Waziri Nape akikabidhiwa tuzo ya heshima na Mwenyekiti wa TEF, Deudatus Balile mara baada ya kuzindua mkutano wa 12 wa jukwaa hilo.
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari Tanzania kufanya kazi kitaaluma bila woga,upendeleo na uonevu.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo kupitia kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akifungua Mkutano wa 12 wa kitaaluma wa Wahariri, unaofanyika mkoani Morogoro ukiwa umeandaliwa na Jukwaa la Wahariri nchini TEF.
"Rais Dkt. Samia anawasalimia sana, ameniambia, kazungumze nao waambie wafanye kazi kitaaluma bila woga, bila upendeleo wala uonevu, haya ni maneno yake mwenyewe," alisema Waziri Nape.
Nape alisema Rais Dkt. Samia ni muumini wa haki ya kujieleza na kutoa maoni, hivyo haoni sababu ya kuminya uhuru wa Habari.
"Rais alishawahi kuniambia wakati wa mchakato ya kupitia Sheria ya Habari kuwa tuhakikishe hatuingilii haki ya watu kujieleza.
"Nasi tumekuwa tukilifanya hilo, niwaombe kwa pamoja tutafsiri maono ya Rais wetu, yeye nia na dhamira yake ni kuona uhuru wa Habari unaleta tija kwa nchi."
Pamoja na mambo mbalimbali aliyozungumza kwenye ufunguzi huo, Waziri Nape alisema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa vyombo vya Habari ingawa anaamini wapo baadhi ya watendaji wa serikali wanakwamisha suala hilo, lakini watashughulika na watu wote wanaokwamisha nia njema ya Rais ya kutaka kuwe na uhuru wa kweli wa Habari.
Baadhi ya Wahariri wanaoshiriki mkutano huo, kutoka kushoto ni Gabriel Mushi, Jimmy Kiango na Absalom Kibanda
Katika mkutano huo Waziri Nape alipewa tuzo ya heshima ikiwa ni tuzo ya kwanza ya heshima kupewa Waziri wa Habari tangu nchi hii kupata uhuru.
Nape alikabidhiwa tuzo hiyo na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile.
0 Comments