Wanaume wanaonyanyua vitu vizito mara kwa mara wana asilimia kubwa ya kuwa rijali zaidi, Utafiti uliofanywa na Wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Harvard cha nchini Marekani umethibitisha.
Taarifa ya utafiti huo inaeleza kuwa Wanaume wenye utaratibu wa kunyanyua vitu vizito mara kwa mara au kuushughulisha mwili zaidi wana faida ya kuwa rijali kwa kuwa na mbegu nyingi za uzazi kuliko wanaume ambao kazi zao hazihitaji sana kuushughulisha mwili.
Wanasayansi wa chuo hicho wamefanya utafiti huo kwa lengo la kutafuta suluhisho la tatizo la utasa linaoonekana kuwa ni mtambuka.
Pia wamegundua kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya afya ya uzazi ya Mwanaume na mazingira yake ya kikazi na mahitaji ya kimwili.
Utafiti huo uliofanywa na Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Harvard na matokeo yake kuchapishwa katika jarida la “Human Reproduction” ulilenga kuchunguza namna kemikali kutoka katika mazingira na mtindo wa maisha inavyoweza kuathiri afya ya uzazi kwa mwanadamu.
Ulihusisha Wanaume na Wanawake 1,500 ambao walikuwa wakitafuta matibabu ya afya ya uzazi , ambapo wenza 377 walikuwa wakitafuta matibabu ya utasa.
Uchunguzi wa kina ulibainisha kwamba Wanaume walioripoti kufanya shughuli nyingi za kimwili katika maeneo yao ya kazi walikuwa na asilimia 46 zaidi ya idadi ya mbegu za uzazi ikilinganishwa na wale walio na kazi chache za kuushughulisha mwili muda wa kazi na wenye kufanya shughuli nyingi za kimwili kazini walikuwa na viwango vya juu vya homoni aina ya testosterone na kwa upande wa wanawake walikuwa na estrojeni.
0 Comments