Ticker

7/recent/ticker-posts

GARI ZINAUA WANYAMA 700 MIKUMI KILA MWAKA

Mhifadhi Utalii Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Herman Baltazary Mtei.

UREFU wa km 50 za barabara inayokatiza kwenye Hifadhi ya Taifa Mikumi zimekuwa janga kwa taifa kutokana na baadhi ya watumiaji wake kusababisha vifo kwa wanyama waliomo ndani ya hifadhi hiyo.

Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) limeweka wazi kuwa Kila mwaka inakadiriwa wanyama takribani 700 tofauti tofauti hupoteza maisha kwa kugongwa na magari.

Ofisa Mhifadhi Utalii wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Herman Mtei amedhibitisha hilo kwenye warsha ya siku mbili iliyohusisha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Katika warsha hiyo iliyoandaliwa na Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana na Inter News iliyofanyika Morogoro, Mtei alisema sababu kubwa ya ajali hizo ni mwendo kasi.


Pamoja na kuwepo vibao vyenye kuonesha kiwango cha mwendo (50) ambacho dereva anapaswa kuvifuata bado madereva wamekuwa wakaida na kuteketeza maisha ya wanyama."

Alisema katika kuhakikisha wanapata suluhu ya changamoto hiyo, sasa wako mbioni kufunga kamera za kuangalia vyombo vya moto vinavyopita hifadhini.

Uamuzi huo ni moja ya  mipango ya Tanapa ya  kulinda wanyama wanaovuka barabara hiyo.

"Lile ni eneo la hifadhi, wanyama wanatembea na kuvuka kushoto na kulia kwa ajili ya kwenda kutafuta chakula na maji, sio rahisi kwetu kuwazuia wasifike huko ila tunaweza kuzuia madereva wasiende kasi."

Amesema kukosekana kwa kamera kunawafanya madereva wengi kuendesha kwa kasi ya zaidi ya km 50 kinyume na taratibu zinavyotaka.


Mkurugenzi wa JET, John Chikomo

Mbali ya kuwepo kwa vibao vinavyoonesha kiasi cha mwendo hifadhini, lakini pia kuna adhabu na faini zimewekwa kisheria kwa wale wanaogonga wanyama.

Amesema faini zilizopo zinawafanya baadhi ya watu kulazimika kuyatelekeza magari yao hifadhini baada ya kuwagonga wanyama.

Utaratibu ni kwamba kila mnyama  ana kiwango chake cha  faini.  

Leo hii ukimgonga Twiga au Tembo mmiliki wa gari analazimika kulipa Dola 15,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 44.


Faini ya zaidi ya milioni 26 kwa aliyegonga Nyati ambazo ni dola 9,000.

Mtei amesema Tanapa wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kujua umuhimu wa hifadhi na faida yake kwa Taifa.

Mkurugenzi wa JET, John Chikomo amesema Chama hicho kitaendelea kupaza sauti juu ya masuala yote yanayohusiana na Mazingira wakiwemo wanyama.

"JET hatutachoka kutetea Mazingira kupitia kalamu zetu, hatutakubali kuona wanyama wanauwawa wakiwa kwenye maeneo yao halali."


Akiongea na AFRINEWS SWAHILI dereva wa gari kubwa linalobeba mizigo na kupeleka Zambia, Othmani Kaganda alikiri ajali za barabarani ndani ya hifadhi kuwa chanzo cha kuteketeza wanyama hifadhini, na hatua ya kuweka kamera itasaidia kupunguza ajali na mauaji ya wanyama.

Post a Comment

0 Comments