAF na inatarajia kumenyana na Marumo Gallants ya Afrika Kusini Mei 10, mwaka huu.
Akizungumzia suala Hilo Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Said Yakub alisema wameiona haja ya kufanya hivyo kwa kuwa nafasi ya kufanya hivyo bado ipo.
Yakub alisema marekebisho hayo makubwa ni muhimu, lakini pia ni muhimu zaidi kwa Yanga, timu ya Taifa na timu majirani kuutumia uwanja huo.
"Hata Yanga ikitinga fainali kama itatakiwa kuutumia uwanja wa Mkapa, tutaruhusu, lakini pia timu ya taifa inamchezo muhimu hapa nyumbani, yote haya yanatufanya turuhusu uwanja uendelee kuutumia."
MCHEZO WA NUSU FAINALI KOMBE LA AZAM WASOGEZWA MBELE
Pamoja na Yanga kupewa nafasi ya kuutumia uwanja wa Mkapa, pia imepewa nafasi ya kujiandaa zaidi kwa ajili ya mchezo huo.
Shirikisho la Soka nchini TFF limetangaza kuisogeza mbele mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam uliokuwa uchezwe Mei 7, mwaka huu kwenye uwanja wa Liti dhidi ya Singida Big Stars.
0 Comments