Ticker

7/recent/ticker-posts

HISTORIA YAANDIKWA TANZANIA,IKULU MPYA YAZINDILIWA

Wakati Tanzania  ikielekea kutimiza miaka 62 ya uhuru wake iliyoupata Desemba 9,1961,hatimae sasa imeweza kumiliki Ikulu yake iliyojengwa na watanzania wenyewe.

Leo Mei 20,2023, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameizindua rasmi Ikulu hiyo iliyopo Chamwino jijini Dodoma.

Ikulu hiyo imebeba majengo mbalimbali likiwemo jengo la ofisi ya Rais na makazi yake.

Hafla hiyo kubwa ilihudhuriwa pia na Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  Dkt. Hussein Ali Mwinyi,  Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Marais wastaafu,Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Dkt. Jakaya Mrisho Kikwte.

Akizungumzia uzinduzi huo Rais Dkt. Samia alisema: Ni tukio adimu na adhimu, kwa mara ya kwanza Watamzania tumeweza kujenga wenyewe Ikulu yetu kwa kutumia wataalamu wetu na rasilimali zetu.

 “Nilipokabidhiwa hatamu za kuongoza nchini niliahidi nitaendeleza miradi iliyopo, Ikulu ya Chamwino ni moja ya miradi niliyorithi, mradi wa kwanza niliorithi ambao tayari niliukamilisha ni ule wa daraja la Tanzanite, Dar es Salaam na Inshaallah Mwenyezi Mugu aniwezeshe niikamilishe miradi yote.”


Dkt. Samia alisema kukamilika kwa jengo hilo kuna toa fursa ya kuendelea na hatua inayofuata ambayo ni ujenzi wa jengo la kisasa “Samia Complex” ukumbi wa mikutano, nyumba za viongozi, Zanzibar lounge, East Africa lounge, uwanja wa golf, njia ya ndege, viwanja vya michezo na sehemu ya kihistoria, michoro iko tayari tunatafuta fedha za kutekeleza ujenzi huo.”

Rais Dkt. Samia alinikuu kauli ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee  Ali Hassan Mwinyi kuwa maisha ni hadithi na tujitahidi kuandika hadithi njema za maisha yetu.

Aidha alimsifu  Rais wa awamu Tano, hayati  Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuweka msukumo mkubwa wa ujenzi wa Ikulu hiyo.


Kwa upande wake Makamu wa Rais Dkt. Mpango alisema jengo hilo ni lulu ya nchi yetu ya Tanzania, ni jengo ambalo lina hadhi ya nchi ya kipato cha Kati ni taa ya kuipeleka nchi yetu kuwa na hadhi ya kipato cha juu ndani ya kipindi kifupi kijacho. "Nikuhakikishie Tanzania nzima inazizima kwa pongezi na shukurani kwako kwa kazi nzuri unayofanya.” Alisema.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Mwingi alimpongeza Rais Dkt. Samia kwa mafanikio hayo ya ujenzi wa majengo mapya ya Ikulu. "Katika Ikulu hii ya Chamwino, imetengwa Ofisi ya Rais wa Zanzibar nakushukuru sana Mhe, Rais.” Alisema Dkt. Mwinyi.

Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Kikwete alisema kwa niaba ya viongozi wastaafu wenzake wamefurahishwa na hatua hiyo kwani historia meandikwa.


“Umuhimu wake ni kuhitimisha dhamira ya baba wa Taifa ya  kuhamishia makao makuu ya nchi kutoka  Dar es Salam kuja hapa Dodoma mwaka 1973, leo mama yetu umekamilisha, kilele cha uamuzi ule."

Dkt. Kikwete alimmiminia sifa Rais Dkt. Samia kwa kuendeleza miradi yote iliyoachwa na mtangulizi wake kwa umahiri mkubwa.

“Umepokea miradi mikubwa na yenye gharama kubwa, ungeweza kusema ah.. mimi naanza na yangu lakini hukufanya hivyo, ulisema kila kilichoanzishwa na mtangulizi wangu nitakiendeleza na umefanya kazi kubwa na kazi yetu ni kukuombea Rais wetu afya njema umri mrefu ili ufanye makuwba zaidi.” 

Katibu Mkuu Kiongozi Dkt.Moses Kusiluku, 


alisema jiwe la msingi la ujenzi wa Ikulu hiyo liliwekwa Mei 30, 2020 na eneo lote la Ikulu lina ukubwa wa Ekari 8,473

“Ujenzi huu umetekelezwa na Watanzania kwa asilimia 100%. Na wajenzi walikuwa ni vijana wa  Suma JKT, huku Wakala wa Majengo (TBA) wakiwa wasimamizi wa ujenzi na Ofisi ya Rais, Ikulu ikifuatilia kwa karibu.”

Wananchi nao hawakuwa nyuma, baadhi yao walisema kukamilika kwa Ikulu ya Chamwino ni ishara tosha ya kwamba Serikali imehamia Dodoma na uchumi wa Mkoa huu utakuwa zaidi, tunamshukuru na kumpongeza sana Rais.

Post a Comment

0 Comments