Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan hii leo amezindua rasmi Ikulu ya Chamwino iliyopo makao makuu ya nchi yeu Dodoma.
Viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa kitaifa waliopo sasa madarakani na wastaafu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wamehudhuria sherehe hiyo ya uzinduzi huo.
Miongoni mwa shughuli zilizoambatana na uzinduzi huo ni pamoja na rais Samia kukagua gwaride maalumu pamoja na kupanda mti wa kumbukumbu.
Baadae Rais Samia pamoja na viongozi wengine walishuhudia upandishwaji wa bendera katika jengo hilo jipya ambalo taswira yake ni sawia na ile ya Ikulu ya Dar es Salaam.
Jengo hilo ambalo ujenzi wake ulianza mwezi Februari, mwaka 2022, lina ukubwa wa mita za mraba 9,340.
Eneo la Ikulu ya Chamwino linaweza kuwa miongoni mwa Ikulu kubwa barani Afrika, huku likiwa na ekari 3,730. Mbali na hayo, pia wanyama kadhaa wa porini kama vile twiga, fisi na wengine wanapatikana humo.
Dodoma ilitangazwa rasmi kuwa makao makuu ya Tanzania mwaka 1973. Hata hivyo, aliyekuwa rais wa awamu ya tano John Pombe Magufuli ndie rais wa kwanza aliyeonekana kusimamia kwa dhati azma hiyo kwa kuishurutisha serikali yake kuhamia Dodoma.
Ujenzi wa Ikulu ya Chamwino ni mojawapo ya miradi mbalimbali iliyoachwa na hayati Magufuli, hivyo kukamilika kwake, bila shaka kunampa faraja Rais Samia na ari ya kukamilisha miradi mengine.
0 Comments