Migogoro nchini DRC imekuwa ikiendelea kwa miongo kadhaa, ambayo kiini chake ni utajiri wa rasilimali kiasi cha kudhani ni laana ya rasilimali. Hata hivyo, ubaguzi uliochochewa na uhamiaji ndiyo chanzo cha migogoro hiyo. Rais wa DRC,Felix Tshisekedi
Andiko hili linakuja kufuatia taarifa ya BBC Swahili ya tarehe 12/2/23, juu ya Wanajeshi saba kuhukumiwa kifo kwa kuonesha uoga. Je ni kweli walikuwa waoga au ni suala lingine? Aidha, ni nini chanzo cha kujiamini katika tamko la Msemaji wa Kundi la M 23 la tarehe 11/03/23 (Official Communique of 11/03/23).
Masuala hayo mawili yamenirudisha kwenye historia ya mgogoro ambao chanzo ni ubaguzi uliochochewa na uhamiaji. Uhamiaji huo ni wa wakati wa Karne ya 14 - 16, wakati wa utafutaji Makoloni, wakati wa ukoloni na baada ya ukoloni.
Katika Karne ya 14 - 16, Wafugaji wenye asili ya 'Nilotic' walifuata malisho na kuhamia katika misitu ya Kongo, ambako Wazawa walikuwa ni Wakulima wa Kibantu, na kusababisha mgogoro wa Wafugaji na Wakulima ambao ni Wahema na Walendu mtawalia.
Wakati wa utafutaji makoloni, Wapelelezi wa Mfalme Leopord II wa Ubeligiji, walipobaini rasilimali zilizopo, wakasema ni 'Free State'. Mfalme Leopord II, aliwatumikisha wenyeji kwa mkono wa shoka, kiasi cha wengi kubaki vilema au kuhama.
Mfalme Leopord II alinufaika hadi akapigiwa kelele juu ya ukatili wake, kisha akabadilisha kuwa Koloni la Ubeligiji, akiwa tayari ameacha mbegu za ubinafsi na ukatili.
Nchi za Ubeligiji na Ujerumani zilifikia makubaliano ambapo waliokuwa chini ya Koloni la Mjerumani (Burundi na Rwanda) walimiminika kuingia Kongo (Kivu) kuwa Vibarua kwenye Koloni la Mbeligiji, ambalo wenyeji wengi tayari ni vilema au wamehama.
Mbeligiji aliweka ubaguzi kati ya Watutsi na Wahutu, hali iliyowafanya Wahutu kuwa wanyonge kiasi cha wachache kukubali utaratibu wa kuhamia daraja la Kitutsi (Kututsishwa).
Madaraja yaliwafanya Wahutu waupinge ukoloni na kujikuta kwenye "Proxy War". Moja ya makabiliano hayo ni maeneo ya Walikale ambako Kundi lijulikanalo kama Kitawala lilianzishwa.
Watu wa daraja la chini hawakuruhusiwa kumiliki aridhi, ili watumike kwenye migodi na mashamba ya Wakoloni. Mwaka 1953, sera hiyo iliondolewa ikiwa imeisha acha chuki baina yao.
Waliokuwa daraja la Kati kwa Kivu Kusini wlikuwa wanaishi karibu na milima ya Mulenge, ambao chuki dhidi yao iliwafanya wazidi kupanda milimani, na kuamua kujiita 'Banyamulenge', ili kuachana na dhana ya 'Banyarwanda'.
Machafuko ndani ya nchi za Rwanda na Burundi kati ya mwaka 1959 - 1962 na mwaka 1973, yalisababisha Wakimbizi wengi nchini Kongo. Sanjari na wakimbizi hao, Mobutu Seseseko naye alipindua nchi na kuibadilisha jina kutoka Kongo kuwa Zaire.
Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Zagamba akiwa madarakani, aliwapa uraia 'Banyarwanda' wote waliokuwepo Kongo kabla ya 1885 (Naturalisation). Hata hivyo, kupewa uraia kulifanya makabila ya Nande, Hunde na Nyanga, kuhofia kwamba 'Banyarwanda' watachaguana katika uongozi, tofauti na awali waliporuhusiwa kupiga kura bila kugombea.
Bunge la Zaire, liliazimia kuwaondolea uraia 'Banyarwanda' waliokuwa wamepata uraia, kwamba waliupata isivyo halali, ambapo wahanga zaidi walikuwa ni 'Banyamulenge'.
Mauaji ya kimbari nchini Rwanda, yaliyoongezea Wakimbizi, ambao miongoni mwao ni Wahutu wa Kikundi cha 'Intarahamwe' kilichobadilisha jina na kuitwa 'Alliance for the Liberation of Rwanda - ALIR'.
Baadaye ALIR ilibadili jina tena kuwa 'Democratic Forces for the Liberation of Rwanda - FDLR', ambacho kimekuwa kwenye mgogoro mkubwa na Jeshi la Rwanda (RDF).
Changamoto za ubaguzi, zilimfanya Laurent Desiree Kabila (LDK) kutoka Jimbo la Katanga kushirikiana na RPF kuanzisha vuguvugu la kumuondoa Mobutu kwa kutumia Kikundi cha 'Alliance Democratic Forces for the Liberation of Congo' (AFDL).
Kikundi hicho kilipata msaada pia toka Jeshi la Uganda (NRA) na baadaye UPDF, kikiwa na Wapiganaji wengi wa Kitutsi hususan Banyamulenge, walioingia vitani na Jeshi la Zaire (Armed Forces of Zaire - FAZ) na kumuondoa Mobutu mwaka 1997.
Mwaka 1998, LDK aliwaondoa wasaidizi wake kutoka Uganda na Rwanda baada ya kutofautiana, ambao walianzisha vita nyingine, iliyokuja kuwa vita kubwa ya pili nchini DRC, baada ya jina la Zaire kubadilishwa. Vita hiyo iliwafanya Wanazuoni kujiuliza kama; Je kulikuwa na lengo la kuanzisha Himaya ya Kitutsi katika Afrika ya Kati!?
Vita hiyo ilianzishwa na Kundi la 'Congolese Rally for Democracy' (RCD - Goma, likiongozwa na Prof Wamba Dia Wamba, aliyekuwa anapata msaada kutoka Rwanda, likijumuisha Wahutu na Watutsi. Wamba baadaye alitofautiana na Viongozi Waandamizi wenzie na kwa kushirikiana na Mbusa Nyamwisi walianzisha Kundi jingine la RCD - Kisangani iliyokuja kuwa RCD - K - ML, iliyokuwa inapata msaada kutoka Uganda.
Vita hiyo ilihusisha Mataifa mengi hadi
Mataifa rafiki ya Rwanda na Uganda kupigana yenyewe ndani ya DRC. Katika vita hiyo LDK aliuwawa kwa risasi na Mlinzi wake mwaka 2001. Nafasi yake ilichukuliwa na mwanaye Joseph Kabila (JK).
JK aliingia kwenye Mikataba ya Amani mwaka 2002/2003 ambayo miongoni mwa makubaliano ilikuwa ni RCD kujumuishwa katika Jeshi la Serikali (FARD), Viongozi wake kupewa nyadhifa za juu na kuachiwa kufanya kazi/kumiliki eneo la Mashariki (Kivu), ambalo Serifuri alipewa kuwa Gavana.
Jenerali Laurent Nkunda, alijitoa katika makubaliano yale na kuanzisha Kikundi cha National Congress for the Defence of people CNDP akiwa pamoja na Gavana wa Kivu - Serifuri na wengineo, huku wakipata msaada toka Rwanda ili kushughulikia haki na maslahi ya "Banyarwanda" kwa kutaka kujitenga. Hata hivyo, Serifuli (Muhutu), hakuridhika kuwa na Nkunda na kuamua kujiondoa na kuanzisha Kikundi Kingine.
Katika tofauti hizo yalitokea mauaji ya Watutsi katika kambi ya Wakimbizi nchini Burundi ambayo yalihusishwa na kisasi cha Wahutu dhidi CNDP ambayo nayo iliua Wakimbizi. Hata hivyo, Kikundi cha 'National Liberation Forces' cha Burundi kilijitangaza kuhusika.
CNDP walikamata maeneo ya Goma mwaka 2008, ambapo UN waliilaumu Rwanda kumuwezesha Nkunda kufanya anayofanya. Aidha, UN na Rwanda walikubaliana, Rwanda imkamate na kumfikisha 'International Criminal Court' (ICC), ili UN nao waisaidie Rwanda kupambana na FDLR.
Makubaliano yalifikiwa tarehe 23/03/2009, ambayo yalihusisha; "Msamaha kwa Wafungwa wa Kivita", "Kuwaingiza Wapiganaji wa CNDP kwenye FARDC" na "Kuundwa kwa Operesheni ijulikanayo kama "UMOJA WETU".
Wapiganaji zaidi ya 16000 wa CNDP walijumuishwa kwenye FARDC, Bosco Ntaganda akiwa Naibu Kamanda wa Majeashi ya Jimboni Kivu. Hata hivyo migogoro na Vikundi vinavyomiliki silaha iliendelea ambayo ilihusisha Vikundi vyenye nia ya kujilinda katika maeneo yao, kujiendesha kiuchumi na kuishawishi Serikali iwalinde.
Vikundi vinavyomiliki silaha vilikuwa ni pamoja na MAIMAI na APCLS. APCLS ni 'Alliance of Patriots for a Free and Sovereign Congo', ambacho kinatetea Wazawa wa Kongo kubaki katika maeneo ya babu zao.
Wakati mgogoro na Vikundi vinavyomiliki silaha ukiendelea, makubaliano baina ya M 23 na FARDC, yalivunjika mwaka 2012 kutokana na uamuzi wa FARDC wa kutaka kuuvunja mtandao wa CNDP uliokuwa unaendelea Kivu, na ndio ukawa mwanzo wa Kundi la M 23.
M 23 iliendesha mapambano na FARDC kiasi cha kukamata maeneo mengi ya jirani na Goma, hadi walipoondolewa na Force Intervention Brigade (FIB) mwaka 2013. Waliokuwa Wapiganaji wa M 23 walikimbilia nchini Uganda kama Wakimbizi pakiwa na maswali mengi yasiyojibika juu ya ukimbizi wao.
Baada ya M 23 kuondolewa DRC, FARDC kwa kushirikiana na FIB walikabiliana na kikundi cha 'ADF - NALU' katika maeneo ya Beni.
'ADF - NALU' ni muunganiko wa Makundi mawili ya 'Alliance Democratic Forces' kilichokuwa kwenye milima ya Rwenzori nchini DRC, na Kikundi cha 'National Alliance for the Liberation of Uganda' ambacho kilianzia Masaka - Uganda na baadaye kukimbilia katika milima ya Rwenzori nchini DRC.
Kikundi kilikuwa kinaongozwa na Jamili Mukulu wa Uganda ambaye alikuwa akizunguka katika Mataifa mbalimbali hadi alipokamatwa mwaka 2015 nchini Tz na kukabidhiwa kwa jeshi la Uganda.
Msaidizi wake aitwaye Musa Baluku aliendeleza makabiliano na FARDC na Washirika wake huku akijinasibu kupata msaada toka ISIS, hadi Kundi lilipogawanyika, ambapo moja lilisalia Beni na lingine kukimbilia Ituri ambako mgogoro wa Wafugaji (Wahema) na Wakulima (Walendu) unaendelea.
Jukumu la kuiondoa ADF - NALU bado linaendelea ambacho ni Kikundi kinachoundwa na Kabila la Wanande wanaoishi Beni Butembo na Rubero ambao kwa pamoja na Wakonjo wa Uganda wanajiita "Kyaghandahira", wakiwa na tamaduni zinazofanana na 'Rwenzururu Empire', ambayo mwaka 2014 ilikuwa kwenye mgogoro mkubwa na Serikali ya Uganda.
Wakati makabiliano ya FARDC na ADF - NALU yanaendelea, Uganda iliingia kwenye makubaliano ya kuongeza nguvu katika kuwasaka ambapo katika kipindi hichohicho, Kikundi cha M 23 kiliibuka tena katika maeneo ya Goma. Nchi za Afrika Mashariki zimeanzisha juhudi za pamoja za kukabiliana nalo, huku mauaji maeneo ya Beni na Ituri yakiendelea.
Kufuatia historia hiyo ya ubaguzi uliochochewa na uhamiaji, migogoro ndani ya DRC inaendelea. Aidha, adhabu ya kifo iliyotolewa mahakaman, pia lile tamko la msemaji wa M 23, yana ashiria uwepo wa Wapiganaji pandikizi kila upande, kama kilivyo chakula aina ya Makande ambacho hata ukitofautisha mahindi na maharage, mchuzi utabaki na mchanganyiko wa vyote. Hata hivyo, mamlaka za usuluhishi zinaendelea na juhudi za kutafuta AMANI YA KUDUMU.
Ahsante kwa kusoma
MAKALA HAYA NI KWA HISANI YA UWANJA WA DIPLOMASIA
0 Comments