Nimrod Mkono wakati wa uhai wake
Ni zaidi ya miaka mitatu sasa kwa mbunge wa zamani wa jimbo la Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (80), kutoonekana mahali popote kwenye ardhi ya Tanzania, habari mbaya mwanasheria huyo amefariki dunia
Mkono mwanasheria nguli na mjuzi amefariki dunia leo asubuhi akiwa nchini Marekani.
Mwana CCM huyo aliingia bungeni mwaka 2000 aliwakilisha jimbo la Musoma Vijijini, hakuwa na mpinzani kutokana na Maendeleo aliyoyapeleka jimboni kwake.
Mafanikio yake yalimfanya kushinda tena ubunge mwaka 2015.
Bahati mbaya mara baada ya kushinda, hakukaa sana nchini, mwaka 2018 alikwenda Marekani kwa matibabu.
Taarifa mbaya ambazo zimeanza kusambaa mapema leo zikithibitishwa na mdogo wake Zadock Mkono ni kuwa mwanasheria huyo amefariki dunia.
"Nimepewa taarifa na shemeji yangu kuwa mzee amefariki, nimempigia shemeji ameshindwa kuongea vizuri.
"Mzee aliondoka nchini tangu mwaka 2018 akaelekea Marekani kwa matibabu kwa sababu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kusahausahau.
"Mimi nipo Tanzania kwa sasa ninachoweza kuthibitisha ni kwamba kweli amefariki taarifa zaidi za kama alikuwa hospitali au amefariki ghafla hizo bado sijajua, nitawapa taarifa zaidi baadae.”
Nimrod Elireheemah Mkono, alizaliwa Agosti 18, 1943 katika kijiji cha Busegwe, alikuwa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini mwaka 2000-2015.
Nimrod Mkono ni mwana maendeleo kwa sababu amejenga shule nyingi baadhi ya shule ni Chief Ihunyo iliyopo Kijiji cha Busegwe, shule ya msingi Busegwe, Chief Wanzagi, Chief Oswald Mang’ombe, Shule ya Sekondari Butuguri.
Wakati wa uhai wake moja ya nyumba ya makazi yake ilitangazwa kupigwa mnada ili kulipa madeni.
Mara kadhaa Mkono amezushiwa kifo kupitia mitandao ya kijamii ambapo tukio la kwanza lilikuwa mwaka 2020 jambo ambalo lilikanushwa na familia yake.
Mbali na hilo pia moja ya ofisi zake zilifungwa kutokana na kile kilichoelezwa na TRA kuwa anadaiwa kodi ambapo baada ya muda ilifunguliwa.
0 Comments