Ticker

7/recent/ticker-posts

AHN YARAHISISHA ZAIDI HUDUMA ZA KUSAFISHA FIGO TANZANIA

 

 

NA MWANDISHI WETU, AFRINEWS DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Huduma za Afya Afrika maarufu kama Africa Healthcare Network (AHN) sasa umerahisisha kwa kiasi kikubwa huduma za usafishaji wa figo (dialysis) nchini Tanzania na kwa gharama nafuu.


Mbali ya kutoa huduma hiyo kwa gharama nafuu, lakini pia AHN imesogeza huduma za kibingwa na kibobezi karibu na wananchi.


Mtandao huo hadi sasa una vituo 16 vya kutoa huduma ya kusafisha figo nchini Tanzania.



DK. EGINA MAKWABE


Akizungumza na AFRINEWS SWAHILI mwanzoni mwa wiki hii, Mkurugenzi wa Tiba kutoka AHN, Dk. Egina Makwabe, alisema mtandao huo ambao upo kwenye nchi mbalimbali za Kusini mwa Jangwa la Sahara, umekuwa ukifanya kazi ya kutoa huduma za afya na hasa afya ya magonjwa ya ndani ukiwemo usafishaji wa figo.

 

Alisema wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa kushirikiana na mashirika bora ya afya Tanzania na Afrika kwa ujumla, ambapo wamefanikiwa kuweka vituo 16 vya kusafisha figo.


“Tumekuwa tukifanya hivyo tangu mwaka 2018 kwa bei nafuu na pia bima ya afya inatumika, tunafanya kazi vizuri na hospitali 16 nchini, kikubwa kinachofanywa na mtandao wetu ni kuendesha vituo hivyo, lakini pia tunajenga na kuleta mashine za kisasa, wataalamu na wafanyakazi na kutoa huduma,” alsiema Dk. Makwabe.


Alizitaja baadhi ya hospitali wanazoshirikiana nazo katika mikoa mbalimbali nchini kuwa ni Hindumandal, CCBRT, Cardinal Rugambwa Ukonga,jijini Dar es Salaam, Serian Arusha, Saint Francis Ifakara, Morogoro, Saint Joseph Peraminho Ruvuma, Nkinga Mission Hopital , Saint Joseph Sengerema na Saint Joseph Kilimanjaro.


Dk. Makwabe kushoto akiwa na Wahariri wa mtandao huu

Dk. Makwabe alisema wamekuwa wakitoa huduma hiyo kwa kushirikiana na hospitali hizo, ambapo wao wamekuwa wakipeleka vifaa na wataalamu huku washirika wao wakitoa maeneo yao.

Alisema fedha inayopatikana kwenye huduma hiyo imekuwa ikitumika kwa shughuli za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kuwalipa mishahara wataalamu na ukarabati wa mashine zinazo haribika.


Akijibu swali la kutokuwepo kwa Hospitali inayosimamiwa na taasisi za Kiislamu, alisema: Bahati mbaya mpaka sasa hatujapata Hospitali ambayo inasimamiwa na taasisi yeyote ya kiislamu, lakini kuna hospitali mpya inajengwa ipo Tabata bado haijafunguliwa, hii itakuwa chini ya BAKWATA kwa asilimia 100, tayari tumeanza kufanya mazungumzo nao na ikiwa tayari tutashirikiana nao katika kutoa huduma hiyo,” alisisitiza   



Dk. Makwabe kulia akiwa na Mhariri wa mtandao huu, Sidi Mgumia 


Mtandao huo wa kwanza kuanzishwa Kusini mwa Jangwa la Sahara umekuwa ukitoa huduma za uhakika za afya. 

AHN ilianzishwa nchini Tanzania kama Africa Healthcare Network, Machi 3, 2017.

 

Hatua  hiyo ya AHN inakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kupunguza gharama za kusafisha figo.

Ikumbukwe kuwa gharama za matibabu ya kusafisha figo ni kubwa na hazibebeki, ambapo mwaka jana serikali kupitia Wizara ya Afya iliweka wazi kuwa inafanya mapitio ya kupunguza gharama hizo.


Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, alitoa ahadi hiyo bungeni, ambapo alisema mkakati wa serikali katika kupunguza gharama za kusafisha figo ni kununua vifaa tiba na vitendanishi moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji. 

Dhamira ya Serikali ni kushusha kiwango cha gharama ambacho kinafikia shilingi 900,000 kwa mgonjwa na pengine iwe shilingi 50,000.

 

Post a Comment

0 Comments