Ticker

7/recent/ticker-posts

KUWEPO KWA FARU NDANI YA MIKUMI KUTAONGEZA IDADI YA WATALII

Hifadhi ya Taifa Mikumi, ni Moja kati ya hifadhi muhimu nchini kutokana na kufikika kirahisi katika nyakati zote za mwaka.

Hata hivyo hifadhi hiyo inayoshika nafasi ya tisa kwa ukubwa nchini ikiwa na  kilomita za mraba 3230 kwa sasa inamkosa mnyama mmoja mkubwa kati ya watano wanaotambulika duniani.

Kati ya wanyama hao wakubwa watano duniani, hifadhi ya Mikumi inawamiliki wanne ambao  ni Simba, Tembo, Chui na Nyati huku  Faru akikosekana hifadhini.


Mhifadhi mwandazi Herman Mtei (kulia) akizungumza na baadhi ya Wahariri, aliye kushoto kwake ni Mhariri wa TBC, Anna Mwasyoke.

Sababu za kutoweka kwa Faru ambae awali alikuwepo zimetajwa na Mhifadhi Mwandamizi wa hifadhi hiyo, Herman Mtei kuwa ni ujangili.

Miaka ya nyuma hifadhi hiyo ilikuwa na Faru, lakini walitoweka hifadhini baada ya kuwindwa na majangili.

Hata hivyo Mtei alisema tayari hifadhi hiyo ambayo ipo wilayani Kilosa mkoani Morogoro imeshaanza kufanya utafiti Ili kuona kama kuna  uwezekano wa kumrudisha mnyama huyo ili akamilishe  idadi ya wanyama wakubwa watano maarufu duniani.


Mtei aliyasema hayo katika mazungumzo yake na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari nchini yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano uliopo ndani ya hifadhi hiyo.

Alisema kwa sasa wanyama maarufu waliopo katika hifadhi hiyo ni Tembo, Nyati, Simba na Chui.

Mtei alieleza kuwa  wameamua kufanya utafiti ili kuona uwezekano wa mnyama huyo kurudishwa katika maeneo hayo.


Sisi kama hifadhi tumeona umuhimu wa kufanya utafiti ili kuhakikisha tunamrejesha Faru, tukilifanikisha hili tutaweza kuitangaza hifadhi zaidi na watalii watapata nafasi ya kuona wanyama wote watano wakubwa.” 

Amesema kuwepo kwa Faru kutaweza kuitangaza hifadhi ya Mikumi zaidi na hivyo kuongeza idadi ya watalii kutokana na kupatikana kwa wanyama wote maarufu wakubwa.


Atakaporejeshwa katika hifadhi hiyo, atajengewa uzio maalumu kwa ajili kuzoea mazingira yaliyopo na baadae ataachiwa.

Mtei aliongeza kuwa kwa sasa si rahisi kusema mnyama huyo atarejeshwa lini kwenye hifadhi hiyo kwani bado utafiti unaendelea na utakapokamilika atapatikana.

"Unajua Faru ni mnyama adimu na analindwa haswa, sasa ukilazimisha aletwe hifadhini, halafu akapata madhara ni hatari zaidi na hilo ndilo linalosababisha suala hili kuchukua muda mrefu"

Post a Comment

0 Comments