●Tanzania na Singapore katika safari mpya ya masoko ya kaboni duniani
Na Fatma Jalala
Ulimwengu unaelekea katika mabadiliko makubwa ya mfumo wa uchumi unaotambua thamani ya mazingira kama mali ya kiuchumi. Katika mwelekeo huu, Tanzania imejikuta katika nafasi ya kimkakati kupitia ushirikiano wa kimataifa unaojikita katika mabadiliko ya tabianchi na biashara ya hewa ukaa, hatua inayoiunganisha moja kwa moja na mfumo wa uchumi wa kaboni duniani.
Msingi wa mabadiliko haya upo katika Mkataba wa Paris wa mwaka 2015, hususan Ibara ya 6, ambayo ndiyo nguzo kuu ya masoko ya kaboni duniani. Ibara hii inaruhusu nchi kushirikiana katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kupitia uhamishaji wa matokeo ya upunguzaji huo kati ya mataifa. Ndani ya Ibara ya 6.2, nchi mbili au zaidi zinaweza kufanya biashara ya moja kwa moja ya matokeo ya upunguzaji wa hewa ukaa, huku Ibara ya 6.4 ikiweka mfumo wa kimataifa wa soko la kaboni chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.
Katika muktadha huo, Tanzania inapata nafasi ya kuuza au kuhamisha mikopo ya kaboni inayotokana na miradi ya uhifadhi wa misitu, nishati safi, kilimo endelevu na usimamizi wa taka. Hii inaifanya rasilimali za mazingira kuwa sehemu ya moja kwa moja ya mfumo wa mapato ya taifa, badala ya kuwa tu suala la uhifadhi.
Ndani ya mfumo wa kisheria wa ndani, Tanzania tayari imeanza kuweka msingi wa ushiriki wake katika soko hili kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191 (Environmental Management Act) ambayo inatoa mamlaka ya kisheria ya kulinda mazingira na kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali asilia. Aidha, Kanuni za Biashara ya Kaboni za mwaka 2022 (National Carbon Trading Regulations) zinaweka utaratibu wa usajili wa miradi, uthibitishaji wa upunguzaji wa hewa ukaa na namna mapato yanavyoweza kugawanywa.
Kwa upande wa kimataifa, mfumo huu unaendana na ahadi za Tanzania chini ya Nationally Determined Contributions (NDCs) chini ya UNFCCC, ambazo zinahitaji nchi kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa kiwango kilichokubaliwa kimataifa. Hii ina maana kuwa ushiriki wa Tanzania katika soko la kaboni si chaguo la hiari tu, bali pia sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa kisheria wa kimataifa.
Katika upande wa Singapore, utekelezaji wa Carbon Pricing Act ya mwaka 2019 unaonyesha namna nchi hiyo ilivyoweka mfumo wa kodi ya kaboni kwa viwanda vinavyozalisha hewa chafu, huku pia ikijihusisha na masoko ya kimataifa ya kaboni. Uzoefu huu unaiweka Singapore katika nafasi ya mshirika wa kimkakati katika kusaidia nchi kama Tanzania kujenga mifumo ya uwazi, uthibitishaji na usimamizi wa miradi ya kaboni.
Hata hivyo, pamoja na fursa hizi, mjadala wa msingi bado unabaki kwenye namna Tanzania itakavyohakikisha kuwa mifumo hii ya kisheria na kimkataba inaleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi. Bila utekelezaji thabiti, kuna hatari ya rasilimali za mazingira kunufaisha zaidi wawekezaji wa nje kuliko jamii zinazozilinda.
Ndiyo maana eneo hili linahitaji zaidi ya makubaliano ya kidiplomasia. Linahitaji utekelezaji wa sheria zilizopo kwa ufanisi, uwazi katika mikataba ya kimataifa, na ushirikishwaji wa wananchi katika miradi ya mazingira. Hapa ndipo nafasi ya vijana inakuwa muhimu zaidi, kwani uchumi wa kaboni unahitaji wataalamu wa mazingira, watafiti wa tabianchi, wataalamu wa data na wajasiriamali wa teknolojia za kijani.
Kwa ujumla, Tanzania iko katika wakati muhimu wa kihistoria. Mfumo wa sheria wa kimataifa kupitia Mkataba wa Paris, pamoja na sheria zake za ndani za mazingira na kanuni za kaboni, unaipa nafasi ya kuwa mchezaji muhimu katika uchumi wa kijani duniani. Lakini mafanikio yake yatategemea si tu makubaliano yaliyosainiwa, bali uwezo wa kuyageuza kuwa matokeo halisi kwa wananchi na vizazi vijavyo.
0 Comments