Fisimaji wamekuwa wakipungua kwa kasi sana duniani licha ya kuwa ni viumbe vyenye kupendeza na kutegemea sana maisha yao kwenye maji.
Upo mwingiliano mkubwa baina ya Fisimaji na binadamu hususani wavuvi, uliosababisha kuuwawa kwa wingi aidha kwa kuwindwa au kujinyonga na mitego ya nyavu zinazotumiwa na wavuvi kwa ajili ya kuvua samaki.
Mgogoro baina ya Fisimaji na wavuvi unatokana na Fisimaji kula samaki hatua inayowachukiza wavuvi na kuona kama uwepo wao utapunguza samaki kwenye maeneo wanayovua.
Changamoto nyingine ni mila potofu juu ya Fisimaji, baadhi ya waganga wa jadi wanaamini fisimaji ana mzizi ambao huutumia kujipatia samaki hivyo basi yeyote atakae muua na kuupata atakuwa tajiri.
Wengine husema ngozi ya fisimaji hutibu kifafa endapo mtoto atalala juu yake na akifungwa kwenye mkono wake.
Wapo walioenda mbali zaidi kwa kusema Fisimaji anaongeza nguvu za kiume, hivyo nyama au supu ya uume wa Fisimaji imekuwa hitaji la wanaume wengi na hivyo kusababishwa kuwindwa.
Jambo jingine ni kukauka kwa vyanzo vya maji kutokana na mabdadiliko ya tabia nchi, kuchafuka kwa maji kwa kuvamiwa na wakulima wanaotumia sumu kuua wadudu au mbolea za kemikali kukuza mazao hususani mboga mboga na matunda.
Kutokana na matishio niliyoyaanisha hapo juu, mhifadhi Wanyamapori Tarafa ya Mikumi iliyopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro, Makene Ngoroma kwa kushirikiana Atupele Camp wameiona haja ya kumlinda na kumuhifadhi mnyama huyo ili asitoweke.
Makene alisema hakuwahi kujua kama kuna Fisimaji hadi pale walipotega kamera kwenye moja ya maeneo ya mto Msowera ulioanzia Kijiji ha Udunghu, kitongoji cha Vidunda ambako kuna maporomoko ya Chizua na Kigaga.
Kinyesi cha Fisimaji
“Tulikuwa tunakutana na kinyesi na awali nilipokuwa naulizwa nilikuwa natoa majibu ya uongo juu ya kinyesi hicho na nilijua ni ya mbwa, lakini swali lilikuwa likijirudia kila nilipokuwa na wageni.
"…Nikaiona haja ya kuuliza mwenyeji, akasema hicho ni kinyesi cha Fisimaji, ili kujiridhisha mwaka jana tukaweka kamera na Januari mwaka huu tukajiridhisha kuwa ni Fisimaji na wanatumia sehemu ya mto Msowera kuendeleza maisha yao.”
Anasema kutokana na tishio la wanyama hao kutoweka wameamua kutafuta namna sahihi ya kuwalinda na kuwahifadhi na njia watakayotumia ni kulinda makzi yao kwa kutoa elimu kijijini, mashuleni pamoja na kupanda miti kwenye eneo la mto.
Makene Ngoroma
Ili kupunguza hatari hizo na nyngine ambazo zinawakabili wanyama hao ni muhimu kuwa na matumizi bora ya ardhi.
Ikumbukwe wanyama hawa wapo katika ngazi ya juu kabisa ya mfumo wa chakula (top of the food chain) kwa maana ya kwamba wanaweza kuwa wa kwanza kupotea kwenye mazingiria endapo chochote kisicho sawa kitaendelea katika maeneo wanayo ishi.
Ukweli ni kwamba Tanzania imebarikiwa kwa kuwa na bioanuai za aina mbalimbali kama vile mimea na wanyama .
Miongoni mwa makundi ya wanyama ambayo nchi yetu imeweza kupewa kipaumbele cha kuwa makazi yake ni wanyama wanaokula nyama (kanivora).
Moja ya picha za Kamera zilizomnasa Fisimaji
Fisi maji ni miongoni mwa aina 35 za wanyama wanaokula nyama ambao wanapatikana Tanzania. Fisimaji hawa wapo katika makundi kumi na tatu ulimwenginu, kati ya hayo matatu yapo Afrika na mawili yanapatikana Tanzania.
Aina ya fisi maji wanoapatikana Tanzania ni pamoja na Fisimaji madoa (spotted necked otter) na Fisimaji mkubwa kijivu (African clawless otter).
ASILI YA JINA FISIMAJI
Jina hili la Fisi maji pamoja na mambo mengine limetokana na mfanano wao na fisi wan chi kavu huku wao wakifurahia maji zaidi.
Maumbile yao yamefanana na Fisi na wanaishi kwa kula na kutembea usiku kama Fisi wa kawaida ila tu maisha yao kwa ujumla yanategemea maji.
Kama nilivyotangulia kuandika hapo juu, chakula kikuu cha mnyama huyu ni samaki na uduvi japokuwa kuna wakati hulazimika kula vyura.
Fisi maji wanapatikana katika maji yanayotembeea na wanapenda maji masafi na yaliyo mbali na makazi ya watu nae neo lao angalau liwe na mawe mawe.
Kwa Tanzania Fisimaji wanapatikana kwenye maziwa mfano Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Mito mikubwa kama Ruaha na Kilombero, mabonde yenye ardhi oevu za kudumu kama vile Ngwazi Mufindi, pamoja na maeneo ya miinuko mikali yenye unyevu nyevu na upatikanaji wa chakula mzuri kama vile kwenye maporomoko ya Rungwe.
Fisimaji hutumia mashimo au majani makubwa pembezoni mwa chanzo cha maji kama maeneo yake ya malazi pamoja na mawe kama maeneo yake ya kujikaushia. Fisimaji hapendi baridi, na ndio maana maeneo mengi ulimwenguni ambako kuna baridi kali huwezi kuwakuta.
0 Comments