Kiingilio cha shilingi 5,900, miundombinu rafiki na urahisi wa kufikika kwa urahisi kwenye Hifadhi ya Taifa Mikumi kumechangia idadi kubwa ya watalii wazawa kufika kwenye hifadhi hiyo iliyopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Hifadhi hiyo kwa sasa inatajwa kuongoza kwa kutembelewa na watalii wengi wa ndani kuliko hifadhi yeyote nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari nchini na Mhifadhi mwandamizi, Herman Mtei, jumla ya watalii waliotembelea hifadhi hiyo kwa mwaka 2022 ni 66,000 wengi kati yao wakiwa ni watalii wa ndani.
Katika kuhakikisha kunakuwa na ongezeko kubwa la watalii, hifadhi hiyo inatarajia kupokea watalii 80,000 kwa mwaka huu wa 2023.
Mtei amethibitisha kuwa Hifadhi ya Mikumi inapokea watalii wengi wa ndani na hilo linatokana na unafuu wa gharama za kuingia hifadhini na miondombinu rafiki.
Aliyasema hayo katika siku ya kwanza ya mafunzo ya siku mbili ya upashaji wa habari za Baionuwai yaliyofanyika mkoani Morogoro.
Mafunzo hayo kwa wahariri, yaliandaliwa na Internews na kuratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET).
Akizungumzia eneo la mapato, Mtei alisema kwa mwaka 2022 walipata kiasi cha tsh.2.6 bilioni na kwa mwaka huu matarajio yao ni kupata tsh. bilioni 4.
Aliongeza kuwa pamoja na idadi kubwa ya watalii kuwa wazawa, lakini pia wamekuwa wakipokea watalii kutoka nje ya nchi.
"Ni kweli watalii wengi ni wazawa, lakini hii haimaanishi hatupokei watalii kutoka nje, kwenye kiwanja chetu kidogo cha ndege kwa sasa tuna uhakika wa kupokea ndege nane kila siku."
Alisema pamoja na kuwa na malengo ya kupokea wageni 80,000 kwa mwaka 2023, dhamira yao kuu ni kupokea wageni 100,000 kwa mwaka.
0 Comments