Washiriki wa mafunzo ya Uhifadhi wa wanyamapori na bioanuai wakiwa katika picha ya pamoja. |
Na Sidi Mgumia, aliyekuwa Bagamoyo
SHUGHULI za kibinadamu hususan kilimo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuyaharibu mapito ya Wanyama maarufu kama ushoroba.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni
wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na Dk. Elikana Kalumanga ambaye ni Meneja
Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi wa Mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya
Kimataifa (USAID) wa Tuhifadhi Maliasili, wakati wa mafunzo ya waandishi wa
habari za mazingira kuhusiana na masuala ya mradi huo.
Dk.Kalumanga alisema shoroba hizo zimekuwa zikiathiriwa na shughuli za
binadamu hususani kilimo na kuhatarisha uwepo wa maeneo hayo na maisha ya
wanyamapori kwa ujumla.
“Shoroba mbalimbali nchini zimekuwa zikiathiriwa na shughuli za binadamu kama vile kilimo na nyinginezo na kuhatarisha uwepo wa maeneo hayo na maisha ya wanyama kwa ujumla,” alisema
Alisema shoroba zina changamoto zake ambapo kwa upande
mmoja kuna shoroba nyingi ambazo ziko
vizuri na zinapitikana lakini zipo ambazo takwimu za Serikali zinaonyesha kuwa zilikuwepo
lakini zimetoweka kutokana na shughuli za wanadamu ambazo si endelevu.
“Kwakweli kumekuwa na changamoto katika uhifadhi wa shoroba
na kama tunavyoona kuwa kwenye zingine kuna makazi ya watu, shughuli za kilimo
na kitu cha kwanza ambacho tunakiona ni kwamba kuna shoroba nyingi hazikuwa
zimeainishwa, zilikuwa hazijulikani kwa wananchi, kwahiyo watu wamekwenda
wameweka makazi, shughuli za kilimo kwasababu zilikuwa hazitambuliki. Lakini
pili zipo ambazo zilikuwa zinatambulika na wanyama wamekuwa wakizitumia lakini
hakukuwa na mikakati au mipango ambayo ilikuwa inaelekeza namna gani hayo
maeneo yahifadhiwe na ndio maana tunaona Serikali sasa inakuja na mikakati ya
kufikiria sasa ni namna gani shorobo hizi zihifadhiwe au kwa ujumla kuwe na
maendeleo endelevu sababu yana umuhimu wake kuchumi, kijamii na pia katika mambo
ya mazingira na kiikolojia,” alisema
Akijibu hoja ya kama kuna uwezekano wa kurejesha shoroba
zilizotoweka, Dk. Kalumaga alisema shoroba hata kama imeharibika kuna uwezekano
wa kuzirejesha na ndio maana kuna juhudi za zakurudishia shoroba kwenye
uhalisia wake.
“Tumeona pia kuna taasisi mbalimbali zikishirikiana na Serikali
kuzirudisha shoroba kwenye uhalisia
wake. Moja wapo ya shoroba ambayo imefanyiwa maboresho ni ile inayoounganisha
Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa, Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Pori la Akiba la Selous,
chini ya ufadhili wa Mradi wa USAID wa Tuhifadhi Maliasili,” alisema
Dk. Kalumanga aliongeza kuwa kwenye
shoroba hizo wananchi wanapata vitu vingi kama dawa, kuni huku akitolea mfano
shoroba ya Laja inayotoka hifadhi ya Taifa ya Manyara kuelekea eneo la hifadhi
ya Taifa ya Ngorongoro, kuwa kuna Wahadzabe ambao wanategemea maeneo hayo
kupata mahitaji yao muhimu kama vile makazi na chakula.
"Katika shoroba hizi kuna wanyamapori wanaowavutia
watalii jambo ambalo linafanya kuwepo uwekezaji wa hoteli
mbalimbali ambazo zinatoa ajira kwa watanzania na wapo wananchi wameweka bidhaa
zao za asili na kuwauzia wazungu na watalii wengine, " alisema Dk.
Kalumanga
Kwa upande wake John
Steven Noronha, Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa Mradi wa Shirika la Marekani
la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wa Tuhifadhi Maliasili alisema migogoro kati
ya binadamu na wanyamapori ni kikwazo kikuu cha kuunganisha uhifadhi na
kupunguza umaskini, kwani gharama za kuishi na wanyamapori huathiri vibaya
maisha ya jamii zilizo kando kando ya hifadhi za taifa na kuzorotesha usaidizi
wa jamii kwa ajili ya uhifadhi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), John Chikomo ameongeza kuwa katika mapambano dhidi ya changamoto za mabadiliko ya tabia nchi elimu ya mazingira na haswa uhifadhi bado inahitaji iepelekwe kwenye jamii lakini pia kusisitiza uwepo wa ushirikishwaji wa sekta na wizara mbalimbali katika masuala ya mazingira.
Nae Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru alisisitiza kuwa ni
jukumu la waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kuchechemua na kuziibua
changamoto za shoroba na kuelimisha jamii juu ya athari zake lengo likiwa ni
kupeleka mambo mapya kwa watunga sera ili wayafanyie kazi mapendekezo yakutatua
changamoto za mausala ya uhifadhi kwa ujumla wake.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za
Mazingira Tanzania (JET), Dk. Ellen Otaru akizungumza na washiriki wa mafunzo |
Mafunzo hayo ambayo yalianza Januari 12, 2023 yameratibiwa
na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) chini ya ufadhili
wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi wake wa
Tuhifadhi Maliasili.
0 Comments