Makamu wa Rais wa Marekeni,Kamala Harris
WAKAZI wa jiji la Dar es Salaam, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kumpokea Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris anaetarajiwa kuwasili nchini kesho Machi 29,2023.
Kamala anakuja nchini Kwa mwaliko wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dkt. Stergomena Tax ndie aliyetoa ombi hilo alipozungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa ujio wa Kamala utakuwa na neema kwa Tanzania kiuchumi, kijamii na diplomasia.
Kamala atapokelewa na Makamu wa Rais l Dkt Philip Mpango.
Machi 30 atafanya mazungumzo na Rais Dkt. Samia Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Mpango.
Dkt. Tax amesema Kamala na ujumbe wake watatembelea Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam na kukutana na vijana wajasiriamali wa Tanzania.
Waziri Tax amesema baada ya shughuli hizo za kikazi, Kamala atashiriki futari iliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais Samia siklu ya Alhamisi Machi 30, 2023.
"Pamoja na mambo mengine, ziara hii ya Mheshimiwa Kamala nchini Tanzania inalenga kuongeza nguvu katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania hususan baada ya kufanyika kwa mkutano kati ya Marekani na nchi za Afrika maarufu kama US – Africa Summit mwezi Desemba 2022, ambapo Rais Samia alihudhuria.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Tax
Ziara hii ni ya kihistoria, Makamu wa Rais wa Marekani ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo, anafanya ziara ya kikazi Tanzania na kukutana na Rais Samia, ambaye pia ni Rais wa kwanza mwanamke wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ziara hii inafanyika takriban miezi 11 tangu viongozi hawa wawili walipokutana Ikulu ya Marekani juu ya majukumu yao katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani uliodumu kwa miongo mingi tangu Tanzania ipate uhuru hadi sasa,” amesema.
Ziara ya Kamala nchini Tanzania inalenga katika kuunganisha nguvu za ushirikiano wa kimaendeleo kati ya nchi HIZI mbili katika sekta za afya, kilimo, utalii, uchukuzi, uchumi wa buluu, mawasiliano, uchumi wa kidijitali, uungaji mkono hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na uhimilivu wake.
Marekani imesajili miradi 266 yenye thamani ya dola za Marekani zaidi 4,000, ambayo imetoa ajira 54,584, hivyo matumaini yao ni kuona baada ya ziara hiyo wawekezaji wanaongezeka zaidi.
Tax amesema kwa miaka ya hivi karibuni sekta ya utalii imepokea watalii wengi kutoka Marekani ambapo kwa kipindi cha mwaka 2022 wamepokea watalii 100,600 kutoka watalii 66,394 mwaka 2015.
Makamu wa Rais Kamala ataambatana na mumewe ambaye atafanya mikutano na wadau wa michezo na utunzaji wa bahari kupitia program ya Tuheshimu Bahari.
Waziri Tax amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu ambazo Mheshimiwa Kamala na ujumbe wake watazitembelea ndani ya bara la Afrika ambapo ameanza ziara yake tarehe 25 hadi 28 Machi nchini Ghana na nchi nyingine ni Zambia.
0 Comments