Ticker

7/recent/ticker-posts

KISA CHA MWAMWINDI NA DKT. KLERUU: GABO AMEUVAA UHUSIKA

Salim Ahemd Issa maarufu kama Gabo Zigamba, jamaa anajua kuigiza mpaka anajua tena, hakuna shaka yeyote kuwa msanii huyu kwa sasa ndio anaweza kuwa kinara wa uigizaji wa filamu zenye maudhui bora yanayoweza kutazamwa na mtu yeyote na mahali popote.

Stori, mandhari na utayarishaji wa filamu za Gabo unavuta hisia za kweli kwa mtazamaji, hana papara awapo mbele ya kamera, anabeba hisia za kweli kwenye kila tukio analoliigiza. Ndio, huyu ni Gabo Zigamba.


Jambo linalosadifu ukweli wa aya zangu mbili za hapo juu ni filamu yake mpya ya Mwamwindi. Ieleweke kuwa kuna baadhi ya matukio katika historia ya Tanzania hayafutiki kirahisi katika kumbukumbu za wananchi. 

Ni matukio ambayo yalibadili namna watu walivyofikiri, yalizua mijadala mikubwa na kuacha alama ya kudumu katika simulizi za taifa. 


Miongoni mwa matukio hayo ni mauaji ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Katibu Mwenezi wa TANU, Dkt. Kleruu, yaliyotokea siku ya Krismasi mwaka 1971.

Miaka zaidi ya hamsini baadaye, msanii na mwigizaji Gabo ameibeba historia hiyo na kuifufua kupitia filamu fupi ya Mwamwindi, kazi ya sanaa inayosimulia kwa ustadi tukio hilo lililotikisa Tanzania na kuvuta hisia za watazamaji wengi.

Filamu hiyo inaangazia mgogoro ulioibuka kutokana na masuala ya ardhi na utekelezaji wa sera ya ujamaa wakati wa awamu za mwanzo za ujenzi wa taifa. 


Katika simulizi hilo, mkulima Mwamwindi analazimishwa kuhamia kwenye mfumo wa vijiji vya ujamaa, jambo ambalo linazua mvutano mkubwa kati yake na viongozi wa serikali.

Hata hivyo, kinachoonekana kuwa kilele cha mgogoro huo ni tukio la kusikitisha ambapo Dkt. Kleruu anadaiwa kuonesha dharau mbele ya kaburi la wazazi wa Mwamwindi. 


Kwa Mwamwindi, hilo halikuwa suala la kawaida. Lilikuwa jambo lililogusa utu, heshima na kumbukumbu za familia yake. Hasira zilipofikia kiwango cha juu, akaamua kuchukua bunduki na kumpiga risasi Mkuu huyo wa Mkoa, tukio lililogeuka kuwa habari kubwa ndani na nje ya Tanzania.


Kwa ustadi mkubwa wa uigizaji, Gabo amefanikiwa kuivaa tabia ya Mwamwindi kwa namna inayomfanya mtazamaji kuhisi maumivu, hasira, msukumo na mazingira yaliyomzunguka mhusika huyo. Kila tukio linaonekana kuwa halisi kiasi cha kumrudisha mtazamaji katika mazingira ya Tanzania ya miaka ya sabini.


Tukio la mauaji ya Dkt. Kleruu lilikuwa miongoni mwa habari zilizotikisa taifa wakati huo. Wapo wanaoamini kuwa tukio hilo liliwafanya baadhi ya viongozi wa serikali kutafakari upya namna ya kutekeleza sera za vijiji vya ujamaa, hasa pale ambapo utekelezaji wake ulionekana kwenda kinyume na matakwa au hisia za wananchi katika maeneo mbalimbali.


Baada ya tukio hilo, Mwamwindi ambae alijipeleka mwenyewe polisi, alifikishwa mahakamani na hatimaye kuhukumiwa kunyongwa. Hukumu hiyo ilitekelezwa, na hivyo kufunga ukurasa mmoja wa simulizi lenye majonzi, hasira na mafunzo mengi ya kihistoria.



Lakini ni muhimu pia kumkumbuka aliyekuwa mhanga wa tukio hilo. Dkt. Kleruu alikuwa mmoja wa wasomi wa mwanzo kabisa wa Tanzania. Akiwa mzaliwa wa Kilimanjaro, alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu (PhD) ya Sayansi ya Siasa mwaka 1962 kutoka Chuo Kikuu cha California nchini Marekani. Alikuwa sehemu ya kizazi cha viongozi wasomi waliobeba matumaini makubwa ya taifa changa la Tanzania kwa wakati huo.


Historia ya Dkt. Kleruu imeendelea kuishi kupitia sanaa kwa miaka mingi. Hii si mara ya kwanza kwa tukio hilo kupewa nafasi katika kazi za kisanii. 

Mwanamuziki nguli Mbaraka Mwinshehe aliwahi kuimba wimbo unaogusia tukio hilo, jambo linalodhihirisha jinsi simulizi hiyo ilivyoendelea kubaki katika kumbukumbu za jamii kwa miongo mingi.


Kilichonifurahisha zaidi baada ya kuitazama Mwamwindi si tu ubora wa uigizaji wa Gabo, bali namna ambavyo timu nzima ya uzalishaji ilivyolichukulia tukio hilo kwa uzito unaostahili. 

Kuanzia script, mpangilio wa matukio, uchaguzi wa wahusika hadi uelekezaji wa filamu, kila eneo linaonesha maandalizi makubwa na heshima kwa historia inayosimuliwa.


Kwa ujumla, Tanzania ina hazina kubwa sana ya matukio ya kihistoria yanayoweza kutumika kufundisha, kuburudisha na kuhifadhi kumbukumbu za taifa. 


Kupata wasanii kama Gabo wanaothubutu kuyafukua matukio hayo na kuyageuza kuwa filamu ni jambo la kupongezwa. Kazi kama hizi si burudani pekee, bali ni maktaba hai kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


Hakika, Gabo ameuvaa uhusika. Na kwa kushirikiana na timu yake ya production, script na direction, wamewasilisha kazi yenye ubora, uzito wa kihistoria na thamani kubwa kwa jamii.

 

Post a Comment

0 Comments