Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuchukua hatua stahiki kwa kushirikiana na nchi jirani, Jumuiya za Kikanda, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha watanzania na raia wengine waliopo nchini Sudan wanakuwa salama wakati huu ambapo nchi hiyo ipo katika changamoto za kiusalama.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax Bungeni jijini Dodoma, leo wakati akitoa Taarifa ya Serikali kuhusu Hali ya Amani na Usalama nchini Sudan.
Amesema tangu kuibuka kwa mapigano mjini Khartoum Aprili 15, 2023 kati ya vikosi vya Serikali (Sudan Armed Forces - SAF) na Vikosi vya Msaada yaani Rapid Support Forces (RSF) na kusambaa katika maeneo mengine ya nchi hiyo, tayari athari mbalimbali zimeanza kujitokeza ikwemo vifo vya watu 185 majeruhi zaidi ya 1,000 na uharibifu wa mali.
Amesema mapigano hayo pia yamechangia kurudisha nyuma jitihada zinazoendelea za kutafuta amani Sudan na kwamba Serikali ya Tanzania inasikitishwa na kuzorota kwa hali ya amani na usalama inayoendelea nchini humo.
Ameongeza kuwa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine inao raia wake wapatao 210 nchini Sudan wakiwemo wanafunzi 171, wanadiplomasia na raia wengine ambao hadi sasa wapo salama na hakuna aliyeathiriwa na mapigano hayo.
Dkt. Tax amesema kuwa, jitihada za pamoja za Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na nchi na taasisi mbalimbali zimefanikisha kusitishwa kwa mapigano nchini Sudan kwa muda wa saa 24 kuanzia Aprili 18, 2023 jioni ili kutoa nafasi kwa misaada ya kibinadamu kutolewa kwa raia.
Pia Dkt. Tax amempongeza Balozi wa Tanzania nchini Sudan, Silima Haji Kombo kwa kuendelea kuhakikisha usalama wa watanzania waliopo Sudan na kwamba Serikali inaendelea kufuatilia hali nchini humo pamoja na kuandaa mpango wa kuwaondoa raia wa Tanzania kadri itakavyohitajika.
Amesema Tanzania ambayo ni mjumbe wa Baraza la Amani la Afrika inaendelea kuunga mkono tamko lililotolewa na Baraza hilo katika mkutano wake uliofanyika Aprili 16,2023 la kulaani mapigano yanayoendelea na kutoa wito kwa pande zote mbili katika mgogoro huo kusitisha mapigano hayo.
Pia Tanzania inaendelea kuzitaka pande hizo mbili hasimu kutatua mgogoro huo kwa njia za amani na usalama huku zikihakikisha mahitaji ya kibinadamu, usalama na ustawi wa raia wa Sudan na raia kutoka nchi nyingine.
0 Comments