WANAOPAKI magari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili watalazimika kulipia ili kuondoa changamoto ya msongamano wa vyombo vya usafiri vinavyoingia hospitalini hapo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Profesa Mohamed Janabi, amesema utafiti uliofanywa na uongozi wa hospitali hiyo umebaini kuwa magari yanayoingia ni kati ya 3200 hadi 3800 kila siku ambapo yanayopaki wakati wowote ndani ya hospitali ni magari 1000 huku uwezo wa maegesho ukiwa ni 250.
Profesa Janabi amesema msongamano huo wa magari unasababishwa na wananchi kugeuza hospitalini kuwa eneo la maegesho kwani huacha magari yao ndani ya maeneo ya hospitali na kwenda kwenye shughuli zao.
"Tulipofanya uchunguzi ikabainika kuwa magari kati ya 400 hadi 600 wenyewe hawapo hospitali hali inayosababisha kuwa na magari mengi hivyo kuleta adha kwa wananchi wanaofika kupata huduma ambapo inamchukua mtu takribani dakika 40 kutafuta sehemu ya kuegesha gari lake” amefafanua Prof. Janabi.
“Wale wanaoleta wagonjwa na kushusha kisha kuondoka hawatalipa kwani mtu atapaswa kulipa tozo mara baada ya dakika 20 tangu aingie hospitalini. Pia fedha zitakazopatikana zitatumika kuboresha maegesho yaliyopo na kujenga mengine ya ghorofa ili kuegesha magari mengi zaidi ili kuondokana na usumbufu uliopo”
Prof. Janabi amebainisha kuwa tozo hizi za maegesho hazitahusu magari ya watumishi wa hospitali zilizo ndani ya Muhimbili, magari ya kubeba wagonjwa na magari ya serikali.
0 Comments