Ticker

7/recent/ticker-posts

ILO:UHAMAJI SALAMA WA WAFANYAKAZI CHANZO CHA UKUAJI WA UCHUMI NA ULINZI WA HAKI ZA WAFANYAKAZI TANZANIA

Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa ILO, Bi. Aida Awel,
Uhamaji wa wafanyakazi umeendelea kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania na Ukanda wa Pembe ya Afrika Mashariki, huku wadau wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi ili kuhakikisha wafanyakazi wanahama kwa njia salama, zenye usawa na zinazolinda haki zao.

Wito huo umetolewa  Juni 10,2026 wakati wa warsha maalum kwa waandishi wa habari kuhusu Usimamizi wa Uhamaji wa Wafanyakazi Tanzania na Ukanda wa Pembe ya Afrika Mashariki (EAHoA), ulioandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) jijini Dar es Salaam.


Akizungumza katika mkutano huo, Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa ILO, Bi. Aida Awel, alisema uhamaji wa wafanyakazi ni miongoni mwa masuala muhimu zaidi duniani kwa sasa kutokana na mchango wake katika uchumi, maendeleo ya jamii na ustawi wa familia.

Alisema mamilioni ya watu katika Ukanda wa Pembe ya Afrika Mashariki huhama kila mwaka wakitafuta ajira, elimu, usalama na fursa bora za maisha, jambo linalofanya uhamaji kuwa sehemu ya uhalisia wa maisha ya watu wengi.


“Nyuma ya kila takwimu ya uhamaji kuna simulizi ya maisha ya mtu. Hawa ni vijana wanaotafuta ajira zao za kwanza, wazazi wanaopambana kuhudumia familia zao na wafanyakazi wanaotafuta maisha bora na yenye heshima,” alisema.

Kwa mujibu wa Bi. Awel, Tanzania ina nafasi ya kimkakati katika mfumo wa uhamaji wa kikanda kutokana na kuwa na moja ya idadi kubwa zaidi ya vijana barani Afrika wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka.


Alisema pamoja na uwepo wa fursa mbalimbali, vijana wengi hukabiliwa na changamoto za upatikanaji wa ajira, kuongezeka kwa ajira zisizo rasmi, kutokuwiana kati ya ujuzi na mahitaji ya soko la ajira pamoja na ukosefu wa taarifa sahihi za ajira.


Kutokana na hali hiyo, alisema uhamaji wa wafanyakazi umekuwa moja ya mikakati muhimu inayotumiwa na kaya nyingi kuboresha maisha na kuongeza kipato.


“Watanzania wengi wanaendelea kutafuta fursa za ajira ndani ya Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani, ikiwemo nchi za Ghuba. Wakati huohuo, Tanzania inapokea wafanyakazi kutoka nchi jirani wanaochangia ukuaji wa sekta mbalimbali kama kilimo, ujenzi, biashara, usafirishaji, ukarimu na kazi za majumbani,” alisema.


Bi. Awel alisisitiza kuwa changamoto si uhamaji wenyewe, bali ni kuhakikisha unafanyika kwa njia salama, za kisheria, zenye utaratibu na zinazoheshimu haki pamoja na hadhi ya wafanyakazi.

Alionya kuwa bila mifumo madhubuti ya ulinzi, wafanyakazi wahamiaji wanaweza kukumbana na udanganyifu katika ajira, gharama kubwa za usajili na uajiri, taarifa potofu, mazingira duni ya kazi pamoja na ukosefu wa huduma za hifadhi ya jamii na haki za msingi, hasa kwa wanawake na vijana.


Aidha, aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua mbalimbali inazoendelea kuchukua katika kuimarisha usimamizi wa uhamaji wa wafanyakazi kupitia maboresho ya sera, kuimarisha mifumo ya taarifa za soko la ajira, kukuza ushirikiano wa kikanda na kuhamasisha ajira za haki.


Alisema ILO inaendelea kushirikiana na serikali kupitia Mpango wa Better Regional Migration Management unaolenga kuimarisha usimamizi wa uhamaji, utambuzi wa ujuzi, upatikanaji wa taarifa za soko la ajira na ulinzi wa wafanyakazi wahamiaji katika hatua zote za safari yao ya ajira.


Hata hivyo, Bi. Awel alisisitiza kuwa sera na sheria pekee hazitoshi bila wananchi kuwa na taarifa sahihi kuhusu uhamaji.

“Watu wanahitaji taarifa sahihi ili kufanya maamuzi sahihi. Jamii zinapaswa kuelewa uhalisia wa uhamaji, na wafanyakazi wanahitaji kufahamu njia salama zilizopo. Hapa ndipo nafasi ya vyombo vya habari inapokuwa muhimu sana,” alisema.


Aliwataka waandishi wa habari kuendelea kuripoti masuala ya uhamaji kwa usahihi, uwiano na uwajibikaji ili kusaidia kupambana na upotoshaji wa taarifa, kuondoa mitazamo hasi dhidi ya wahamiaji na kuimarisha mshikamano wa kijamii.


Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Vijana, Bw. Oddo Hekela, alisema Tanzania haitazamii kujenga uchumi wake kwa kutegemea fedha zinazotumwa nyumbani na wafanyakazi walioko nje ya nchi kama ilivyo katika baadhi ya mataifa mengine.


Alisema pamoja na mchango wa uhamaji katika maendeleo ya uchumi, kipaumbele kikuu cha Tanzania ni kuhakikisha haki, hadhi na ustawi wa wafanyakazi vinazingatiwa wakati wote.

“Kipaumbele chetu cha kitaifa ni ulinzi wa wafanyakazi. Tunataka kuhakikisha kila Mtanzania anayehamia kufanya kazi nje ya nchi anafanya hivyo kwa usalama, kwa heshima na kwa mujibu wa sheria,” alisema.


Bw. Hekela pia alizungumzia changamoto ya uhamaji usiofuata taratibu na umuhimu wa matumizi sahihi ya istilahi zinazohusu uhamaji katika mijadala ya umma ili kujenga uelewa sahihi kuhusu suala hilo.


Washiriki wa mkutano huo walikubaliana kuwa ushirikiano wa karibu kati ya serikali, waajiri, vyama vya wafanyakazi, washirika wa maendeleo na vyombo vya habari ni muhimu katika kujenga mfumo salama, wa haki na wenye manufaa kwa wafanyakazi na uchumi wa Tanzania.

Post a Comment

0 Comments