Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye NA MWANDISHI WETU, AFRINEWS-DODOMA |
LAINI za simu milioni mbili ziko mbioni kufungwa kutokana na kutohakikiwa.
Uamuzi huo umetangazwa leo na Serikali baada ya muda uliotolewa kwa wananchi kukamilisha zoezi hilo kuelekea ukingoni.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ndie ametoa taarifa hiyo leo januari 24,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma.
“Sababu ya kuzifungia laini hizo ni kuondoa utapeli uliopo hivi sasa kupitia simu za mkononi kwani laini zinazotumika ni zaidi ya milioni 60 katika watu milioni 61 tuliopo hapa nchini.
“Eneo hili la mawasiliano linagusa watu wengi lakini hata hivyo kuna utapeli mwingi ndio maana tuliposema watu wafanye uhakiki ni laini milioni 58 tu ndiyo zilisajiliwa na zaidi ya milioni mbili hazijahakikiwa.”
Hata hivyo alisema Serikali imeongeza muda wa kuhakiki laini zao kutoka Januari 31 mwaka huu Hadi February 13 mwaka huu ili kutoa nafasi zaidi kwa watu kuhakiki laini zao.
“Zipo laini nyingi mtaani na nyingi zinatumika katika utapeli ,wapo mawakala wasiokuwa waaminifu kwani wanahifadhi namba na picha za watu wenye namba za NIDA na kuwasajilia watu wengine huku muhusika mwenyewe akiwa hajui kama jina lake linatumika na watu wengine na nyingine ndiyo hizo zinatumika katika utapeli,hivyo tutazima laini zote zilizosajiliwa kwa uongo lengo kubwa ni kuondoa matapeli.
0 Comments